29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

SAUTI YA ALI KIBA ILIVYOMGUSA YVONNE CHAKACHAKA

Na BADI MCHOMOLO


WAHENGA husema kuwa vizuri hujiuza na vibaya hujitembeza. Msemo huu unaonekana katika mambo mengi ikiwamo sanaa ya muziki wa Bongo Fleva ambao kwa sasa unaonekana kuitangaza vyema nchi ndani na nje.

Muziki huo unasaidia kuitangaza vyema nchini, huku ikisaidia kuongeza idadi ya watalii ikiwemo wasanii, waongozaji wa filamu za muziki huo wanaokuja kufanyia shughuli zao hapa nchini na wasanii wanaopata mialiko kwa ajili ya kushiriki matamasha ama kushiriki kazi za baadhi ya wasanii nchini.

Baadhi ya wasanii wanaojitangaza ndani na nje ya nchi huku wakipata nafasi ya kushirikiana na wasanii wenye majina makubwa duniani, ni pamoja na Nasib Abdul (Diamond), Ambwene Yessaya (AY), Judith Wambura (Jay De) na Ali Kiba ambaye hivi karibuni anatarajia kuachia wimbo wake akiwa ameshirikiana na mwanamuziki mashuhuri nchini Afrika Kusini anayetambulika duniani kutokana na nyimbo zake kutumika kipindi cha ukombozi wa Afrika Kusini.

Ali Kiba alivyokutana na Yvonne Chakachaka

Wiki iliyopita, Ali Kiba alitoa video ya wimbo wake wa ‘Aje Remix’, video ambayo ilitazamwa na watu milioni tano kwa kipindi kifupi, jambo ambalo lilifurahisha uongozi wa Kampuni ya Sony Music yenye maskani yake nchini Afrika Kusini.

Mafanikio hayo yaliifanya Sony Music inayosimamia usambazaji wa kazi za msanii huyo kumwita nchini Afrika Kusini kwa ajili ya kumpatia zawadi hiyo.

Baada ya kupewa tuzo hiyo, msanii huyo alifanikiwa kukutana na nguli wa muziki Afrika na dunia kwa ujumla, Mama Yvonne Chakachaka aliyetamba na nyimbo zake mbalimbali za ukombozi.

Ilikuwa kama bahati nzuri kwa Ali Kiba kukutana na mkongwe huyo mwenye miaka 52 ambaye baada ya kuzungumza naye na kuomba asikilize baadhi ya nyimbo zake, alivutiwa na sauti ya Ali Kiba kiasi cha kupenda kufanya naye kazi.

Yvonne Chakachaka anapenda zaidi wimbo wa Aje wa msanii Ali Kiba, huku akisema kilichomvutia zaidi ni sauti ya msanii huyo kiasi cha kukubali kufanya naye kazi, huku muda mwingi akiutumia nyumbani kwake na kula chakula pamoja na Ali Kiba akimuona kama mtoto wake.

Mbali ya kuwa mwanamuziki, Yvonne Chakachake ni mwalimu, mwandishi wa nyimbo na mfanyabiashara na hivyo kupata muda mchache sana wa kupumzika.

Ilikuwa kazi rahisi kwa Ali Kiba kukubaliwa ombi lake la kufanya kazi na mwanamama huyo anayemchukulia Ali Kiba kama mtoto wake na kwa kuwa yeye ni mama hawezi kumwacha arudi Tanzania bila ya kufanya naye kazi.

“Baada ya Ali Kiba kukutana na kuomba tufanye kazi pamoja, nilimchukua hadi nyumbani kwangu, nilijiona nipo na mwanangu na mimi ndio mama.

“Nilipika chakula tukala pamoja kama mtu na mtoto wake, tuliongea mengi sana kuhusu muziki, baada ya hapo tukaanza kubadilishana mawazo juu ya aina ya muziki ambao tunatakiwa kuufanya, Ali Kiba ni msanii wa kipekee na ana uwezo wa aina yake, nimefurahi sana kufanya kazi na mwanangu kutoka Tanzania.

“Watu kutoka nchini Afrika Kusini wanampenda sana msanii huyo kama ilivyo Tanzania, nadhani Ali Kiba alikuwa na furaha sana kuonana na mama yake ambaye ni mimi, kilichobaki ni kusubiri kuona nini kinakuja kati yetu,” alisema Mama Chakachaka na kuongeza:

“Ali Kiba ni msanii anayefanya vizuri sana, ninaamini atakuja kufanya makubwa duniani hivi karibuni.”

Kabla ya mafanikio hayo, Ali Kiba alipewa tuzo ya 2016 MTV EMA’s kama msanii bora wa Afrika ambayo awali alipewa mkali kutoka nchini Nigeria, Wizkid kimakosa.

Historia ya Yvonne Chakachaka

Yvonne Chakachaka ni msanii aliyetajwa miongoni mwa wanawake 100 duniani wenye ushawishi mkubwa kwa jamii na wakaeleweka.

Mwaka 1981, alikuwa msanii wa kwanza mweusi nchini Afrika Kusini kuonekana kwenye runinga na baada ya hapo nyota yake ilizidi kung’aa na kufanya shoo mbalimbali na wasanii waliokuwa wakitamba katika muziki kipindi hicho akiwemo Paul Hewson ‘Bono’ kutoka visiwa vya Ireland, Annie Lennox kutoka nchini Scotland na Youssou N’Dour kutoka Senegal.

Alipokuwa na miaka 27 tu, alizidi kutikisa nchi za Afrika hasa Zimbabwe, Kenya, Gabon, Sierra Leone na Ivory Coast na Tanzania akitamba na nyimbo zake kame vile ‘I’m Burning Up’, ‘Thank You Mister DJ’, ‘I Cry for Freedom’, ‘Makoti’, ‘Motherland’ na nyinginezo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles