25.9 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 6, 2022

Contact us: [email protected]

Wafanyakazi 597 waachishwa NIDA

NIDANa Elizabeth Hombo, Dar es Salaam

MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imesitisha mikataba ya wafanyakazi wake 597 kwa kile kilichodaiwa kuwa bajeti ndogo ya kuwalipa.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Dk. Modestus Kipilimba, ilisema kuwa hatua hiyo imetokana na mamlaka hiyo kutokuwa na bajeti ya kutosha ya kuwalipa wafanyakazi hao.

“NIDA imesitisha mikataba yote ya wafanyakazi wa mkataba waliopo katika ofisi zetu zote nchini; hii ni kutokana na mahitaji ya watumishi na bajeti kwa hali ya sasa NIDA hatuna bajeti ya kuendelea kuwalipa wafanyakazi ambao idadi yao ni 597,”ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Dk. Kipilimba katika taarifa hiyo alieleza kuwa sababu nyingine ni kubadilika kwa mpango kazi wa mamlaka ambao kwa sasa hatua zote za usajili zitafanyika katika ngazi ya wilaya.

“Hivyo kwa idadi ya watumishi waliopo kwa masharti ya kudumu inakidhi kuendelea kukamilisha kazi iliyokusudiwa ngazi za wilaya kwa kushirikiana na watendaji wa vijiji na mitaa.

“Hatua hii pia ni mwendelezo wa mpango wa mamlaka wa kurekebisha maeneo ambayo yanahitaji mabadiliko makubwa ili kuendana na kasi ya serikali ya awamu ya tano ya Hapa Kazi Tu.

“ NIDA inapitia upya mikataba yote ya huduma ambayo ilifanya kwa wadau mbalimbali kujiridhisha kama taratibu zote za kisheria zilifuatwa na kwa ile ambayo itabainika haikufuata sheria itasitishwa mara moja,”alisema.

Januari 25 mwaka huu, Rais John Magufuli alitengua uteuzi wa mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Dickson Maimu na kuwasimisha maofisa wengine wanne wa mamlaka hiyo ili kupisha uchunguzi wa namna Sh bilioni 180 zilivyotumika wakati wananchi waliopatiwa vitambulisho vya taifa ni wachache.

Maofisa hao waliosimamishwa kazi ni pamoja na Mkurugenzi wa Tehama, Joseph Makani, Ofisa Ugavi Mkuu, Rahel Mapande, Mkurugenzi wa Sheria, Sabrina Nyoni na George Ntalima ambaye ni Ofisa Usafirishaji.

Kutokana na hilo, Rais Magufuli aliielekeza Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA), Taasisi ya Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalumu wa manunuzi yote yaliyofanywa na NIDA.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,603FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles