28.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

SERENGETI BOYS YAJIKWAA

  • Yaupiga mpira mwingi Taifa yaishia kupigwa na Nigeria

MOHAMED MHARIZO-DAR ES SALAAM

TIMU ya soka ya Taifa ya Tanzania kwa vijana walio na umri chini ya miaka 17, Serengeti Boys, imeanza vibaya fainali za  Afrika kwa umri huo baada ya jana kuchapwa mabao 5-4 na Nigeria katika mchezo wa ufunguzi uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo wa kundi A, Serengeti Boys iliuanza kwa kusuasua, huku ikiruhusu mashambulizi ya mara kwa mara ambayo yaliweza kuokolewa mara kwa mara na kipa wa timu hiyo, Mwinyi Yahya. Mashambulizi hayo ya Nigeria yaliigharimu Serengeti Boys, ambayo ilijikuta ikifungwa bao dakika ya 20 na Olatomi Olaniyan.

Hata hivyo, dakika moja baadaye, Serengeti Boys ilisawazisha kupitia kwa Edmund John, aliyepiga shuti kali lililokwenda moja kwa moja wavuni, baada ya kupewa pasi na Kelvin John.

 Dakika 30, Nigeria iliandika bao la pili kupitia kwa Wisdom Ubani.

 Bao hilo liliiongezea nguvu Nigeria, ambayo ilizidi kuishambulia Serengeti Boys, hatua iliyomlazimu kocha wa kikosi hicho, Oscar Mirambo, kufanya mabadiliko dakika ya 34, ambapo alimtoa Misungwi Chananja na kumwingiza Edson Mshirakandi.

 Pamoja na mabadiliko hayo, Serengeti Boys ilijikuta ikifungwa bao la tatu dakika ya 37 kupitia kwa Akinkunmi Amoo.

Amoo aliifungia bao hilo Nigeria baada ya kuwazidi kasi mabeki wa Serengeti, kisha kumlamba chenga kipa na kuuzamisha mpira wavuni.

Hadi mapumziko Nigeria ilikuwa mbele kwa mabao 3-1.

Kipindi cha pili kilipoanza, Serengeti Boys iliionekana kuwa na nguvu mpya na kufanikiwa kupata bao la pili dakika ya 51 lililofungwa na John.

Dakika ya 55, nahodha wa Serengeti, Morice Abraham, aliisawazishia timu yake hiyo kwa kuifungia bao la tatu, baada ya Pascal Msindo kuangushwa ndani ya eneo la hatari na mwamuzi Issa Sy kutoka Senegal kuamuru ipigwe penalti.

Bao hilo liliiongezea nguvu Serengeti, kwani dakika ya 59 Edmund John aliiandikia bao la nne, baada ya mmoja wa mabeki wa Nigeria kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari.

Lakini almanusura Serengeti ipoteze mkwaju huo, baada ya mpira kugonga mwamba kisha kumgonga kwa nyuma kipa wa Nigeria, Suleman Shaibu na kujaa wavuni.

Dakika ya 69, Abraham alionyeshwa kadi ya njano, baada ya kucheza mpira usio wa kistaarabu.

 Dakika ya 71, Nigeria ilifanya mabadiliko, alitoka Olatomi Olaniyan na kuingia Ibraheem Jabaar.

Mabadiliko hayo yaliineemesha Nigeria, ambayo ilifanikiwa kusawazisha dakika ya 72 kupitia kwa Wisdom Ubani, ambaye mkwaju wake wa mpira wa adhabu ulikwenda moja kwa moja wavuni.

Baada ya kusawazisha, Nigeria ilirejea mchezoni na kuanza kuliandama lango la wenyeji wao, Serengeti.

Dakika ya 78, Nigeria iliandika bao la tano lililofungwa na Agiri Ngoda kwa shuti la mbali.

Katika kuhakikisha inachomoa na pengine kufunga la ushindi, Serengeti ilifanya mabadiliko dakika ya 80, alitoka Morice Abraham na kuingia Ladaki Chasambi.

Pamoja na mabadiliko hayo, dakika 90 za pambano hilo zilimalizika kwa Serengeti kulala kwa mabao 5-4 dhidi ya Nigeria.

Serengeti Boys: Mwinyi Yahya, Arafat Swakali, Mustapha Nankuku, Alphonce Msanga, Misungwi Chananja, Edmund John, Kelvin John, Pascal Msindo, Dominic William, Ally Rutibinga, Morice Abraham.

Nigeria: Suleman Shaibu, Shedrack Tanko, Ogaga Oduko, Samson Tijani, Clement Ikenna, David Ishaya, Olakunle Olusegun, Mayowa Abayomi, Wisdom Ubani, Akinkunmi Amoo, Olatomi Olaniyan.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles