25.9 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali kuanza ujenzi wa reli, matawi liganga na mchuchuma

Na Elizabeth Kilindi-Njombe

SERIKALI inatarajia kuanza ujenzi wa reli kutoka Mtwara hadi Mbambabay, huku matawi yakielekezwa Mchuchuma na Liganga wilayani Ludewa mkoa wa Njombe yanapopatikana madini ya makaa ya mawe na chuma ili kurahisisha zaidi usafirishaji wa madini hayo.

Hayo yamebainishwa na makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni mgombea mwenza wa kiti cha Urais kupitia chama cha mapinduzi (CCM) Samia Suluhu Hassan, alipokuwa wilayani Ludewa kwa ajili ya kampeni za chama hicho.

“Katika kuupa nguvu mradi (Liganga na Mchuchuma) Serikali tunakwenda kujenga reli kutoka Mtwara hadi Mbambabay, Lakini matawi ya reli yatakwenda Mchuchuma na Liganga, lengo ni kurahisisha usafirishaji wa chuma,”alisema Samia.

Aidha Samia alisema mradi wa Liganga na Mchuchuma umechelewa kuanza kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo urekebishwaji wa mikataba. 

“Mchuchuma na Liganga ni mradi ambao umekaa muda mrefu haujaanza lakini ni imani yetu kwamba miaka mitano inayokuja mradi utaanza na katika kuendeleza mradi ule,tutaufanyia kazi kwa pamoja baina ya serikali na sekta binafsi,”alisema.

Kuhusu fidia kwa wananchi wanaopakana na miradi alisema; “Tulikuwa na mazungumzo ya muda mrefu na mwekezaji, tumeelewana sasa mambo yako vizuri na kwa upande wa fidia, mkataba wa mradi unataka fidia ilipwe na mwekezaji, lakini kuna ujanja umefanywa kuonyesha fidia ilipwe na serikali sasa hapo tunaendelea na mazungumzo,” alisema Samia.

Awali kabla ya ufafanuzi wa mradi huo ambao umekuwa ukizungumzwa na kutegemewa na wakazi wa Wilaya ya Ludewa,mgombea wa ubunge wa jimbo hilo Wakili Joseph Kamonga,aliposimama mbele ya wananchi kwa ajili ya kuomba kura alieleza miradi mingi inayofanywa na serikali katika wilaya hiyo huku akigusia mradi huo wa Liganga na Mchuchuma.

“Upo mradi mkubwa wa makaa ya mawe,Mchuchuma na Liganga ulifanyika thamini kwa maana ya kulipa fidia lakini kwa bahati mbaya wananchi bado hawajalipwa fidia toka 2015, lakini wananchi wanasema bado wana imani ya kulipwa fidia zao kwa kuwa wanajua uzalendo wa rais wetu” alisema Kamonga.

Pia aliiomba serikali kuangalia uwezekano wa kutumia maji ya Ziwa Nyasa ili kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji jimboni humo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles