VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAA
MKURUGENZI Mstaafu wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), Valerie Msoka, amesimulia jinsi alivyothubutu kupambana kuleta usawa wa jinsia katika sekta ya habari nchini.
Msoka aliyasema hayo mwishoni mwa wiki katika tukio la kwanza la Mtandao wa Wanawake wa Habari na Mawasiliano Tanzania uliohusu mada ya kujitambua.
Alisema yeye ndiye mwandishi wa kwanza mwanamke kuripoti habari za Ikulu.
Akizungumzia nafasi ya uongozi, Msoka ambaye sasa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui katika Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), alisema si jambo rahisi.
“Wanawake tuna majukumu mengi inahitaji nidhamu ya muda kufanya yote, unapokuwa kiongozi inabidi utambue unafanya kazi kwa manufaa ya wengi, hivyo lazima kufanya uamuzi sahihi wenye tija.
“Mimi ndiye mwanamke wa kwanza Tanzania kuripoti habari za Ikulu, enzi zile kulikuwa na ‘gap’ kubwa waandishi wanaume tu ndiyo waliitwa Ikulu.
“Siku moja nilihudhuria mkutano wa waandishi wa habari na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere wakati huo, alishangaa akaniuliza umefikaje hapa.
“Binafsi nilipenda uandishi wa habari tangu nilipokuwa mdogo, lakini kwa sababu kipindi tunasoma wale ambao tulikuwa tuna uwezo mkubwa darasani ilikuwa lazima tusome sayansi hata kama hupendi, hivyo nikasoma kemia, fizikia na baiolojia (PCB),” alisema.
Mkurugenzi wa Tanzania Women CEO’S Roundtable, Emma Kawawa, alisema pamoja na yote hayo ni muhimu pia kuchagua angalau watu watatu watakaoweza kukushauri vizuri.
Mwenyekiti wa muda wa mtandao huo, Bokhe Mwita alisema unakusudia kuamsha ari ya utendaji kazi na kujitambua kwa kundi hilo nchini.