Na FARAJA MASINDE
SERIKALI ya awamu ya tano inajitahidi kufanya kila linalowezekana ili kuhakikisha kuwa wanafunzi kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne wanapata elimu bure, mpango ambao ulianza kutekelezwa Januari mwaka huu nchini kote.
Mkakati huo wa serikali umekuwa ni katika kile ilichodhamiria kwamba watoto wote wanaostahili kwenda shule wanapata elimu hiyo bila ya kutozwa gharama yoyote, kwa lengo la kuhakikisha nchi inazalisha na kuandaa wataalamu wengi wa kutosha katika fani mbalimbali.
Awali ilibainika kuwa watoto waliokuwa wakipata elimu bora ni wale tu waliokuwa na haki ya kupata elimu walikuwa ni wale tu ambao familia au wazazi wao walikuwa na uwezo wa kuwagharimia mahitaji muhimu ya shule ikiwamo ada ya kila mwaka.
Changamoto hii hasa ilikuwa ikiwakabili wanafunzi wengi waliokuwa wakichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza na hivyo kujikuta wengi wakiishia njiani au hata kukacha kabisa masomo na kujitumbukiza kwenye masuala mengine ikiwamo kuolewa, kutumia dawa za kulevya na mambo mengine yasiyofaa.
Itakumbukwa kuwa mwishoni mwa mwaka jana Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, alitoa agizo kwa wazazi wote ambao watashindwa kuwapeleka shule watoto wao serikali haitaacha kuwachukulia hatua kali za kisheria.
Namnukuu: “Kwa mzazi yeyote ambaye atasababisha mwanafunzi kuacha masomo au kuhudhuria kwa namna yoyote ile atambue fika kuwa lazima atachukuliwa hatua kali za kisheria kwani atakuwa anarudisha nyuma jitihada za serikali za kuhakikisha kuwa inakuwa na taifa la watu wasomi na wenye uelewa,” anabainisha Masaju.
Kauli hiyo pia imeungwa mkono hivi karibu na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambapo alipigilia msumali akisema kuwa serikali haitavumilia kuona mamia ya vijana waliofaulu mitihani ya darasa la saba na kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wakibaki nyumbani eti kwa sababu hakuna madarasa ya kutosha.
“Serikali haitaridhika kuona vijana waliofaulu vizuri wanashindwa kwenda kidato cha kwanza, halmashauri si ilishajua tangu mapema ni wanafunzi wangapi wanaenda shule za msingi… kwa hiyo nataka kuona wote waliofaulu wanakwenda sekondari kwa asilimia 100,” anabainisha.
Waziri Majaliwa anasisitiza kuwa serikali imedhamiria kutoa elimu bure kwa kila mtoto na kwamba litakuwa ni jambo la kushangaza kuona watoto wengine wakifaulu na kushindwa kujiunga na elimu ya sekondari.
“Tumesema elimu ni bure hakuna sababu ya kufanya wengine wasiende shule wakati azma ya serikali ni kutoa elimu ya bure, hivyo hakikisheni wote wanaingia katika chagua la kwanza,” anasema Waziri Majaliwa.
Majaliwa alitoa kauli hiyo hivi karibuni alipokuwa akizungumza na viongozi na watendaji wa Mkoa wa Lindi mara baada ya kupokea taarifa ya mkoa huo kwenye Ikulu ndogo wilayani Nachingwea.
Pia anawataka wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri ambazo zimefaulisha wanafunzi lakini hazina madarasa na madawati ya kutosha warudi mezani na kujipanga upya ili kuhakikisha wanafunzi wote waliofaulu wanapangwa na kuanza na wenzao katika chaguo la kwanza…
nasema wakisubiri chaguo la pili watakuwa wamechelewa na hivyo kuwa nyuma kimasomo.
Kwa mara ya kwanza Tanzania ilifuta ada kwa wanafunzi wa shule za msingi mwaka 2002 ambapo hali hiyo ilisaidia kuongeza kiwango cha uandikishwaji wa wanafunzi kwa asilimia 94 kujiunga na darasa la kwanza.
Licha ya kuondolewa kwa ada hizo bado wazazi walikuwa na jukumu la kuchangia huduma za ziada kama vitabu na sare za shule hali ambayo ipo pia kwenye shule za sekondari kwa sasa.
Ni wazi kuwa kwenye nchi masikini kama Tanzania, kilimo ndio imekuwa uti wa mgongo kwa asilimia 80 ambapo watoto wamekuwa wakitumika kama nguvu kazi ya kulifanikisha hilo kwenye familia nyingi na hivyo kujikuta kwamba watoto wengi wakizuiwa kuendelea na masomo hasa ya sekondari, badala yake hulazimisha kushiriki kwenye shughuli za kilimo.
“Nilikuwa na haki ya kuendela na elimu yangu ya sekondari lakini sikufanikiwa baada ya kuona kwamba hakukuwa na mtu wa kuweza kumudu kunilipia gharama za masomo, wazazi wangu walikuwa hawana uwezo wa kunilipia ada.
“Nililazimika kukimbilia Dodoma mjini baada ya kushawishiwa na rafiki yangu ambaye naye alishindwa kuendelea na masomo baada ya wazazi wake kufariki… akaniambia kuwa nikienda mjini sitakosa kazi ya kufanya, nilimsikiliza nikamfuata hadi Dodoma ndipo nilipoanza kuuza zabibu kwenye stendi ya magari makubwa nikiwa na nia ya kuweka fedha kwa ajili ya kujisomesha.
“Azma yangu ya kutaka kujiendeleza haikufanikiwa baada ya kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwamo wazazi kunitegemea mimi kwa kila kitu.
“Kwa sasa nafanya kazi ya kuuza vitu vidogovidogo kama pipi, lakini pia nanunua fedha chakavu pamoja na dola hapa eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam angalau nimudu kuendesha maisha,” anasema Geofrey Mdimu (23) si jina lake halisi.
Mdimu alitamani kurejea shule baada ya kusikia elimu inatolewa bure, lakini anapshindwa kwa sababu familia yake huko kijijini inamtegemea yeye.
Katiba ya nchi kama Uganda ambayo ni miongoni mwa nchi zinazotoa elimu bure, inasema kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa mzazi ambaye atamnyima mtoto haki ya kupata elimu. Hii ni tofauti na Tanzania ambako hakuna hatua sheria ambazo zimewekwa kwa ajili ya kupambana na aina hiyo ya wazazi wasiopeleka watoto wao shule.
“Iwapo mzazi mmoja au wawili wataadhibiwa kwa kosa la kushindwa kupeleka watoto wao shule ni wazi kuwa litakuwa ni fundisho ambalo litafanya wengine pia kutii maagizo yanayotolewa na serikali,” anasema Grace Mshaba ambaye ni Mwenyekitio wa Chama cha Girl Guide Tanzania kinachojishughulisha na kutetea haki za wanafunzi wa kike nchini hususan ambao wazazi wao wamekuwa wakiwatumia kwenye masuala ya ulevi.
Anasema katika utafiti waliofanya mwanzoni mwa mwaka huu kwenye maeneo ya Jiji la Dar es Salaam, wame baini kuwapo kwa baadhi ya watoto ambao wamekosa haki yao ya msingi ya kupata elimu kutokana na wazazi kuendekeza pombe.
“Maeneo kama Mabibo, Tabata ni miongoni mwa sehemu ambazo watoto wengi wapo nyumbani kutokana na wazazi wao kujikita kwenye pombe na hivyo wamejikuta wakikosa haki yao ya msingi ya kwenda shule.
“Tatizo hili hasa limekuwa likichangiwa kwa kiasi kikubwa na wazazi kwani pindi wanapopata fedha wamekuwa wakiishia kulewa na kusahau kutimiza mahitaji ya msingi ya mtoto kama kumpatia elimu,” anasema Grace.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) linaeleza kuwa kiwango cha watoto ambao wameshindwa kupelekwa shule na wazazi wao kilikuwa milioni 2.4 kwa mwaka 2013 kwenye nchi za ukanda wa jangwa la Sahara.
Idadi ambayo inakadiriwa kufikia milioni 30 kwa sasa katika Bara la Afrika, huku duniani ikiwa ni milioni 59.
Sababu nyingi ambayo inatajwa kama chanzo cha changamoto hizo ni pamoja na kukosekana kwa vifaa vya kutosha vya kufundishia kwenye shule za sekondari ikiwamo vitabu, mazingira yasiyokuwa rafiki licha ya kuwapo kwa madawati ya kutosha.
Robert Jordan wa Shirika lisilokuwa la kiserikali la ATD Dunia ya Nne, anabainisha kuwa changamoto nyingine mbayo bado inawakabili wanafunzi wengi kwa sasa kushindwa kupata elimu licha ya kuwapo kwa madawati ya kutosha shuleni ni pamoja na umasikini uliokithiri.
“Katika moja ya tafiti zetu tumebaini kuwa watoto wengi wamejikuta wakikosa haki yao ya kupata elimu si kwa sababu wazazi wanawazuia isipokuwa ni umasikini uliokithiri unaochangia kwa kiasi kikubwa kuwafanya wasiende shule hasa wale wanaoingia sekondari.
“Tumeangalia kwenye baadhi ya familia nyingi fedha ya chakula ni changamoto hivyo linakuwa si jambo jepesi kwa mzazi kumudu kupata nauli ya kila siku kwa ajili ya mtoto wake kwenda na kurejea shule, hapo bado hajampatia fedha ya chakula shuleni.
“Utakuta watoto wengi wanalazimika kukaa nyumbani na kufanya kazi za vibarua kwa kushirikiana na wazazi wao ili kupata fedha ya chakula licha ya kupata ufaulu mzuri, kwani wengi wanashindwa kuvumilia maisha ya kuomba omba kila siku,” anasema Jordan.