LIBREVILLE, Gabon
MOJA kati ya timu zinazopewa nafasi kubwa ya kubeba taji la michuano ya Afrika (Afcon) ni Senegal (Simba wa milima ya Teranga) ambao wamekuwa wakionyesha uwezo wa hali ya juu katika mashindano hayo yanayofanyika mwaka huu huko nchini Gabon.
Senegal wanaoongoza katika viwango vya ubora barani Afrika huku katika viwango vya dunia ikikamata nafasi ya 33 na kuwapiku Ivory Coast mabingwa watetezi wa kombe hilo la Mataifa ya Afrika, walikuwa wakiongoza katika viwango vya ubora kabla ya kushushwa na wababe hao.
Miamba hiyo ya Afrika Kaskazini inaongozwa na mshambuliaji anayefanya vizuri katika klabu ya Liverpool inayoshiriki Ligi Kuu ya England, Sadio Mane, ambaye amekuwa mwiba katika fainali hizo hadi sasa amekwishapachika mabao mawili katika michezo aliyoshuka uwanjani.
Mane ambaye amefuata nyayo za mkongwe, El hadji Diouf, kukipiga katika klabu ya Liverpool yenye maskani yake huko Merseyside amekuwa moto wa kuotea mbali na kuwa tegemeo la Wasenegal ambao wameonyesha kumwamini kutokana na uwezo wake.
Nyota wengine ambao wapo katika kikosi hicho ni pamoja na mlinzi wa kati wa Napoli ambaye aligoma kucheza timu ya taifa ya Ufaransa, Kalidou Koulibaly, kiungo wa kati wa Everton, Idrissa Gueye, pamoja na kiungo mpya wa wagonga nyundo wa jiji la London, West Ham, Cheikhou Kouyate pamoja na winga Balde ambaye yupo kwenye fomu ya hali ya juu.
Wakali hao ambao wapo kundi moja na Algeria, Tunisia pamoja na Zimbabwe ni moja ya makundi yenye ushindani mkubwa huku wao wakiwa wameshinda michezo yao katika kundi lao wamekuwa wakitolewa macho na wadau wengi barani Afrika na duniani kwa ujumla kutokana na kukusanya wachezaji nyota wanaocheza ligi mbalimbali barani Ulaya na America.
Simba hao wa Teranga walijihakikishia mapema safari yao ya robo fainali wakiwa na mchezo mmoja mkononi mara baada ya kushinda michezo yao miwili na kuwa kikosi cha kwanza kuingia katika hatua hiyo mapema zaidi kuliko timu zote.
Senegal ambao wapo chini ya kocha Aliou Cisse, mchezaji wa zamani wa Montpellier HSC na timu ya Taifa ya Senegal ambaye aliiwakilisha timu hiyo katika mashindano ya Kombe la Dunia nchini Korea Kusini na Japan ambapo Brazil walinyakua taji hilo mara baada ya kuwafunga Ujerumani katika mchezo wa fainali.
Mkongwe huyo ameweza kuyarudisha makali ya kikosi cha Simba hao ambao walikuwa na kasi kubwa mwaka huu kutokana na kuwarudisha katika hali ya kujiamini katika kikosi chake ambacho mara kwa mara kimekuwa kikisindikiza katika fainali mbalimbali, lakini mwaka huu wamepania kufanya vizuri zaidi na kusimika ufalme wao.
Senegal ambao wamejijengea heshima kubwa duniani, watakumbukwa kwa uwezo wao mkubwa waliouonyesha mwaka 2002 katika fainali ya Kombe la Dunia zilizofanyika nchini Korea Kusini na Japan ambapo kikosi hicho kilikuwa na wakali kama vile El hadji Diouf, Pape Bouba Diop, Makthar N’Diaye, Moussa N’Diaye pamoja na Sylvain N’Diaye, waliokuwa moto wa kuotea mbali.
Vijana hao wa Cisse wamekuwa katika kiwango cha hali ya juu zaidi kiasi cha baadhi ya wachambuzi na wachezaji wa timu nyingine kuwamwagia sifa huku wakiwapigia chapuo kuwa iwapo wataendelea kuwa katika kiwango hicho huenda wakatwaa taji hilo.
Mchezaji bora wa Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi ya ndani ya bara hili, Dennis Onyango, amesema Senegal anawapa nafasi kubwa ya kubeba taji hilo mwaka huu kutokana na ubora wa kikosi chao kilichosheheni wachezaji wenye uwezo mkubwa.
Onyango mlinda mlango wa timu ya Taifa ya Uganda, aliyasema hayo mara baada ya kuulizwa anaipa nafasi timu gani ya Taifa kuwa itabeba taji la fainali za mwaka huu, alishindwa kuzuia hisia zake na kuwataja wakali hao wa Afrika Kaskazini.
Wakali hao ambao wameshiriki fainali za mataifa ya Afrika mara 13 na kuwa moja ya nchi ambazo zinafanya vizuri katika michuano hiyo, wameshiriki katika miaka ya 1965, 1968, 1986, 1990, 1992, 1994, 2000, 2002, 2004, 2006, 2008, 2012 pamoja na 2015.
Mwaka huu Simba hao wa Teranga wamecharuka mara baada ya kujifunza kupitia makosa yaliyojitokeza miaka miwili iliyopita walipoishia katika hatua ya makundi jambo ambalo lilitengeneza picha mbaya kwa wapenzi wa soka nchini Senegal.
Hata hivyo, timu yoyote inaweza kutwaa ubingwa wa michuano hiyo kama itaweza kutumia nafasi kwa kuwa soka ni mchezo wa makosa, hivyo chochote kinaweza kutokea.
Kwa upande wa mabingwa watetezi, Ivory Coast, wana kikosi ambacho kimejaa wachezaji ambao wanacheza soka la kulipwa barani Ulaya, lakini msimu huu wanaonekana kuwa na kasi ndogo, ila kwa hatua inayofuata wanaweza kuonesha makubwa zaidi.