23.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 27, 2023

Contact us: [email protected]

TUWAFUNDISHE WATOTO KUJIJENGEA UWEZO WA KUFIKIRI

Na MWANDISHI WETU


wanafunzi-wa-shule-ya-awali-wakiwa-darasaniMOJA ya malalamiko katika jamii yetu ni kwamba watendaji wetu hasa serikalini wamekuwa wakifanya kazi kwa mazoea na wanashindwa kubuni majibu kwa ajili ya matatizo yetu, tena mengine ni matatizo madogo.

Jibu langu mojawapo ni kuwa tatizo lilianza shuleni, walimu hawatufundishi kwa mtindo wenye kulenga kujenga uwezo wa kufikiri na kutatua matatizo (problem solving skills). Nitaeleza ufundishaji kwa mtindo wa kutatua matatizo maana yake nini na mkakati wake wa kufundisha.

Ufundishaji wa kujenga uwezo wa kutatua matatizo maana yake ni kutumia maarifa uliyonayo ili kujenga wa kugundua kile ambacho hukijui. Yaani mwalimu anaamini kuwa mwanafunzi ana hazina ya taarifa na maarifa ambayo akiitumia vizuri anaweza kupata maarifa mengine ambayo awali hakuwa nayo.

Ufundishaji kwa mtindo huu humweka mwanafunzi kwenye vikwazo ambavyo anatakiwa kuvitatua, kujenga mikakati ya kutafuta majibu, hatimaye anaweza kujua njia bora ya kupata majibu sahihi.

Mwalimu anatakiwa kufundisha kwa lengo hilo akiwa na mbinu zifuatazo. Kwanza amfanye mwanafunzi kuwa ndio mtafuta maarifa au taarifa. Mwalimu ampatie mwanafunzi orodha ya vitabu vya kusoma vyenye taarifa zinazohitajika, mwanafunzi asome na akipata taarifa hizo amweleze mwalimu ili kuona kama yuko sahihi au hapana.

Au mwalimu anamtuma mwanafunzi kwa watu nje ya shule ambao wanaweza kutoa taarifa. Kwa mfano; mwanafunzi anataka kujua namna usukani wa gari unavyofanyakazi… anampeleka kwa fundi makenika na kupewa maelezo… akirudi mwalimu anapewa taarifa na kumuuliza maswali juu ya suala hilo, ambayo mwanafunzi akijibu yote kwa usahihi, basi atakuwa amefanikiwa kumwezesha mwanafunzi kupata taarifa mpya… kama mwanafunzi hajaweza kujibu vizuri, basi atatakiwa kurudi tena kwa mtaalamu na kuuliza maswali hadi apate majibu yaliyo sahihi.

Hili likifanyika vizuri basi mwanafunzi atakuwa amejifunza mambo mapya kwa juhudi zake mwenyewe, kazi ya mwalimu inakuwa kusahihisha makosa madogo madogo, kumjengea mwanafunzi uwezo wa kuuliza maswali, na kumuwezesha kuyaweka majibu yake – yaani maarifa mapya kwa uzuri zaidi.

Anapokuja kukuelezea alichokipata basi mwanafunzi anakuwa anajitayarisha na hivyo kukuza uwezo wake wa kufikiri. Lakini inamsaidia pia kujenga uwezo wake wa kuamua jambo. Wanapokuwa kwenye kikundi na kugawana majukumu juu ya kazi uliyowaachia, wanajifunza kuamua kwa pamoja, na kweli kutafuta majibu mazuri ya kuweza kumridhisha mwalimu. Mwalimu atatakiwa kuweka viwango vya juu kuhusu majibu na namna ya kuyawasilisha.

Mwalimu anatakiwa sasa kupitishwa kwenye hatua ya kulijua tatizo lenyewe kwa undani, na ikiwezekena mwambie alielezee tatizo lenyewe analotakiwa kulifanyia kazi kwa undani na alifanyie uchambuzi kujua linajumuisha mambo gani. Bila mwanafunzi kulielewa tatizo lenyewe hataweza kulitatua kwani hatajua pa kuanzia, na vipengele vyake hatavijua.

Akishaweza kulijua tatizo hilo ni rahisi kutambua vikwazo ambavyo vinaweza kumkwamisha na kushindwa kulitatua kazi yake kwa uzuri. Na umwulize anawezaje kuvitatua vikwazo vyake. Kwa mfano; anataka kujua historia ya eneo fulani na kuna bibi ambaye anaijua historia hiyo lakini hataki usumbufu je, watafanya mbinu gani hadi waweze kumfanya bibi huyo azungumze? Wakiwa kwenye kundi na kujadili, wanaweza kuja na majibu ya mbinu za kulitatua tatizo hilo.

Mwalimu unaweza sasa kuwatayarishia mazingira mbalimbali ambayo wanaweza kukutana nayo na kwa hiyo wajitayarishe nayo ili kuweza kupata mbinu mbadala kama moja itashindwa. Na hili ni jambo muhimu sana kwa wanafunzi, kuwa na njia mbadala ya kutatua tatizo kama moja itashindwa, wanafunzi wajengewe uwezo wa kujua hilo- yaani kuna njia mbadala katika kila kikwazo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,729FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles