27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

SERIKALI ILIPASWA KUADHIBIWA BADALA YA WALIMU

Waziri Mkuu, Kassim MajaliwaTABIA ya kuwavua madaraka walimu wakuu kama sehemu ya adhabu baada ya wanafunzi kufeli mitihani limekuwa ni jambo la kawaida katika siku hivi karibuni. Kila yanapotokea matokeo mabaya kwenye mitihani, walimu ndio wanaobebeshwa lawama. Tumelishuhudia hili hata baada ya kutolewa kwa matokeo ya mitihani ya upimaji ya kidato cha pili iliyofanyika mwishoni mwa mwaka jana.

Huko mkoani Mtwara, uliotoa shule tisa kati ya kumi zilizoshika mkia katika mitihani hiyo ya kidato cha pili, walimu kadhaa wameadhibiwa kutokana na shule zao kushika nafasi za mwisho. Lakini inashangaza kuwa inapotokea shule zikafanya vizuri basi Serikali hutoka mbele na kujinadi kuwa sera zake nzuri ndio zimeleta mafanikio hayo. Ukisoma ripoti kadhaa za utendaji na mafanikio ya idara na wizara za Serikali utaliona hilo.

Inashangaza kuwa mambo yanapokuwa mabaya, walimu ndio wanabebeshwa lawama lakini mambo yanapokuwa mazuri Serikali inajibebesha sifa!

Naamini kuwa kunapaswa kuwa na mamlaka moja ya kuwajibika kuhusiana na hali ya elimu nchini na Serikali, ambayo ndiye mlezi na mwezeshaji mkuu wa sekta hiyo, inastahili wajibu huo. Serikali ndio inapaswa kusifiwa pale matokeo katika sekta ya elimu yanapokuwa mazuri lakini pia inapaswa kubeba lawama pale mambo yanapoharibika.

Serikali ndio ina wajibu mkubwa wa kuhakikisha upatikanaji wa vifaa vya kufundishia, vitabu vya kiada na ziada, walimu wa kutosha wenye ujuzi, madarasa, ofisi, maabara, nyumba za walimu na matundu ya vyoo kwa kutaja vitu vichache, ili kuhakikisha kuwa sekta ya elimu inapata na kuleta mafanikio.

Si jukumu la mwalimu kuhakikisha kuwa shule ina madarasa ya kutosha au vitabu vya kutosha. Yeye kazi yake ni kufundisha. Na ili aifanye kazi hiyo vizuri anapaswa kupewa zana bora na vitendea kazi vya kufaa. Zana na vitenda kazi hizo ndio kichocheo na kiwezeshi cha mwalimu kuifanya kazi yake vizuri.

Iwapo zana na vifaa hivyo havitapatikana, ni vigumu sana kwa mwalimu kuifanya kazi yake vizuri. Katika mazingira kama hayo, inapotokea mwanafunzi akafeli, kwa kweli kumlaumu mwalimu ni kumuonea.

Serikali, ambayo ndio imeshindwa kumpatia mwalimu zana na vifaa anavyovihitaji ili kuifanya kazi yake kwa ufasaha, ndio inapaswa kulaumiwa na kuadhibiwa.

Mwalimu aadhibiwe pale tu ambapo Serikali itakuwa imemkamilishia mahitaji yake yote na bado wanafunzi wakafeli. Lakini hizi adhabu zinazotolewa sasa ni za uonevu kwa sababu utekelezaji wa mambo yanayosababisha wanafunzi wafeli hayapo nchini ya mwalimu.

Adhabu hizi kwa walimu zitazidi kuharibu hali ya mambo. Ili kuirekebisha hali hii Serikali ilipaswa kuchukua hatua ambazo zitaleta matokeo tofauti.

Unapomshusha cheo mwalimu kwa kumuonea namna hii, kwanza unamuondolea motisha wa kufanya kazi kwa bidii kwa sababu umemuadhibu kwa kosa ambalo kimsingi si lake. Mwalimu huyu atazidi kuvurugikiwa na kushindwa kufundisha vizuri kwa sababu adhabu hiyo itamwongezea mrundikano wa mawazo kutokana na shida nyingine alizonazo dhidi ya mwajiri wake kama vile kutolipwa stahili zake kwa wakati.

Kwa kuwaadhibu walimu hawa Serikali inaweza kujiona kama imefanikiwa kuonyesha ukali wake lakini kimsingi kinachofanyika kinazidi kuiharibu sekta ya elimu nchini. Kabla ya kuwaadhibu, Serikali ilipaswa kwanza kuwasikiliza walimu hawa wakitoa sababu za hali hiyo. Kama Serikali ingefanya hivyo ingebaini kuwa kwa kiasi kikubwa yenyewe ndio kisababishi kikubwa cha wanafunzi wengi kufeli kwenye mitihani yao kwa sababu imeshindwa kuandaa mazingira mazuri ya kutoa elimu nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles