27.4 C
Dar es Salaam
Sunday, April 14, 2024

Contact us: [email protected]

SCORPION AHUKUMIWA MIAKA 7 JELA, FAINI MIL. 30

Na KULWA MZEE-DAR ES SALAAM


MWALIMU wa sanaa ya kujihami, ‘Martial arts’ Salum Njwete maarufu Scorpion amenusurika kwenda jela miaka 30 kwa unyang’anyi wa kutumia silaha badala yake anakwenda jela miaka saba na kulipa fidia ya Sh milioni 30 kwa kujeruhi kwa kumtoboa macho Said Mrisho.

Scopion alitiwa hatiani jana katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala mbele ya Hakimu, Flora Haule, kwa kumjeruhi Saidi Mrisho kwa kumtoboa macho.

Mahakama hiyo ilimuachia huru kwa shitaka la unyang’anyi wa kutumia silaha baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha tuhuma za unyang’anyi wa kutumia silaha.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Haule alisema upande wa mashitaka ulikuwa na mashahidi 10 huku mshtakiwa akijitetea mwenyewe.

“Mshtakiwa umetiwa hatiani kwa kifungu namba 225 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

“Mahakama imejiridhisha kuwa mlalamikaji, Said Mrisho alishambuliwa kutokana na majeraha mbalimbali kwenye mwili wake ambayo madaktari walithibitisha.

“Mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa kwamba mshtakiwa ndiye aliyemjeruhi mlalamikaji na ni kinyume na sheria kujeruhi au kumuadhibu mtu hata kama ana makosa.

“Ushahidi umeonyesha Scorpion alikuwa anajishughulisha na ulinzi ambako uhalifu eneo la Buguruni umepungua kwa kazi yake,” alisema Hakimu Haule.

Alisema dhamira ya mshtakiwa ilikuwa ni kupambana na mtu aliyemdhania kuwa ni mhalifu na siyo nia yake kuiba, hata hivyo hakuna shahidi aliyeeleza kama mshtakiwa aliiba.

Wakili wa Serikali, Frank Tawale aliiomba mahakama kutoa adhabu inayostahiki kwa mshtakiwa kwa kuzingatia ulemavu aliomsababishia mlalamikaji.

Alidai kuwa taifa limepoteza nguvu kazi kwa mlalamikaji kupata majanga hayo na kwamba familia inamtegemea ikizingatiwa hawezi kuwajibika na ndoto zake zimefifia.

Akitoa utetezi, Wakili wa utetezi, Hussein Hitu aliomba mahakama impunguzie adhabu mshitakiwa kwa kuwa ni kosa lake la kwanza na ni mtu mwema kwa kuwa hata ushahidi umeeleza kuwa uhalifu eneo la Buguruni ulipungua.

Hitu alidai mshtakiwa ana familia inayomtegemea hivyo iangalie adhabu itakayotoa mshitakiwa aendelee na shughuli nyingine.

Inadaiwa kuwa Septemba 6, 2016 maeneo ya Buguruni Sheli wilayani Ilala, Dar es Salaam, Scopion aliiba mkufu wa dhahabu gramu 38 yenye thamani Sh 60,000 bangili ya mkononi Sh 331,000 na pochi, vyote vina thamani ya Sh 476,000, mali ya Mrisho.

Pia inadaiwa kabla ya wizi huo, mtuhumiwa alimchoma na kisu tumboni, mgongoni na machoni ili kujipatia mali hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles