25.4 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

SERIKALI: KUNA USHINDANI MKUBWA MAKAA YA MAWE

Na Shermarx Ngahemera


SERIKALI imesema hakuna kuanguka kwa mahitaji ya saruji nchini kwa kutumia kigezo cha ununuzi wa makaa ya mawe kutoka kampuni ya Tancoal, kwani si chanzo sahihi cha habari na si msemaji wa masuala ya saruji.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, kujibu hoja ya mwandishi wa habari kuwa mauzo ya makaa yamepungua Tancoal ikiwa ni kielelezo kuwa mahitaji ya saruji ni madogo na hivyo kupunguza mahitaji ya bidhaa ya makaa ya mawe kwa viwanda husika.

“Si kweli kuwa mahitaji ya saruji yamepungua bali yako vilevile na inategemewa kuongezeka na kuthibitisha kuwa kupungua mauzo ya makaa ya mawe chini ya kawaida yanayoonekana kwa Tancoal, ni matokeo ya ushindani katika soko la ndani kutokana na kuanzishwa uzalishaji wa migodi mingine mitatu nchini na hivyo kuongeza ushindani wa soko,” alisema Mwijage.

Alifafanua kuwa migodi mitatu iliyoanzishwa mwaka huu ni pamoja na ule wa Kampuni ya Taifa ya Uchimbaji Madini (Stamico). Anasema taharuki hiyo inatokana na ukweli kuwa Tancoal ilikuwa pekee katika biashara hiyo na hivyo kuhodhi soko lakini sasa kuna ushindani kila pembe.
Rekodi zinaonesha kuwa ukiachana na Tancoal, migodi mingine ni Kiwira Songwe Coal &Power Mine, Kibo Mining na Rukwa Coal (Edenville).

Alitoa angalizo kuwa kazi ya serikali ni kuwezesha uanzishwaji wa migodi lakini watu au kamapuni binafsi kuendesha na kufanya uzalishaji mali na hivyo kuitaka kampuni ya Tancoal kusimama kidete kwenye ushindani huo mkali na kuwa na mikakati mizuri ya mauzo.

Alisema kuwa kwa miaka mingi makaa ya mawe yalikuwa yanaagizwa nchi za nje, lakini sasa hiyo ni historia kwani nchi imeazimia kujitegemea kwenye hilo kwa kuanzisha migodi mingi na itajihusisha vilevile kuzalisha nishati ya umeme na kuwekwa katika gridi ya taifa.

Kwa uchumi wa kileo ununuzi na uuzaji wa vifaa vya msingi vya ujenzi ni kigezo kinachotumika na wachumi kama mwenendo wa uchumi wote na ukuaji wake. Hivyo basi, matumizi ya saruji ni kigezo tosha kuonesha kupanda au kushuka kwa uchumi husika.

Lakini kupungua matumizi ya saruji kunaweza kuwepo kwa mengi na si kuwa uchumi husika umepatwa au kufambatwa na ukuaji wake, kutokana na maelezo ya wanauchumi katika Chuo Kikuu cha Dares Salaam (UDSM).
Akitoa maoni yake anasema wakati mwingine ni hali ya muda tu kutokana na mzunguko wa bajeti ya Serikali na hivyo, kutegemea mzunguko mpya mwezi Julai mambo yanaweza kupanda tena.

Masuala ya ujenzi yana miradi mingi ikiwamo Makao Makuu Dodoma na Bomba la Mafuta Ghafi la Uganda (East Africa Crude Oil Pipeline) toka Hoima Uganda hadi Bandari ya Tanga nchini.

Katika tamko lake kwa vyombo vya habari, Tancoal imesema kuwa imezalisha tani 49,154 za makaa ya mawe mwezi Juni ikiwa mara mbili ya uzalishaji wake wa mwaka jana katika muhula kama huu na kuuza tani 45,320 tu na kubakia na tani 3,824.

Kampuni hiyo huuza bidhaa yake katika nchi za Kenya na Rwanda tani zisizopungua 10,000 (tpm) kwa mwezi na inategemewa kupanda hadi tani 18,000 kuanzia Septemba mwaka huu kwa masoko mapya ya nchini Zambia, Uganda , Kenya na Madagascar.

Tancoal vilevile ilithibitisha kuwa haijaathirika sana na mabadiliko ya Sheria Mpya za madini zilizopitishwa hivi karibuni katika udhibiti, sheria, mambo ya kifedha na uendeshaji sheria tatu ambazo zililenga zaidi kwenye dhahabu na vito na kutoruhusu kuweka fedha nje ya nchi.

Mwezi Juni mwishoni Serikali ilifanya mapitio makubwa ya sheria za madini kufuatia kasheshe ya makinikia ya Kampuni ya Acacia kukwepa kodi na kuibia Serikali mapato yake kwa kudanganya kilichomo kwenye makinikia hayo.

Mabadiliko hayo ya Sheria ya Madini na Nishati yataiwezesha Serikali kumiliki machimbo hayo na kujadili upya mapatano ya uendelezaji wa migodi (MDA).
“Hayo ni mabadiliko makubwa na yataathiri kwa kiasi kikubwa shughuli za uchimbaji madini nchini na hivyo kuzuia au kupunguza uwekezaji katika sekta hiyo,” inasema taarifa ya Tancoal.

Hata hivyo, Tancoal inamilikiwa na Serikali kupitia NDC kwa asilimia 30 na haina MDA, kwani ilikuwepo kabla ya mahitaji hayo na hivyo hayatahusu Intra Energy Corporation (IEC) na mgodi wa Ngaka Coal Mine ambapo kuna mpango wa kuzalisha nishati ya umeme wa MW 300 kuuzwa gridi ya ataifa.

Tancoal ni Kampuni ya Ushirikiano (JV) kati ya kampuni ya Austria ya Intra Energy Corporation kwa asilimia 70 na NDC asilimia 30.
Mvua nayo ni sababu tosha ya kupunguza mauzo kwani migodi iliko huwa haifikiki kirahisi wakati wa mvua na hivyo kuleta mdororo unaosemwa na Tancoal.

Hata hivyo, mwezi Mei wakati wa ukaguzi wake Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) illionya juu ya mwenendo usioridhisha wa ukuaji uchumi na kudai juhudi ifanyike.

Serikali ilipiga marufuku kuleta makaa ya mawe toka nje mwezi Agosti mwaka jana ili kufanya viwanda vya saruji vinunue bidhaa toka migodi ya ndani.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles