26.7 C
Dar es Salaam
Monday, June 24, 2024

Contact us: [email protected]

Saruji Tanga kuifufua reli

saini 1Na Amina Omari, Tanga

LICHA ya miundombinu ya barabara kuboreshwa usafiri wa reli bado unapaswa kuwapo kutokana na umuhimu wake hasa katika kurahisisha usafirishaji.

Mizigo mingi inayosafirishwa na malori, iwe ndani ama nje ya nchi, inaweza kusafirishwa kwa njia ya reli na kuondoa msongamano wa malori pamoja na makontena bandarini kama ilivyo sasa.

Usafiri wa gari moshi bado una umuhimu katika usafirishaji kwani gari moja linaweza kubeba hadi makontena 50 yenye urefu wa futi 40 kwa mara moja, hivyo kurahisisha usafirishaji na kupunguza gharama za uchukuzi wa mzigo huyo.

Rais Dk. John Magufuli aliahidi kuimarisha mtandao wa reli kama alivyofanya kwenye barabara wakati akiwa waziri wa ujenzi.

Ikiwa ni pamoja na kuwashawishi wazalishaji wa viwanda nchini kutumia njia za reli kusafirishia shehena ya bidhaa zao kwenda ndani na hata nje ili kudhibiti uharibifu wa barabara lakini kupunguza gharama za usafirishaji.

Ahadi hiyo imeanza kutekelezwa baada ya hivi karibuni Kampuni ya Saruji Tanga kusaini mkataba wa makubaliano na Shirika la Reli Tanzania (TRL) kusafirisha tani 35,000 za saruji kwa njia ya reli.

Makubaliano hayo ambayo yalishuhudiwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, yalifanyika katika kiwanda hicho kilichopo Tanga.

Makubaliano hayo yataongeza safari za TRL katika njia ya Tanga na kuipatia kampuni hiyo suluhisho la usafirishaji wa shehena ya bidhaa ya saruji inayozalishwa na kiwanda hicho kwa gharama nafuu.

Waziri Mbarawa anasema kupitia makubali hayo TRL imeandika historia mpya kwa kuanza tena kusafirisha shehena kubwa ya mzigo kama hapo zamani.

Anasema kwa kipindi cha zaidi ya miaka mitano toka kurejea tena shirika hilo limekuwa likisafirisha shehena ya mizigo tani 150,000 hadi 200,000 kwa mwaka pekee.

“Hivyo kwa usafirishaji wa tani 35,000 kwa mwezi ina maana kwa mwaka mzima TRL itakuwa na uwezo wa kusafirisha saruji tani 420,000 mzigo ambao ni mkubwa kuwahi kusafirishwa na shirika hilo kwa kipindi kirefu,” anasema Profesa Mbarawa.

Anasema kupitia usarifishaji huo shirika linatarajiwa kutengeneza faida ya Sh milioni 40 kwa kusafirisha shehena ya mzigo kwa mwezi kutoka Tanga – Kigoma – Mwanza.

“Lengo la serikali ni kuwezesha viwanda vyetu kuzalisha kwa wingi lakini pia kuweka miundombinu bora ambayo itawezesha bidhaa kumfikia mlaji kwa haraka na kwa gharama nafuu ili kuwakomboa wananchi wetu kiuchumi,” anasema.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TRL, Masanja Kadogosa, anasema makubaliano hayo yatawezesha shirika lake kusafirisha shehena ya saruji inayozalishwa kiwandani hapo kwa urahisi na kuisambaza maeneo mbalimbali.

Anasema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji ambao walishauanza mwaka 2014/15 ambapo kiwanda cha saruji kiliweza kusafirisha tani 44,000 kupitia njia ya reli.

Hivyo kufuatia ongezeko la shehema hiyo shirika lake limeweza kutenga vichwa vitano vya treni na kimoja cha shanta maalumu kuhudumia kampuni hiyo ya saruji.

“Tunatarajia kusafirisha shehena ya saruji zaidi ya tani 20,000 kwa mwezi kutoka kiwandani hapo hadi Kigoma na tani 15,000 kutoka Pongwe kuelekea Mwanza,” anasema Kadogosa.

Anasema kiwanda hicho kitakuwa kimepata suluhisho madhubuti la usafirishaji wa mizigo mikubwa na mizito jambo litakalowanufaisha wateja wa kampuni hiyo na Watanzania

Mkurugenzi huyo ameiomba kampuni hiyo kulipa gharama za usafirishaji kwa wakati ili kusaidia shirika hilo kutoa huduma bora.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Reinhardt Swart, anasema mkataba huo utawezesha kusafirisha saruji tani 35,000 ujazo ambao ni theluthi ya tani 105,000 inayozalishwa kiwandani hapo kwa mwezi.

Anasema kampuni yake itaongeza ufanisi katika uzalishaji ili kuleta ushindani katika soko pamoja na kupunguza gharama za usafirishaji.

“Kumekuwapo na malalamiko kwa wateja wetu kuhusu gharama za saruji lakini tulikuwa tunatumia gharama kubwa katika usafiri kwa njia ya barabara, ambapo wakati mwingine bidhaa ilikuwa inachelewa kufika kwa wakati kutokana na changamoto zilizopo barabarani,” anasema Swart.

Swart anasema matumizi ya reli yanazingatiwa duniani kote kama njia stahiki ya usafirishaji yenye gharama nafuu na athari ndogo za kimazingira ukilinganisha na usafiri wa barabara.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigella, anasema mkoa utaendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji ili wawekezaji hao waendelee kuwekeza na kuongeza pato la uchumi la mkoa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles