28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Sera ya jinsia kumaliza ubaguzi katika vyombo vya habari

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Sera zinazosimamia usawa wa jinsia katika vyombo vya habari zitamaliza ubaguzi na kutoa fursa sawa kwa wanawake na wanaume imeelezwa.

Utafiti uliofanywa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) kuhusu wanawake katika vyumba vya habari
unaonyesha walio katika nafasi za uongozi ni asilimia 21 wakati wanaume ni asilimia 79.

Akizungumza wakati wa mkutano kuhusu uongozi na ukatili wa kijinsia katika vyumba vya habari ulioandaliwa na Shirika la Habari la Internews na kufanyika kwa njia ya mtandao, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amesema lazima zifanyike juhudi za kumaliza ubaguzi wa kijinsia katika vyumba vya habari.

“Hatuwezi kuendelea kulalamika tuchukue hatua ambazo zitaleta usawa wa kijinsia katika vyombo vya habari, tutetee asilimia 30 iingizwe kwenye sheria tutakuwa na sheria nzuri itakayowaingiza kina mama katika nafasi za maamuzi,” amesema Balile ambaye aliwasilisha mada kuhusu uongozi katika vyombo vya habari na nafasi ya mwanamke katika uongozi ndani ya vyombo vya habari.

Waandishi wa habari wakiwa kazini

TEF tayari limewasilisha Serikalini mapendekezo ya mabadiliko ya sheria za habari ikiwemo ya kutaka asilimia 30 wawe wanawake katika vyombo vya habari.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), Dk. Rose Reuben, amewataka waandishi wanawake kutambua kuwa wao si wa kuongozwa kila siku bali nao wanaweza kuongoza na kutoa maamuzi katika vyombo vyao vya habari.

“Waandishi wanawake ni muhimu sana katika vyombo vya habari ili kufikia usawa wa jinsia, kama hawapo hatutarajii tutakuwa na taarifa za usawa wa jinsia na kubadili mitazamo ya wananchi na kumaliza ukatili wa kijinsia,” amesema Dk. Rose.

Aidha ameshauri ufanyike utafiti kujua kwanini wanawake wengi wakimaliza vyuo vya uandishi wa habari hawavutiwi kufanya kazi katika vyombo vya habari na hata wanaoingia kwenye vyombo hivyo baadhi yao hawavutiwi kuendelea kubaki.

Wakichangia katika mkutano huo baadhi ya washiriki wamesema wanawake wengi hawajiamini hali inayowafanya waendelee kubaki nyuma.

Mmoja wa washiriki hao Anna Mwasyoke kutoka Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), ameshauri wanawake katika vyombo vya habari hasa vya kielektroniki wawe wabunifu na kufanya kazi zao wenyewe badala ya kuishia kutangaza zilizoandaliwa na wengine.

Mshiriki mwingine Moza Ali kutoka Hits FM ya Zanzibar, amesema baadhi ya wanawake hawana utayari kwani hata wanapokwenda kwenye mafunzo kwa vitendo hujichagulia kazi za kufanya kama vile kutangaza.

Naye Jane Mihanji kutoka magazeti ya Uhuru na Mzalendo, ameshauri kukomeshwa kwa tabia ya kuwanyanyapaa wanawake na kuwataka wahariri kuwapa majukumu mazito kama wanavyofanya kwa wanaume.

Edwin Soko ameshauri wanaume wawe mabalozi kuhakikisha kuna usawa wa jinsia katika vyombo vya habari.

Theophil Makunga kutoka Tumaini Media, ameshauri kuwe na mafunzo ya kuwajengea ujasiri wanawake sambamba na kupanua wigo wa muundo wa nafasi katika vyombo vya habari.

“Kuna mtu mwingine anataka kuwa mwandishi aliyebobea na kuna wengine hawataki kuwa wahariri hivyo, lazima kutengenezwe ‘structure ya interest’ ya mtu,” amesema Makunga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles