27 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Sekoutoure yadhibiti vifo vya akina mama wanaojifunguaio

Na Clara Matimo, Mwanza

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza (Sekoutoure) imefanikiwa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kutoka 18 mwaka 2017 hadi nane mwaka 2021.

Hayo yamebainishwa hivi karibuni na Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Bahati Msaki, wakati akitoa taarifa fupi ya  mradi wa jengo  la mama na mtoto  ambalo limegharimu fedha za ndani za serikali takribani Sh bilioni 9.8 kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel, aliyekuwa katika ziara ya kukagua huduma zinazotolewa katika jengo hilo.

KARIBU: Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel(kushoto) akijadiliana jambo na Mganga Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Thomas Rutachunzibwa(katikati) pamoja na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Sekoutoure, Dk. Bahati Msaki (kulia) alipoenda kukagua huduma zinazotolewa katika mradi wa jengo  la mama na mtoto hivi karibuni.

Dk. Msaki alisema mafanikio hayo yametokana na ongezeko la ubora wa huduma  za afya wanazozitoa hospitalini hapo huku akifafanua kwamba wanawake wanaojifungua  kwa siku moja ni  25 hadi 30  kati yao watatu hadi 10 hujifungua kwa njia ya upasuaji.

“Ongezeko la ubora wa huduma umesababisha kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa kutoka 155,718 mwaka 2014 hadi kufikia 246,627 mwaka 2015 hali hiyo iliibua wazo la kuanza kujenga majengo mapya hususan eneo la huduma ya mama na mtoto  ujenzi ulianza Oktoba mwaka 2017 jengo hili linauwezo wa kubeba vitanda 261ambalo mheshhimiwa Mkuu wa Mkoa unakagua leo huduma tunazozitoa humu.

“Ujenzi wa mradi huu wa jengo la mama na mtoto umefikia asilimia 97 ukikamilika jengo hili litakuwa na vyumba viwili vya upasuaji vikubwa na vya kisasa, mbali na huduma za kina mama jengo litakuwa na eneo la watoto wachanga ambalo limegawanyika katika maeneo manne chumba cha watoto wachanga cha uangalizi maalum (NICU),  waliozaliwa kabla ya mimba kukomaa (KMC) wenye uambukizo( Infectious) na wasiokuwa na uambukizo(NCU),” alieleza Dk. Msaki.

Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza, Costantine Sima  pamoja  na  Diwani Kata ya Isamilo, Charles Nyamasiriri, ambako hospitali hiyo ipo, waliipongeza serikali kwa kutumia rasilimali ardhi vizuri  kujenga jengo hilo la ghorofa kwani linapandisha hadhi ya hospitali hiyo ya mkoa huku wakibainisha kwamba  kukamilika kwa jengo hilo kutawanufaisha wananchi wa Mkoa wa Mwanza hususani wa hali ya chini kiuchumi pia litasaidia kuendelea kupunguza vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi pamoja na  watoto wenye umri chini ya miaka mitano kwa kuwa  madaktari bingwa wataongezeka.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk. Thomas Rutachunzibwa, alisema takribani Sh bilioni 40.2 zinatumika kutekeleza miradi mbalimbali ya sekta ya afya ndani ya mkoa huo ukiwemo wa   Sekoutoure, upanuzi wa hospitali ya Nansio wilayani Ukerewe lengo ni kuiwezesha hospitali hiyo kutoa huduma za kibingwa kama zinazotolewa hospitali ya mkoa, hospitali mbalimba za wilaya zinaendelea kupanuliwa, ujenzi wa zahananti na vituo vya afya.

“Saizi tunaendelea kupokea vifaa tiba kupitia mradi wa ustawi wa taifa na mapambano dhidi ya ugonjwa wa UVIKO 19 pia tunao watumishi wetu ambao tumewapeleka kwenye mafunzo kwa ajili ya kuja kutoa huduma kwenye jengo hili ambalo utalikagua leo mheshimiwa mkuu wetu wa mkoa,” amesema.  

KUWA KWA KIMO NA HEKIMA: Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel,(aliyebeba mtoto) alipotembelea wodi ya wanawake waliojifungua alipoenda kukagua huduma zinazotolewa katika mradi wa jengo  la mama na mtoto lililolojengwa hospitali ya Sekoutoure hivi karibuni wa pili kutoka kushoto ni Meya wa Jiji la Mwanza, Constantine Sima, mwenye shati la kijani ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Nyamagana, Godfrey Kavenga.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Gabriel, aliwasihi wakazi wa mkoa huo, kwenda kupata huduma bora za matibabu hospitalini wanapougua badala ya kuanzia kwa waganga wa tiba asili kwani  serikali inaboresha huduma za afya katika hospitali za mikoa na wilaya ili kusogeza huduma za kibingwa jirani na wanchi lengo ni kuokoa maisha yao na kuwapunguzia gharama za kusafiri mwendo mrefuu kufuata huduma hizo.

“Mnapougua msichanganye miti shamba haina dozi kama unachangamoto ya kiafya anzia kwa wataalam wa afya wao wana mitambo itabaini ugonjwa unaokusumbua siyo kila kitu ni ushirikina ukienda kwa waganga wa kienyeji watakwambia leta ng’ombe umerongwa, pia peleka maombi yako kwa Mwenyezi Mungu,  tumegundua vifo vingi vinatokana na wagonjwa kuchelewa kufika katika hospitali kupata huduma bora za afya,”alisema Mhandisi Gabriel.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles