23.3 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 21, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali kujenga maabara za muda Taasisi ya Sayansi za Bahari Zanzibar

Na Jestina Zauya (TUDARCo), Zanzibar

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako, amesema Wizara itahakikisha Taasisi ya Sayansi za Bahari ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam iliyoko Zanzibar inajengewa Maabara za muda na kuwekewa vifaa baada ya moto kuteketeza maabara zote.

Moto ulioteketeza na kuunguza na vifaa ulitokea Oktoba 2, mwaka huu.

Profesa Ndalichako amesema ujenzi huo unafanyika haraka ili kuwezesha wanafunzi kuendelea na masomo watakapofungua chuo.

Akizungumza mjini Zanzibar Oktoba 4, 2021 baada ya kukagua uharibifu uliotokea kwenye jengo la maabara la Taasisi hiyo lililoko eneo la Mizingani Bandarini, Waziri Ndalichako amesema pamoja na kujenga maabara za muda Wizara ina mpango wa kujenga maabara za kudumu na kwamba tayari Serikali kupitia Wizara ilishatoa Shilingi bilioni moja kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa maabara mpya, hivyo ameagiza sehemu ya fedha hizo zitumike kununua vifaa muhimu vya maabara zitakazotumika kwa muda.

Alisema Wizara inaendelea kutekeleza kwa vitendo maono ya Rais ya kuhakikisha elimu ya Tanzania inatoa vijana wenye ujuzi katika eneo hilo la sayansi za bahari na ndio maana wiki iliyopita wametoa kwa Taasisi hiyo Shilingi bilioni moja kwa ajili ya kukamilisha maabara mpya.

Aidha, Prof. Ndalichako amemuagiza Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa William Anangisye kuhakikisha Chuo kinafunguliwa Oktoba 25, 2022 kama ilivyopangwa ili kutoathiri mzunguko wa Mwaka wa Masomo na kuwataka wanafunzi wa Chuo hicho kutokuwa na hofu .

Ndalichako ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Jeshi la Polisi, Idara ya Zimamoto kikosi cha Bandarini na Kamisheni ya Maafa iliyoko chini ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar pamoja na Raia wema kwa kazi kubwa ya kudhibiti na kuzima moto huo.

Kwa upande wake Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Simai Mohamed Said amemshukuru Prof. Ndalichako kwa kufika katika eneo hilo na kuahidi kushirikiana na chuo hicho kuhakikisha shughuli za Masomo zinaendelea kutokana na umuhimu wa Taasisi hiyo kwa uchumi wa nchi.

“Sote tunatambua umuhimu wa Taasisi hii ambayo ni chachu na kitovu cha kuimarisha uchumi wa Buluu na maabara hizi zilikuwa tegemeo si kwa Tanzania tu bali hata nchi za jirani hivyo tutashirikiana kuhakikisha zinarejea katika kipindi kifupi,” amesema Simai.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles