Na MWANDISHI MAALUM-DODOMA
SERIKALI kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imesema haina upungufu wa chanjo wa aina yoyote, hivyo kuwataka wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao kuwapatia chanjo katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya, Dk. Leonard Subi jijini hapa jana, alipotembelea ghala ya kuhifadhia chanjo iliyopo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kukagua hali ya chanjo katika mkoa huo.
Dk. Subi alisema chanjo zote aina tisa ambazo zinakinga dhidi ya magonjwa 13 zipo kwenye ghala hilo.
“Tulikuwa na upungufu wa aina mbili kati ya tisa za chanjo nchini, ambazo tumekuwa tukizitoa, lakini sasa hivi chanjo zote zipo, kwani zimeshawasili hapa nchini na usambazaji unaendelea,” alisema Dk. Subi.
Hata hivyo Dk. Subi alisema kuwa upungufu huo wa chanjo ulitokea baada ya dunia kukumbwa na janga la mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19 ambapo anga zote zilifungwa kwani chanjo husafirishwa kwa mnyororo baridi, kwa hiyo huitaji usafiri wa anga.
“Tunamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli kwa kulifungua anga la Tanzania ambapo chanjo sasa zimeanza kuingia nchini, na hadi sasa mikoa 13 chanjo hizi zimeshapokelewa kati ya mikoa 26, na mikoa mingine 13 ya Tanzania Bara usambazaji unaendelea kupitia Bohari ya Dawa (MSD),” alisema Dk. Subi.
Aidha, Dk. Subi alisema kuwa usambazaji wa chanjo hizo mbili ambazo wananchi walikuwa wanazikosa ulishaanza na watazipata kwa uhakika, huku akielekeza MSD kuhakikisha chanjo zote zimefika katika mikoa iliyosalia ya Tanzania Bara ifikapo mwishoni mwa wiki hii.
“Waganga wakuu wa mikoa na halmashauri wote nchini hakikisheni chanjo hizo mnazipeleka kwenye vituo vyetu vya kutolea huduma za afya na muwajulishe wananchi kwamba chanjo zipo na zinapatikana bila malipo yoyote, wazazi na walezi pelekeni watoto wenu kupata chanjo katika mikoa yenu,” alisisitiza Dk. Subi.
Kwa upande wa taarifa iliyotolewa na moja ya chombo cha habari hapa nchini kuhusu kukosekana kwa chanjo ya kuzuia kuhara (Rota) Dk. Subi alifafanua kuwa Tanzania haijawahi kukosa chanjo hiyo.
Aliweka bayana kuwa chanjo zilizopungua kwa mwezi mmoja na nusu ni chanjo ya Polio na Surua-Rubella hali iliyosababishwa na mlipuko wa Covid-19 duniani, huku akisisitiza kuwa Serikali imekuwa ikinunua chanjo hizo kutoka nchi za Ulaya na Asia.
Aliendelea kusema kuwa Serikali inaendelea kutoa fedha za chanjo na kwamba hadi sasa imetoa zaidi ya Sh bilioni 18 kwa ununuzi wa chanjo na kuifanya Tanzania kuendelea kuwa katika kiwango cha juu cha utoaji wa chanjo kwa zaidi ya asilimia 98 kwa miaka sita mfululizo.
Hata hivyo, Dk. Subi alisema kuwa Tanzania haijawahi kupata mgonjwa wa kupooza tangu mwaka 1996, jambo linalotokana na uwepo wa hali nzuri ya upatikanaji wa chanjo, huku akidai kuwa Tanzania tayari imepata cheti cha utambuzi kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 2015.