Riyadh, Saud Arabia
SERIKALI ya Saudi Arabia imezuia wageni wote wanaoingia nchini humo kwa safari za kidini, ikiwemo wanaotembelea miji mitakatifu katika dini ya Kiislamu – Makka na Madina.
Mamilioni ya watu huingia Saudia mwaka mzima kufanya ibada ya Umra, na wengi zaidi huingia kwa pamoja kufanya ibada ya Hija.
Tofauti na Hija, Umra (ambayo pia hufahamika kama Hija ndogo) hufanyika katika kipindi chochote cha mwaka, na kwa sasa marufuku hiyo inawalenga mahujaji raia wa nchi za nje wanaoenda kuitekeleza.
Bado haijulikani kama ibada ya Hija, ambayo inategemewa kuanza mwishoni mwa mwezi Julai kama itaathirika na zuio hilo pamoja na kusambaa kwa virusi vya corona duniani.
Wizara ya mambo ya nje ya Saudia inasema marufuku hiyo ni ya muda – lakini wizara hiyo haijataja lini marufuku hiyo itaondolewa.
Saudia pia imewapiga marufuku watu kutoka nchi zilizokumbwa na virusi hivyo kuingia nchini humo.
Watalii ambao si wa kidini ambao wanatoka katika nchi ambazo virusi vya corona vimethibitisha kuingia pia watakataliwa kuingia Saudia.
Msikiti wa Madina ni wa pili kwa utukufu katika Uislamu na ndipo alipozikwa Mtume Muhammad.
Makka, ndio mji ambao Mtume Muhammad alipozaliwa, na kuna msikiti mtakatifu zaidi. Madina ndipo alipofariki na kuzikwa.
Hadi sasa Saudia bado haina mtu ambaye amethibitika kuambukizwa virusi hivyo.
Saudi Arabia imeeleza kuwa tangu mwezi Oktoba imetoa viza zaidi ya 400,000 za watalii kutoka nchi mbali mbali duniani.
Shirika la Afya Duniani (WHO) mapema wiki hii limeonya kuwa dunia inapaswa kujiandaa kwa uwezekano wa janga la virusi vya corona.
WHO japo imesema kuwa ni mapema sana kuuita mlipuko wa virusi hivyo janga lakini nchi zinapaswa kuwa katika “awamu ya maandalizi”.
Janga ni pale maambukizi ya ugonjwa yanaposambaa kwa urahisi kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine katika maeneo mengi ya dunia.
Visa zaidi vya virusi ambavyo husababisha ugonjwa kupumua Covid-19, vinaendela kujitokeza, huku milipuko ya ugonjwa huo ikibainika katika mataifa mengi zaidi ya China ambapo ndipo ulipoanzia.
Hadi sasa zaidi ya watu 2,700 wameshafariki dunia kutokana na ugonjwa wa Covid-19.
Tangu virusi vya corona viripotiwe mwezi Disemba, zaidi ya watu 80,000 duniani, kutoka katika mataifa takribani 40 tayai wameshaambukizwa virusi hivyo. Wengi wao wakiwa nchini China.
Iran ambayo imetenganishwa na Saudia kwa mkondo mwembamba wa bahari hadi sasa imesharipoti vifo 19 – ambavyo ni namba kubwa zaidi ya watu kwa mataifa ya nje ya China.
Hata hivyo vifo hivyo vinatokana na wagonjwa 139, hali ambayo inawafanya madaktari wa magonjwa ya kuambukiza kuhofia kuwa nchi hiyo inaweza kuwa na wagonjwa wengi zaidi inaowaficha.
Barani Ulaya hali ni mbaya zaidi nchini Italia ambako hadi sasa watu 400 wamethibitika kuambukizwa ugonjwa huo kutoka watu 80 siku ya Jumanne.
Watu 12 tayari wameshafariki nchini humo kutokana na mlipuko huo.
Kwa Afrika ni nchi mbili hadi sasa zimethibitisha kuingia kwa ugonjwa huo.
Algeria na Misri kila moja imeripoti mgonjwa mmoja.