33.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali imepeleka wapi fedha za umeme?

pic+muhongoKATIKA miezi yake ya kwanza serikali ya awamu ya tano imejinasibisha kwa mambo kadhaa. Moja kati ya mambo hayo ni udhibiti mkubwa wa rasilimali za taifa. Serikali imeonyesha kuwa inadhamiria kuhakikisha kuwa rasilimali za nchi haziwanufaishi wachache, bali zinatumika kwa manufaa ya watanzania wote.

Hilo linaonekana katika hatua za serikali kupambana na ubadhirifu na wizi wa mali ya umma, ufisadi na rushwa. Katika hili tumeshuhudia watu kadhaa wakiwajibishwa, katika mtindo ule maarufu wa kutumbua majipu.

Lakini pia hilo limeonekana katika kukua kwa makusanyo ya serikali. Katika kipindi cha miezi michache iliyopita tumeshuhudia mapato yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) yakiongezeka kwa kiasi kikubwa na kuna mwezi makusanyo hayo yalifikia Sh trilioni 1.4. Hizi ni juhudi kubwa sana.

Lakini tumeshuhudia pia kuwa serikali, hasa uongozi wa juu, ukiongoza kwa kutoa uamuzi ambao unatoa ishara kubwa kuwa kuna lengo si tu la kubana matumizi ya serikali, bali kuhakikisha kuwa kile kidogo kilichokusanywa kinatumika ipasavyo.

Naamini kuwa hatua hizo zilichukuliwa baada ya kubaini kuwa hakutakuwa na maana yoyote kwa serikali kukusanya fedha nyingi lakini ikazitumia kwa kuzitapanya. Makusanyo hayo mengi hayatawasaidia watanzania. Iwapo hakutakuwa na nidhamu katika kutumia kile kilichokusanywa, malengo mengi ya kufikia maendeleo hayatafikiwa.

Ingawa bado kuna kasoro nyingi katika utendaji wa serikali, lakini kwa ujumla kile kilichofanywa na serikali kimetoa ujumbe wa nini hasa serikali ya awamu ya tano inakusudia kukifanya kwa ajili ya nchi na wananchi wake.

Kutokana na kasoro zilizopo, malengo hayo yanaweza yasifikiwe kwa kasi ambayo itawaridhisha watanzania wengi. Lakini iwapo kila mtu atahakikisha kuwa anatimiza wajibu wake pale alipo, naamini kuwa malengo haya yanaweza kufikiwa, tena kwa urahisi. Na pale yatakaposhindwa kufikiwa, kila mtu atafahamu ni kwanini hali kama hiyo imejitokeza.

Kikubwa ambacho kitasaidia malengo yaliyoonyeshwa na serikali yanafikiwa, ni kuweka mfumo endelevu na wa kitaasisi wa kuhakikisha malengo hayo yanafikiwa. Hatutafanikiwa kufikia malengo yaliyopo iwapo tu juhudi za kupambana na ufisadi, kuboresha makusanyo na kuweka nidhamu ya matumizi itakuwa ikifanywa na viongozi wachache, hasa wale wa juu.

Tumeshuhudia katika miezi hii michache, Rais na Waziri Mkuu wakihangaika kuonyesha hayo. Ni kweli kuwa juhudi zao zimezaa matunda ambayo yameanza kuwafurahisha watanzania kwa sababu yanaonyesha sura ya Tanzania mpya, yenye neema ikianza kuonekana.

Lakini, iwapo tutaendelea kuwaachia hawa wawili waendelee kuyafanya yale ambayo wamefanya, haitashangaza kuwa wanachokifanya kikageuka kuwa nguvu ya soda.

Kama binadamu, kuna uwezekano mkubwa wakafika mahali wakachoka na hivyo kama hakutakuwa na mfumo endelevu wa kitaasisi wa kuyafanya yale ambayo Rais na Waziri Mkuu wamedhamiria kuyafanya kwa ajili ya nchi, mambo hayo yatakoma.

Na iwapo yatakoma, wote tunafahamu nini kitakachotokea. Kwa ufupi, tutarudi kule ambako tunatoka hivi sasa.

Kutokuwepo kwa mfumo endelevu na wa kitaasisi wa kutekeleza mambo mbalimbali kumeshaonyesha madhara yake. kwa wanaofuatilia vikao vya Bajeti mjini Dodoma mathalani, watakuwa wanafahamu jinsi ambavyo wabunge wamekuwa wakilalamikia kitendo cha serikali kuchukua fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya jambo na kwenda kuzitumia kutekeleza jambo jingine ambalo wabunge hao hawakulipitisha.

Mbaya zaidi, wabunge hao wanalalamika kuwa kuna fedha nyingine ambazo zimehamishwa kutoka kwenye eneo zilikokuwa zimetengwa na hazijulikani zimepelekwa wapi. Kinachosikitisha zaidi ni kuwa baadhi ya fedha hizi ziliwekewa wigo.

Mathalani, hadi hivi sasa Serikali haijatoa maelezo ni wapi yaliko mabilioni ya shilingi ambayo yalipaswa kupelekwa kwa Mamlaka ya Umeme Vijijini (REA).

Fedha hizo ziliwekewa wigo pale wabunge walipopitisha sheria ambayo inataka kodi zitakazokusanywa kwenye mafuta, Sh 100 kwa kila lita itengewe kwa ajili ya kazi ya kuambaza umeme vijijini.

Lakini cha kushangaza ni kuwa sehemu kubwa ya fedha hizo hazikupelekwa REA na serikali haisemi ziko wapi kwa sababu mafuta yalishauzwa na kodi ikakusanywa.

Hili halijatokea mwaka huu tu. Hata mwaka jana jambo kama hili lilitokea katika eneo hilohilo la umeme vijijini na wabunge wakaja juu kwanini serikali iliamua kuchukua fedha zilizowekewa wigo na kuzitumia kwenye mambo mengine.

Ni jambo la bahati mbaya sana serikali ileile inayotaka kuuonyesha umma wa watanzania kuwa imedhamiria kujenga nidhamu ya matumizi ya rasilimali za nchi, ndiyo hiyo hiyo ambayo inafanya mambo ambayo yanaanza kuzusha maswali iwapo kweli serikali hii imedhamiria kukifanya kile ambacho ilituahidi au wanataka kutupaka mafuta kwa mgongo wa chupa?

Haiwezekani kwa serikali ambayo imeshatumbua majipu ya watu kadhaa kutokana na kutowajibika kwa namna fulani, leo ikanyamaza kimya na kupatwa na kigugumizi pale inapotakiwa kujibu kuhusiana na kiasi kikubwa cha fedha ambazo zilikuwa ziende kusambaza umeme vijijini.

Jambo hili lina madhara makubwa. Kwanza linatoa picha kuwa kuna uwezekano hiki kinachokazaniwa na serikali ni nguvu ya soda. Lakini kwa upande mwingine, kushindwa kwa serikali kutoa maelezo ya kuridhisha kuhusiana na fedha za kusambaza umeme vijijini kunaweza kuwakatisha tamaa wananchi ambao wanaweza kuiona serikali hii kuwa sawa na zile zilizotangulia. Na wananchi watakaodhani hivyo hawatakuwa na makosa.

Pia, watu wanaweza kudhani kuwa zile hatua za kutumbua majipu zilikuwa ni njama za kuwalenga watu fulani fulani ndani ya serikali. Kwa maana kati ya wale waliotumbuliwa, wapo ambao maelezo yanaonyesha kuwa walisababisha ukosefu wa mapato ya serikali kwa kiasi kidogo ukilinganisha na fedha za kusambaza umeme vijijini.

Serikali inapaswa kutoa maelezo ya kina ni nini kilitokea kwa fedha hizi za kusambaza umeme vijijini. Kuna uwezekano kuwa kuuelezea ukweli kuhusu suala hilo kunaweza kuonekana kama serikali kujivua nguo yenyewe.

Lakini kufanya hivyo kutasaidia sana kujenga uaminifu wa wananchi kwa serikali yao. Watu wakiona serikali inaweza kujikosoa namna hiyo na kisha ikachukua hatua kwa wale waliosababisha makosa hayo, watazidi kuiamini kuwa imedhamiria kukifanya kile ambacho imekiahidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles