Serikali imezitaka taasisi zote kujiunga katika matumizi ya Kituo cha Taifa cha Kutunzia Kumbukumbu (Internet Data Center) ili kupunguza gharama kubwa za utunzwaji wa ‘data’ wanazolipia nje ya nchi.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Edwin Ngonyani, lengo la kujenga kituo hicho ni kutunza ‘data’ nchini kwani ni salama zaidi kuliko nje ya nchi ambapo baadhi ya watu wasio waaminifu wanaweza kusambaza data zako bila wewe kujua.
“Kutokana na kuwepo kwa kituo hiki kutakuwa na gharama ndogo za kulipia huduma ikiwa tofauti na nje ya nchi ambako wanalipia gharama kubwa kutasaidia kuongeza pato la Taifa,”alisema Mhandisi Ngonyani.
Alisema kituo hicho kinauwezo mkubwa wa kutunza data na kuwa ujenzi wa kituo hicho umegharimu shilingi bilioni 77 na bado gharama zinaendelea kuongezeka .