25.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 16, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali kusimamia shughuli za Uchumi wa Buluu

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Serikali imesema itaendelea kusimamia na kuratibu kwa ufanisi shughuli za Uchumi wa Buluu nchini ili kuhakikisha wananchi wananufaika kwa kutumia rasilimali hizo kwa ukuaji wa uchumi na maendeleo endelevu.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk. Ashatu Kijaji wakati wa Kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira cha kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mkakati wa Utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uchumi wa Buluu ya mwaka 2024 kwa kipindi cha Julai hadi Oktoba 2024 pamoja na taarifa ya utekelezaji wa Mkataba wa Nairobi wa Hifadhi ya Mazingira ya Bahari jijini Dodoma leo Oktoba 16, 2024.

Amesema katika kuhakikisha usimamizi huo unafanikiwa, Ofisi ya Makamu wa Rais imeandaa mapendekezo ya uanzishwaji wa Idara ya Maendeleo ya Uchumi wa Buluu itakayokuwa na jukumu la kuratibu, kufuatilia na kufanya tathmini ya utekelezaji shughuli zote za sera hiyo.

Katika kuhamasisha matumizi endelevu ya rasilimali za maji, Dk. Kijaji amefafanua kuwa Serikali itaandaa mpango wa matumizi ya maeneo ya rasilimali za maji ambapo mwongozo wa maandalizi ya Mpango wa Matumizi ya Maeneo ya Rasilimali za Maji wa mwaka 2023 umeandaliwa.

Aidha, Waziri Dk. Kijaji amesema Ofisi imeandaa maandiko 13 kwa ajili ya kuyawasilisha kwa wadau wa maendeleo ili kupata fedha zitakazosaidia katika utekelezaji wa miradi ikiwemo ile ya uchumi wa buluu.

Katika hatua nyingine, amesema kutokana na Tanzania kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Sekretarieti ya Mkataba wa Nairobi na kuwa mwenyeji wa mkutano wa 12 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Nairobi, nchi inatarajia kunufaika na fedha za miradi ya maendeleo.

Dk. Kijaji ametaja manufaa mengine kuwa ni kutangaza fursa za uwekezaji kwa wadau mbalimbali kupitia fursa zilizopo nchini katika nyanja ya Uchumi wa Buluu ambao tayari Serikali imeshaanda Sera yake.

“Lengo kuu la Mkataba wa Nairobi ni kudhibiti uchafuzi wa mazingira ya ukanda wa pwani na bahari kutokana na vyanzo na shughuli zinazofanyika nchi kavu na kuwezesha nchi wanachama kushirikiana katika kuandaa na
kutekeleza mipango na mikakati ya pamoja ya kuhifadhi, kusimamia na kuendeleza mazingira ya ukanda wa pwani na Bahari ya Hindi,” amefafanua.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira Jackson Kiswaga ametoa pongezi kwa Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuwa na mikakati endelevu ya kuhifadhi mazingira.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles