25 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Sera ya Kilimo ya Nyerere iwe inarejewa

wakilima-3

NA ALOYCE NDELEIO, DAR ES SALAAM

IPO misemo kadhaa ambayo imekuwa maarufu katika ulingo wa siasa ikiwa inatumika kuonesha umuhimu wa kilimo na baadhi ikiwa ni mikongwe kama vile ‘kilimo ni uti wa mgongo wa taifa’ na mwingine ni siasa ni kilimo ambao ulitokana na Azimio la Iringa.

Katika miaka ya hivi karibuni baada ya baadhi ya maazimio yaliyoasisiwa na Hayati Baba wa Taifa kuachwa yatima au kubadilishwa maana yake, ikaibuka kauli nyingine kama vile kuhuisha Azimio la Iringa ikiwa ni ‘Kilimo Kwanza’.

Pamoja na hali yote hiyo kauli mbili za kwanza ndizo kongwe na zimekuwepo ndani ya jamii kwa kipindi kirefu tangu enzi za itikadi za chama kimoja, itikadi moja kwa kuzingatia kwamba kwa wakati huo kilimo kilipewa kipaumbele katika utekelezaji wa mikakati yote ile ya kisiasa.

Aidha, katika kutekeleza azma hiyo ya kuonesha kuwa kilimo ni uti wa mgongo wa taifa, miradi kadhaa ya kilimo iliyoendeshwa kitaalamu ilianzishwa na hususani katika kuzalisha mazao ya chakula kwa nia ya kulifanya taifa lijitosheleze kwa chakula.

Hata hivyo, ukweli ukabakia kuwa miradi hiyo mikubwa iliendeshwa na mashirika mbalimbali ya kutoka nje na miongoni mwa mazao yaliyopewa kipaumbele ni pamoja na kilimo cha mpunga kwa kuwepo kwa skimu za umwagiliaji.

Taswira iliyojitokeza ilionyesha kuwa yapo  mabonde ambayo yakiendeshwa kwa kitaalamu yanaweza kuifanya nchi ijitosheleze kwa chakula hususani katika kuzalisha mpunga.

Kilichojionesha kwa mashirika hayo ya nje  kuendesha miradi hiyo ni kwamba kilimo kinahitaji fedha nyingi na kwamba mtu hawezi kuendesha kilimo cha kisasa bila fedha nyingi za kutosha kwa maana kuwa na mtaji mkubwa.

Hata hivyo, kila uchao mkulima wa Tanzania anaelezwa kuwa ni masikini kwa kuwa kilimo anachokiendesha ni cha kukidhi mahitaji yake ya chakula na kama inakuwepo ziada inakuwa ni kidogo ambayo huiuza.

Kama ni kuangalia nchi zilizokitumia kilimo kupata maendeleo au kuleta mapinduzi kama China ni kwamba walipoamua kuendelea kama nchi enzi za Mao, walihakikisha kwamba watu wanashiba kwanza na wakaleta mapinduzi ya kilimo kwa kulima kwa kutumia mashine.

Hali kadhalika mapinduzi ya viwanda katika nchi za Ulaya yalifanikiwa baada ya kutokea mapinduzi ya kilimo.

Limekuwepo tatizo kwamba sera za kilimo  na ufugaji zimekuwa zikiendeshwa kisiasa sana na utaalamu ukiwekwa kwa mbali.

Mfano sera za kilimo na ufugaji zimekuwa  zinaendeshwa kisiasa na hata kufikia hali ya kuwafanya maofisa ugani na maofisa mifugo pamoja na maofisa uvuvi wamekuwa katika mgawanyiko na hususani walipokuwa chini ya wizara tofauti.

Lakini ukweli unabakia kwamba Mwalimu Nyerere alitunga na kutumia dhana ya siasa ni kilimo kwa kuzingatia Tanzania ni nchi iliyokuwa inategemea kilimo, hivyo uti wa mgongo wa uchumi wake ulikuwa ni kilimo na sehemu kubwa ya wananchi wakiwa wakulima.

Kwa wakati wote Mwalimu Nyerere alifundisha kuwa siasa itambue na kuzingatia uhalisia huo kwamba ni lazima siasa zitambue masilahi ya wale wanaoushikilia uti huo wa mgongo, maisha yao yaboreshwe na mbinu za kilimo  ziboreshwe pia.

Hatua hiyo ilikuwa na maana kuboresha kilimo kwa kutumia mkondo wa kisiasa  kungeleta mafanikio na hata kuzuia  mtiririko wa watu kuhamia mijini na ama iwe kinyume chake kwamba sehemu kubwa ya nguvu kazi ingetumika katika uzalishaji wa kilimo zikiwemo malighafi.

Kwa maana hiyo imani yake ilikuwa hata huduma zilizokuwa zinapatikana mijini  zipatikane pia vijijini. Lakini ni dhahiri kuwa wakati Mwalimu alitumia juhudi nyingi kutafakari mambo na kuyaeleza kwa wananchi, baadhi ya viongozi walifanya mambo kwa uzembe.

Katika hilo ndio maana aliwahi kusema  walikuwepo baadhi ya viongozi ndani ya CCM ambao kama wangepewa mtihani kuhusu Azimio la Arusha hakuna ambaye angefaulu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles