24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

MAYWEATHER HII SASA DHARAU

ADAM MKWEPU NA MITANDAO


Floyd-MayweatherINAWEZEKANA kikawa kitendo cha kawaida kwa watu wenye fedha lakini cha dharau kwa ambao hawana fedha.

Hii ni kauli inayokuja baada ya bondia  wa uzito wa kati, Floyd Mayweather, kumkejeli mpinzani wake, Conor McGregor, kuwa ni fukara na hana hadhi ya kupambana naye.

Mayweather amemwambia McGregor  mwenye utajiri wa dola milioni mbili kuwa, ili wazichape anatakiwa awe na utajiri wa zaidi ya dola milioni 25.

Bondia huyo mwenye utajiri wa dola milioni 650, ametamka maneno hayo mbele ya Rais wa Ngumi za Kulipwa nchini Marekani (UFC), Dana White, ambaye ametoa dau la dola milioni 50 ili kufanikisha pambano hilo.

“Nitamlipa fedha nyingi Mayweather ambazo nafahamu zitamshawishi kwa kuwa fedha ninazolipa katika mapambano yangu huwa ni nzuri.

“Kila mmoja nitamlipa kiasi cha dola milioni 25, pia tutafanya mazungumzo kuhusu fedha zitakazopatikana kupitia mauzo ya tiketi,” anasema White.

Hata hivyo, kauli hiyo ilipingwa vikali na Mayweather kwa kumfananisha White na mchekeshaji.

“White ni kituko, hivi kabla ya kutaja hizo fedha anaweza kuthaminisha gharama ya saa yangu ya mkononi na kuniambia nimenunua kiasi gani,” anahoji Mayweather.

Mayweather anasema atakuwa tayari kupanda ulingoni endapo mtayarishaji wa pambano hilo atamlipa kitita cha dola milioni 100.

Bondia huyo hakusita kutoa masharti, ambapo anataka kitita hicho mpinzani wake alipwe kiasi cha dola milioni 15 ikijumuishwa na mapato ya kiingilio cha mlangoni.

Mkurugenzi huyo wa Kampuni ya TMT  anasema kwamba, kiasi cha dola milioni 25 ni kidogo sana na ameona iwapo atapokea fedha hizo ni kama atadharauliwa.

Bondia huyo pia alimweleza mpinzani wake kuwa anastahili kupokea kiasi cha dola milioni mbili na si dola milioni 25 kwa kuwa ni fukara ndio maana ameshindwa kuwa na utajiri wa dola milioni 25.

Mayweather aliendeleza kejeli hizo hadi katika mitandao ya kijamii ambapo aliweka kiasi cha fedha akimaanisha utajiri alionao pamoja na kuweka utajiri wa mpinzani wake ambapo ilionekana kuwa na tofauti kubwa.

Kiwango cha kawaida cha fedha anachotakiwa kulipwa Mayweather ni dola milioni 32 kama ilivyokuwa katika pambano lake lililopita dhidi ya Andre Berto mwaka 2015.

Hata hivyo, kiasi hicho kilikuwa kidogo ikilinganishwa na alichopata katika mgawo wa dola milioni 100 baada ya  pambano lake na Manny Pacquiao.

Katika pambano hilo, McGregor, anatakiwa kulipwa kiasi cha dola milioni 3 kutokana na nafasi yake.

Katika mapambano yake ya awali, McGregor alilipwa dola milioni 1 katika pambano lake dhidi ya Nate Diaz na marudiano alilipwa dola milioni 3.

Fedha hizo pia alilipwa wakati alipopigana na Eddie Alvarez ingawa alidundwa.

“Kutokana na malipo yake ya mapambano ya awali ni dhahiri kwamba kiasi chake cha malipo hakifanani na kile ambacho kimetajwa,” anasema Mayweather.

Mwaka uliopita, McGregor alitajwa kuwa wa kwanza katika historia ya UFC baada ya jina lake kuingizwa katika orodha ya jarida la Forbes ya mabondia wanaolipwa mkwanja mrefu ulingoni baada ya kuingiza kitita cha dola milioni 22.

Fedha hizo zilijumlishwa kabla ya pambano lake la marudio dhidi ya Diaz lililofanyika Agosti mwaka jana na Alvarez ambaye walizichapa Novemba mwaka jana.

Aidha, mwendelezo wa kejeli zinazofanywa na Mayweather zinaonesha dhahiri kwamba, McGregor bado yupo nyuma kimapato dhidi ya Mmarekani huyo.

Hata hivyo, baada ya kejeli za Mayweather, mwandaaji wa pambano hilo, White anasema kwamba mbali na kitita anachotaka kuwalipa mabondia hao, Mayweather, amehakikishiwa kulipwa dola milioni 30 zaidi ya mpinzani wake.

Kwa vyovyote vile fedha hizo huenda zikamshawishi Mayweather kuvaa glovu zake tena na kupanda ulingoni baada ya kupita mwaka mmoja na nusu tangu atangaze kujiuzulu.

“Kitendo cha Maywether kusema ndio mwenye jina kubwa zaidi ya McGregor si kweli, licha ya kupewa nafasi kubwa ya kushinda lakini Conor anaweza kuonesha maajabu katika pambano hilo,” anasema White.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles