25.3 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Serikali kumsaidia Mbwana Samatta kutangaza utalii kimataifa

MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

SERIKALI itaendelea kumsaidia kwa hali na mali nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, anayechezea Klabu ya Genk ya nchini Ubelgiji, Mbwana Samatta ili kuhakikisha kuwa anafungua milango ya uwekezaji na kuiweka juu ramani ya Soka la Tanzania katika anga la kimataifa.

Akizungumza na Nahodha huyo, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi amesema Samatta ameonyesha njia iliyoshindwa kufikiwa na wachezaji wengi wa miaka ya nyuma waliojaribu kucheza Soka la kulipwa katika vilabu mbalimbali vya nchi za nje hususani bara la Ulaya.

Dk Abbasi amesema serikali imemteua Sammatta kuwa Balozi wake wa Utalii kutokana na mafanikio makubwa za mchezaji huyo nje ya mipaka ya Tanzania kwa kuwa Serikali ina Imani naye katika kufungua milango ya fursa za uwekezaji hususani katika miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano hapa nchini.

Kwa mujibu wa Dk Abbasi amesema kwa sasa yapo mambo makubwa na mazuri hususani vivutio vya sekta ya utalii, hivyo kupitia nafasi yake ya ubalozi serikali itatoa msaada wowote unaohitajiwa na mchezaji huyo ili kuhakikisha kuwa vivutio vya Tanzania vinabainishwa na hivyo kutangaza mambo mazuri ya Tanzania.

Aidha Dk Abbasi amesema Ofisi yake imeandaa mikakati mbalimbali ya mawasiliano ya kitaifa katika maeneo mbalimbali hivyo amemtaka mchezaji huyo kutumia majukwaa hayo kwa ajili ya kuona namna bora ya kutumia fursa hizo ili aitangaze Tanzania nje ya mipaka yake.

Kwa mujibu wa Dk Abbasi amemtaka mchezaji huyo awasiliane naye iwapo kutakuwa na changamoto yeyote wakati wa kutekeleza majukumu yake ya nafasi ya Ubalozi kwani kwa sasa Serikali ya imefungua milango ya ushirikiano na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha kuwa Tanzania inapiga hatua katika kuwaletea maendeleo wananchi wake.

Mbwana Samatta amesema akiwa nchini Ubelgiji tayari amefanya juhudi kubwa katika kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini, ambapo mwanzoni mwa mwezi ujao madaktari watano wa timu hiyo wanatarajia kuja nchini kwa ajili ya kutembelea maeneo mbalimbali ya utalii hapa.

Samatta amesema raia wengi wa kigeni wana shauku ya kutembelea Tanzania kutokana na kuona uzuri wa vivutio mbalimbali vya utalii ikiwemo wanyama, hivyo akiwa balozi wa Utalii atafanya kila liwezekanalo  kukaa karibu na viongozi na wachezaji wa klabu ya KRC Genk kuwaeleza uzuri wa Tanzania ili na wao waonyeshe nia ya kuitembelea Tanzania.

“Wachezaji wengi hususani wale wa kiafrika waliopo nje wanaipenda sana Tanzania na hi ni kutokana na sifa tuliyonayo na hivyo kwa kutumia nafasi yangu ya ubalozi nitaendelea kushawishi waitembelee Tanzania,” amesema Samatta.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya Utalii ya Samatta Tours, Hamis Waziri ameishukuru serikali kutokana na jitihada mbalimbali inazofanya kwa ajili ya kuhamasisha sekta ya utalii nchini na kusema taasisi hiyo itakuwa tayari kutangaza matukio mbalimbali kwa ajili ya kulitangaza jina la Tanzania.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles