24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Amref yasaidia asilimia 99 ya wenye VVU Simiyu kutumia dawa

Na Derick Milton, Simiyu,

SHIRIKA la Amref Health Africa, limetajwa kuwa moja ya wadau wa afya katika Mkoa wa Simiyu ambao wamefanikisha kufikia asilimia 99 ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI kutumia dawa za kufubaza (ARVs).

Hayo yamebainishwa na Kaimu Mratibu wa UKIMWI mkoani huo Oscar Tenganamba wakati wa maazimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani kimkoa ambayo yamefanyika mjini Bariadi.

Tenganamba amesema kuwa kupitia mradi ambao Amref wanatekeleza mkoani humu, wamekuwa wakitekeleza shughuli mbalimbali ambazo zimewezesha mapambano dhidi ya VVU kuendelea kuwa makubwa.

Amesema kuwa pamoja na hilo, eneo la watu wote kupima afya zao, Mkoa wa Simiyu umefikia asilimia 89 kati ya 95 ambazo wanatakiwa kufikia ifikapo mwaka 2030, ambapo Amref wameanzisha huduma za upimaji katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma.

Aidha amesema kuwa asilimia 96 ya wale ambao wanatumia dawa za ARVs, virusi vimeanza kufubaa kwenye miili yao.

Amesema kuwa kupitia mradi huo, Amref wamekuwa wakiwafuatilia wale wote wanaotumia dawa na kuwapatia elimu ya kutumia dawa hizo mara kwa mara.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, David Kafulila, akiangalia takwimu za mradi.

“Amref pia wamekuwa wakitekeleza huduma za tohara kinga kwa wanaume, lakini pia kupambana katika kuzuia maambukizi toka kwa mama kwenda kwa mtoto, ambapo kwa mkoa kiwango cha maambukizi hayo ni asilimia moja, ni moja ya eneo ambalo Amref wamesaidia na tukafikia hapa,” amesema Mratibu huyo.

Mratibu wa mradi huo mkoani Simiyu, Paschal Nyagonde amesema kuwa kupitia mradi huo zaidi ya vituo 90 vya kutolea huduma za afya vinatoa huduma za upimaji wa VVU.

Aidha Nyagonde amesema kuwa pamoja na upimaji, kupitia vituo hivyo Amref inatoa huduma za tiba na matunzo kwa watu wenye VVU ili kuendelea kutumia dawa zaidi na kuwakinga wengine.

“ Amref kupitia mradi wetu huu, tumeendelea kutoa elimu kwa vijana mbalimbali juu ya kujikinga na ugonjwa huu, vijana wote wa rika balehe wamekuwa wakipewa elimu ya jinsia,” amesema Nyagonde.

Akifunga maonyesho hayo Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, David Kafulila, amewapongeza wadau wote ambao wamekuwa wakishirikiana na serikali katika kupambana na maambukizi ya virusi vya UKIMWI, huku akitaka suala la ugonjwa huo kuwa ajenda katika vikao mbalimbali vya maendeleo.

Kafulila amewataka wazazi pamoja na viongozi wa dini kuendelea kulea watoto katika tabia njema, kwani asilimia kubwa ya watu ambao wameambukizwa na ni vijana ambao ndiyo nguvu ya taifa.

“ Suala la mapambano dhidi ya Ukimwi liwe ajenda kuu katika vikao vyote vya maendeleo kuanzia ngazi ya kata hadi mkoa, mapambano lazima yazidi kuwa makubwa kuhakikisha ugonjwa huu unaisha kabisa au maambukizi kupungua,” amesema Kafulila.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles