26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Waitara atangaza kugombea ubunge Tarime Vijijini

Peter Fabian – Tarime

MBUNGE wa Ukonga, Dar es Salaam, Mwita Waitara (CCM), ametangaza kugombea ubunge Jimbo la Tarime Vijijini mkoani Mara, akidai ametumwa na Rais Dk. John Magufuli.

Waitara ambaye ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), aliyejichimbia kwa muda akifanya vikao ndani na mikutano ya hadhara, alitangaza uamuzi wake huo hivi karibuni wilayani Tarime alipokutana na viongozi wa chama na jumuiya, wenyeviti wa vitongoji na vijiji kuanzia ngazi ya mashina, matawi na kata.

Aliwaeleza wajumbe hao zaidi ya 700 kuwa ameamua kurudi nyumbani kugombea, huku akitamba yeye ndiye mtu pekee ndani ya CCM mwenye uwezo na nguvu za kukomboa jimbo hilo kutoka Chadema.

Jimbo hilo kwa sasa linaongozwa na John Heche (Chadema) aliyeshinda katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

“Niseme nisiseme au kuna mtu atanuna humu ndani, si mnajua nakuja nyumbani au ngoja niseme tu, naogopa nini, mie nagombea ubunge Jimbo la Tarime Vijijini, mchakato utafanyika wa kura za maoni, kisha utaratibu wa vikao vya wilaya utapitia.

“Itafikia hatua ya mkoa na mwisho vikao vya juu vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM kuteua jina moja ambalo ni la Waitara, kisha NEC wanatuunganisha na upinzani kuanza kampeni za miezi mitatu kabla wananchi kutupigia kura Oktoba, mwaka huu,” alisema Waitara.

Waitara ameendelea kufanya vikao vya kukutana na baadhi ya wajumbe wa mkutano mkuu wa wilaya, akitumia ushawishi wa kutoa ahadi kedekede, kuwapatia nauli na wakati mwingine kuchinja mifugo na kuandaa chakula na vinywaji baridi, akidai ni sehemu ya kubadilishana mawazo na kuweka mikakati ya kuunda timu ya watu watakaomsaidia kumtafutia kura kwa wajumbe wa mkutano mkuu ili kumuwezesha kuibuka mshindi wa kura za maoni ndani ya chama hicho.

“Nasikia kuna watu wengine wana vitambi na wana hela nao wameonyesha nia na kusema watakuja kugombea, naomba niwambie hawatanishinda, hawana uwezo wa kurejesha jimbo hili ambalo lilichukuliwa na Heche kirahisi,” alisema Waitara.

Akizungumza na gazeti hili, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Samwel Kiboye baada ya kutafutwa na mwandishi wa habari hii kutaka kujua taratibu na kanuni za chama hicho, na kuwepo kwa taarifa kuhusu Waitara kutangaza kugombea, alikiri kupokea taarifa hizo na kusema tayari wamepokea ushahidi na watamwita kwenye vikao ngazi ya wilaya na mkoa.

Alisema anasikitishwa na makada na wanachama wanaotumia vibaya jina la mwenyekiti wao kuwa amewatuma.

Katibu wa CCM Wilaya ya Tarime, Hamisi Mkaruka alipopigiwa simu kuhusu hali hiyo alisema haoni shida ya makada kupita pita jimboni kutangaza nia kwa kuwa majimbo ya Tarime Vijijini na Tarime Mjini yanaongozwa na wabunge wa upinzani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles