31.3 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

SERIKALI ILIVYOHENYESHA MAJANGILI

Na MAREGESI PAUL-DODOMA


WAKATI takwimu za Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (Tawiri) zikionyesha ujangili ulifanya idadi ya tembo nchini kushuka kutoka 316,300 mwaka 1979 hadi 50,443 mwaka 2015, taarifa ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, iliyosomwa bungeni jana, imebainisha jinsi Serikali ilivyoweza kupambana na wahalifu hao na kuwakamata 7,085 na silaha 23,919.

Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2017/18, Profesa Maghembe alisema juhudi za kulinda wanyamapori dhidi ya ujangili na biashara haramu, zimeendelea kuimarishwa kupitia Idara ya Wanyamapori.

“Katika mwaka wa fedha 2016/17, Idara ya Wanyamapori, Tanapa, NCAA na Tawa, iliendesha doria 349,102 ndani na nje ya maeneo ya hifadhi. Matokeo ya doria hizo ni kukamatwa kwa watuhumiwa 7,085. Meno ya tembo 129 na vipande 95 vyenye uzito wa kilo 810.03 vilikamatwa pia.

“Vielelezo vilivyokamatwa kuhusiana na matukio ya ujangili, ni pamoja na silaha za kivita 148, silaha za kiraia 1,058, magobore 406, silaha za jadi 22,307, pikipiki 189, baiskeli 214, magari 20, ng’ombe 79,831 na samaki kilo 4,043.

“Kwa upande wa kesi, zilifunguliwa katika mahakama mbalimbali 2,097 na kesi 802, zilimalizika,” alisema Profesa Maghembe.

Akizungumzia sakata la Faru John, alisema: “Namshukuru sana mke wangu na watoto wangu ambao walinifariji na mara zote walikuwa pamoja nami katika kutekeleza majukumu yangu, hasa wakati wa sakata la Faru John.”

Itakumbukwa kuwa wakati wa sakata la Faru John, maofisa watano wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) wanaotuhumiwa kushiriki kumwondoa mnyama huyo Creta ya Ngorongoro, walikamatwa kwa mahojiano ili kujua ukweli kuhusu mazingira ya kutoweka kwa mnyama huyo.

Kuhusu Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, alisema wizara yake imeweka mawe ya mipaka kati ya hifadhi na makazi ya wananchi baada ya wananchi hao kuongezeka kutoka wakazi 8,000 mwaka 1959 hadi zaidi ya wakazi 90,000 mwaka jana.

Kwa upande wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania, alisema wizara yake imeendelea kufanya utafiti wa uhifadhi wa mbwa mwitu waliokuwa hatarini kutoweka katika mfumo wa ikolojia ya Serengeti.

Kuhusu Bodi ya Utalii (TTB) ambayo imepewa jukumu la kutangaza utalii ndani na nje ya nchi, alisema mkakati wa bodi hiyo wa kuanzia mwaka 2012 hadi 2017 ambao kwa sasa unafanyiwa mapitio, umeainisha masoko ya utalii na mbinu za kuyafikia.

Chini ya mkakati huo, alisema TTB imeingia makubaliano ya ushirikiano na Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) katika kutangaza utalii ambapo jarida la ATCL liitwalo Safari Njema, limeanzishwa kutoa habari za vivutio vya utalii wa Tanzania na usafiri wa anga.

 

BAJETI

Akizungumzia maombi ya bajeti yake, Profesa Maghembe aliliomba Bunge limuidhinishie Sh bilioni 148.5 zikiwa ni ongezeko la Sh bilioni 12.8 ya fedha alizoidhinishiwa na Bunge katika mwaka wa fedha 2016/17.

 

KAMATI YA BUNGE

Wakati Profesa Maghembe akisema hayo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, iliishauri Serikali iendelee kulinda na kusimamia uhifadhi wa maliasili nchini na pia ifanye utafiti wa kutosha juu ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika huduma ya utalii iliyoanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2016/17.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Atashasta Nditiye ambaye ndiye aliyesoma taarifa hiyo, kuna mgongano wa taarifa zinazotolewa na Wizara ya Maliasili na Utalii na wadau wa utalii kuhusu VAT inayotozwa katika sekta hiyo.

“Kwa upande wa wadau hao, wanasema utoaji wa kodi hizo umepunguza idadi ya watalii na kuongeza gharama za uendeshaji na upande wa wizara wanasema utoaji wa kodi hiyo haujaathiri kwa namna yoyote sekta hiyo.

“Kwa kuwa kamati haijaweza kujiridhisha na ukweli wa kodi hiyo, ni vema Bunge lijadili suala hilo na ikiwezekana Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) akakague suala hilo na kulishauri Bunge,” alisema Nditiye.

 

NGO NGORONGORO ZIPUNGUE

Kamati hiyo pia ilishauri Serikali ifute Taasisi zisizokuwa za Serikali (NGOs), zinazofanya kazi katika Pori Tengefu la Loliondo, lililoko mkoani Arusha.

 “Kuna taasisi zisizokuwa za Serikali zaidi ya 25 ambazo zote zimejikita katika masuala ya utalii, uhifadhi na utetezi wa wananchi katika Pori Tengefu la Loliondo.

“Taasisi hizi nyingi zinamilikiwa na wanasiasa na kufadhiliwa na taasisi za kimataifa ambazo kamati haina uhakika na lengo la taasisi hizo kufadhili uhifadhi nchini mwetu,” alisema Nditiye.

 

FARU FAUSTA

Kwa upande wa Faru Fausta kamati hiyo iliitaka Serikali kuharakisha mchakato wa kufanya uamuzi wa kuokoa gharama ambazo Serikali imekuwa ikiingia kwa kumtunza faru huyo ambaye amewekwa katika uangalizi maalumu kutokana na maradhi aliyonayo na umri wake.

 

KAMBI YA UPINZANI

Kwa upande wake, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, ilisema mgogoro wa Loliondo unachangiwa na pande tatu zinazovutana ambazo ni wawekezaji, Serikali na wananchi wanaoishi katika eneo hilo.

Katika taarifa ya kamati hiyo iliyosomwa na Msemaji wa Kambi hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko (Chadema), ilionyesha kutoridhishwa na mkataba wa uwindaji unaomilikiwa na Kampuni ya Uwindaji ya kigeni ya OBC.

Kwa mujibu wa kamati hiyo, uwepo wa kampuni hiyo katika eneo hilo, ni chanzo kingine cha mgogoro kwa kuwa wafanyakazi wa kampuni hiyo wamekuwa wakiharibu mali za wananchi.

“Kwa hiyo, ili kutatua mgogoro huo, kambi ya upinzani inaitaka Serikali ieleze njia sahihi za kutatua mgogoro huo, kilomita za mraba 2,500 zilizoelezwa na Waziri Maghembe kwamba ziwe za wananchi na mifugo yao, yachimbwe mabwawa makubwa ya maji ya mifugo, itenge eneo la malisho ya mifugo, ieleze tuhuma zinazoikabili Kampuni ya OBC na pia Serikali ichunguze uhalali wa mifugo iliyoko katika eneo hilo kwa kuwa kuna taarifa baadhi ya mifugo inatoka nchini Kenya,” alisema.

Akizungumzia suala la Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika sekta ya utalii, Matiko alisema kodi hiyo imesababisha kuyumba kwa sekta hiyo kwa kuwa baadhi ya wafanyabiashara wamepunguza wafanyakazi na wamiliki wa baadhi ya hoteli wamelazimika kuziuza baada ya kushindwa kuziendesha kutokana na uwepo wa kodi hiyo.

Pamoja na hayo, kambi hiyo ililalamikia wingi wa kodi zinazotozwa katika sekta hiyo kwa kusema Tanzania ina kampuni 1,050 za utalii, lakini ni 300 tu ndizo zilizoweza kutimiza masharti ya kulipa kodi.

Kuhusu biashara ya pembe za ndovu, kambi hiyo iliitaka Serikali iimarishe ulinzi dhidi ya tembo kwa kuwa wamekuwa wakipungua kila mwaka.

“Kwa mujibu wa sensa iliyofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (Tawiri), mwaka 1979 kulikuwa na tembo wapatao 316,300, mwaka 2006 kulikuwa na tembo 136,753, mwaka 2009 walikuwapo tembo 109,051 na mwaka 2015 wanyama hao walipungua hadi 50,443.

“Kwa hiyo, tunaitaka Serikali ichukue kila hatua zinazotakiwa katika kukabiliana na majangili wa wanyama hao,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles