26.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

SELF yasogelea wajasiriamali Kanda ya Kaskazini

jengo-la-nssfNa WINFRIDA NGONYANI-DAR ES SALAAM

MFUKO wa Kutoa Mikopo kwa Wajasiriamali Wadogo (SELF), unatarajia kufungua ofisi mpya Kanda ya Kaskazini mapema Novemba mwaka huu.

Hatua hiyo itaufanya mfuko huo kutoa huduma katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Tanga, Singida na Dodoma.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jijini Dar es Salaam na mfuko huo, ilieleza kuwa, hatua hiyo itawasaidia wajasiriamali wa kanda hiyo kunufaika na huduma za haraka za mfuko huo.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa, huduma zitakazotolewa na mfuko kwenye ofisi hiyo iliyopo kwenye jengo la NSSF lililoko Barabara ya Old Moshi mjini Arusha, itapunguza gharama za uendeshaji kwa wadau watakaoweza kuhudumiwa kwa haraka zaidi tofauti na awali, ambapo ni mikoa hiyo iliyokuwa inahudumiwa na Ofisi ya Kanda ya Mashariki.

“Tunatarajia asasi zitaongeza ufanisi kwenye utendaji wake pamoja na kuweza kutimiza malengo ya kuongeza ubora na upatikanaji wa huduma za kifedha kwa walengwa wa mfuko,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Awali mfuko huo ambao unatoa huduma Tanzania Bara na Visiwani, ulikuwa una kanda tatu ambapo kuongezeka kwa kanda hiyo kumefanya idadi ya kanda kuwa nne.

Mfuko wa Self ambao ulisajiliwa kwa Sheria ya Makampuni ya mwaka 2002 chini ya udhamini wa Serikali, ulianzishwa kukidhi nia ya Serikali ya kupata suluhisho la kudumu kwa tatizo la wananchi hasa wa vijijini kutofikiwa na huduma za kifedha.

SELF inatoa mikopo ya masharti nafuu kwa wajasiriamali wadogo kupitia asasi ndogo na za kati za kifedha kama vile Vyama vya Ushirika wa Mikopo (Saccos), Benki za Jamii, Mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) na Kampuni za fedha zinazotoa huduma za mikopo.

Aidha, mfuko huo unawapa fursa watu wa kipato cha chini kujiletea maendeleo kwa kupambana na umasikini na hivyo kujenga misingi bora, imara na endelevu ya kujiongezea kipato na hivyo kuboresha maisha.

Hadi kufikia Juni mwaka huu, Mfuko ulikuwa umetoa mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 76.2 kwa mtandao wa asasi 456 unaoshirikiana nazo kufikisha huduma hii ya mikopo.

Zaidi ya  asimilia 80 ya asasi hizo ni Vyama vya Akiba na Mikopo (Saccos). Aidha, asilimia 60 ya asasi hizi ni za vijijini, ambapo asilimia 28 ni za mijini na 12 ziko katika miji midogo.

Mikopo hii imesaidia kukuza sekta ya Kilimo na Ujasiriamali kwa kunufaisha zaidi ya wateja wapatao 107,962 ambao kati yao asilimia 56 ni wanawake.

Inaelezwa kuwa mikopo imetengeneza takriban ajira zipatazo 236,365, ikiwa ni pamoja na wajasiriamali waliojiajiri wenyewe na walioajiriwa katika miradi na biashara hizo.

Inakadiriwa kuwa takriban watu wapatao 492,500 kwa njia moja au nyingine, wamenufaika na mikopo hiyo.

Katika kuboresha huduma za asasi, Mfuko huwa unajenga uwezo wa kiutendaji kwa wabia wa mfuko, kwa kuwatengenezea mazingira mazuri na ya kisasa yanayohamasisha ufanisi kwa wafanyakazi, ili watoe huduma bora kwa wateja na wanachama wao.

Mfuko pia unatoa  mafunzo ya biashara na ujasiriamali kwa wateja na wanachama wa asasi, ili waweze kuwekeza mikopo yao vizuri, wapate faida, waondokane na umasikini na pia waweze kurejesha mikopo hiyo vizuri na hivyo kuzungusha rasilimali fedha.

Hadi kufikia Juni  mwaka huu, mfuko ulikuwa umetoa mafunzo kwa wajasiriamali wadogo wapatao 11,948, pamoja na watendaji wa asasi za fedha 4,664 kutoka katika asasi zipatazo 690.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles