27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali ibadilishe utaratibu utoaji mikopo elimu ya juu

ndalichakobombaTAARIFA iliyotolewa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu hivi karibuni inaeleza kuwa, bodi hiyo inadai wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu zaidi ya Sh billion 119.

Bodi hiyo ilianzishwa kwa sheria ya Bunge Namba 9 ya mwaka 2004.Baadhi ya majukumu makuu ya bodi ni pamoja na kutoa mikopo kwa wanafunzi wahitaji waliodahiliwa katika masomo ya shahada au stashahada ya juu katika taasisi za elimu ya juu zinazotambuliwa na Serikali hapa nchini na nje ya nchi.
Aidha, sheria hii imeipa bodi mamlaka ya kudai na kukusanya mikopo yote iliyotolewa kwa wahitimu wa taasisi za elimu ya juu walionufaika na mikopo hiyo kuanzia mwaka 1994 ili fedha hizo ziweze kukopeshwa kwa wanafunzi wengine watakaohitaji kama mfuko wa mzunguko.

Tangu mwaka 1994, kumekuwa na awamu tatu za ukopeshaji ya kwanza ikianza kutekelezwa mwaka 1992/93 ambapo wanafunzi walitakiwa kujilipia gharama za usafiri kwenda chuoni na kurudi nyumbani, gharama za udahili na usajili pamoja na michango ya serikali za wanafunzi. Gharama hizi zilikuwa ni ndogo na kila mwanafunzi aliweza kuzimudu.

Katika awamu ya pili, mwanafunzi pamoja na kuchangia gharama zilizoainishwa katika awamu ya kwanza, alilazimika pia gharama za chakula na malazi. Gharama hizi ambazo kwa wakati huo zilifikia Sh 350,000.00 kwa mwaka zilionekana kuwa kubwa kwa wanafunzi walio wengi.

Lakini, serikali katika kuhakikisha kuwa kuna fursa sawa katika utoaji elimu ya juu, ilianzisha utaratibu wa mikopo ili wanafunzi ambao hawana uwezo wa kujigharamia waweze kukopeshwa moja kwa moja kutoka serikalini. Utaratibu huu ulianza kutumika mwaka 1994/95 na uliendelea kutumika hadi mwaka 2004/2005.

Na katika awamu ya tatu iliyoanza utekelezaji wake mwaka wa masomo wa 2005/06 baada ya kuanzishwa kwa bodi, mwanafunzi anapaswa kujigharamia pamoja na gharama zilizotajwa kwenye awamu ya kwanza na pili, gharama zote zingine za masomo, ama kwa njia ya mkopo kutoka kwenye bodi au kwa njia zake mwenyewe.

Sheria hiyo inaeleza kuwa, baada ya kuhitimu, mnufaika anapewa mwaka mmoja wa kupumua na baadaye anaanza kulipa bila riba.

Hata hivyo, ukusanyaji wa madeni umekuwa hauendi vizuri na limekuwa linatishia uhai wa bodi yenyewe kwa kunyemelewa na ufilisi jambo ambalo imeilazimu bodi hiyo kutumia nguvu ya ziada, kwa kuingia mkataba wa kukusanya madeni na makampuni ya kukusanya madeni ina maana imekubali kupoteza asilimia ya mapato yake ili iweze kumlipa mkusanyaji.

Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani, ililipa uzito suala la ukusanyaji wa madeni ya wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu. Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknalojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako aliwahi kuliambia Bunge kuwa Serikali ina mpango wa kurekebisha sheria ya bodi ili kuipa meno ya kukusanya madeni.

Hatua mbalimbali tayari zimechukuliwa na Serikali ikiwa ni pamoja na kuwaagiza waajiri kuhakikisha kama imemwajiri mnufaika wa mikopo ya elimu ya juu ihakikishe inamkata kiasi fulani cha fedha kwa ajili ya kulipa mkopo aliochukua.

Mambo mengi yametokea na kuripotiwa kuhusiana na bodi hiyo ukiwamo ufisadi uliokuwa unafanyika kupitia mwanafunzi hewa ambao walikuwa wakikopeshwa.

Ukweli ni kuwa bodi kwa kiasi kikubwa imeonekana kushindwa kutekeleza majukumu yake kama ambavyo ingetarajiwa na ni muda muafaka kwa serikali kufikiria njia mbadala ambayo itakuwa na tija katika utoaji wa mikopo kwa ajili ya elimu ya juu.

Ingekuwa ni jambo la busara endapo serikali ingehamishia jukumu la kukopesha fedha kwa mabenki ambayo kimsingi ukopeshaji ndiyo kazi yake.

Serikali inaweza kuweka dhamana kwa mabenki kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu na kuyaachia majukumu ya kutoa mikopo pamoja na kufuatilia.

Bodi inaweza kufanya kazi za uratibu kuhakikisha kuwa wanaopata mikopo ni wale wanaostahili kwa mujibu wa vigezo vilivyoweka.

Uzoefu unaonyesha kuwa, fedha za mikopo zinazotolewa na benki ni lazima zilipwe na mabenki yamekuwa na utaratibu mzuri wa kufuatilia mikopo na kuhakikisha kuwa inalipwa.

Kama zitapewa jukumu la kutoa mikopo ya elimu ya juu kwa dhamana ya serikali ni wazi kuwa nidhamu katika urejeshaji wa fedha utakuwepo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles