26.1 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

SEDUCE ME YA KIBA KUITETEMESHA ARUSHA

NA REHEMA SIMON (TUDARCO)

WASANII nyota wa muziki hapa nchini, Ali Kiba, Joh Makini, Dogo Janja, Madee na Lulu Diva, ni miongoni mwa wasanii waliosajiliwa ili kutoa burudani katika tamasha la Tigo Fiesta 2017-Tumekusoma.

Wasanii hao pamoja na wengine lukuki, walisajiliwa katika matukio yaliyofanyika wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, lakini lile la Mbagala Zakheem likionekana kutia fora kutokana na kuwahusisha wasanii wakali hapa nchini, wakiongozwa na Ali Kiba.

Wengine ni Shilole, Jux, Vannesa Mdee, kundi la Weusi likiongozwa na Joh Makini, Stamina, Roma Mkatoliki, Mr Blue, Maua Sama, Fid Q, Harmonize, Rayvanny, Rich Mavoko, Said Kalori na wengineo wengi.

Kati ya wasanii wote hao, Ali Kiba ndiye anayeonekana kuvuta hisia za wengi zaidi jijini humo, huku wimbo wake wa Seduce Me ambao umetokea kubamba vilivyo, ukitarajiwa kufunika.

Lakini mbali ya wimbo huo, pia kuna ule wa Zimbabwe, ulioimbwa na Roma ambapo iwapo mwana hip hop huyo atapanda jukwaani na kuimba, ni wazi vumbi litatimka kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, litakakofanyika tamasha hilo la aina yake.

Kwa mujibu wa waratibu wa tamasha hilo, msimu huu wataanzia kukinukisha jijini Arusha Jumamosi hii, kabla ya kuhamia kwenye maeneo mengine.

Akizungumza jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Mtendaji Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Tigo, William Mpinga, alisema kwa watakaonunua tiketi za tamasha hilo la Jumamosi kwa Tigopesa, watapata punguzo la asilimia 10.

Mpinga aliwashauri wapenzi wa Tigo Fiesta kuchukua fursa hii kupata tiketi zao kwa Sh 9,000 tu, hii ikiwa ni punguzo la asilimia 10 ya bei halisi ya Sh 10,000 kwa watakaonunua kwa fedha taslimu.

“Kununua tiketi ni rahisi. Fuata utaratibu wa kawaida wa kutuma pesa na tuma TZS 9,000 kwenda namba ya TigoPesa 0678 888 888. Hapo hapo utapokea ujumbe mfupi wa SMS unaothibitisha manunuzi yako ya tiketi. Hifadhi huo ujumbe mfupi. Baadaye utapokea maelekezo ya jinsi na wapi pa kwenda kuchukua tiketi yako,” alisema Mpinga.

Aliongeza: “Tigo inajiandaa kutoa ofa nyingine kibao katika msimu huu wa Tigo Fiesta 2017, kwa hiyo wateja wetu na wapenzi wote wa Tigo Fiesta 2017 wakae tayari kufurahia ofa hizi bomba kadri ya tutakavyokuwa tunazitangaza.”

Mwaka huu msimu wa Tigo Fiesta 2017 – Tumekusoma utajumuisha mikoa ya Arusha, Kahama, Musoma, Mwanza, Tabora, Dodoma, Iringa, Songea, Njombe, Sumbawanga, Morogoro, Tanga, Moshi na Mtwara, kabla ya kuhitimishwa jijini Dar es Salaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles