28.7 C
Dar es Salaam
Thursday, June 13, 2024

Contact us: [email protected]

Baada ya ahueni ya madeni, Afrika yarejea ilikotoka

Mzigo wa madeni huzikosesha uhuru serikali kutumia fedha kuboresha hali za wananchi wakeJOSEPH HIZA, DAR ES SALAAM

USTAWI katika nyanja mbalimbali za maisha ni ndoto za taifa lolote lile duniani, achana na njozi za baadhi ya watawala wenye fikira za kujinufaisha wao binafsi.

Kuna mambo yanayoweza kukwamisha ustawi huo, ikiwa ni pamoja na umasikini ambao husababishwa na sababu kama vita, ufisadi na usimamizi mbovu wa uchumi.

Lakini pia kuna sababu nyingine zinazoweza kukwamisha taifa kujikwamua kutoka katika umasikini huo licha ya jitihada fulani, nazo ni pamoja na mzigo wa deni usio himilivu.

Nusu ya watu milioni 600 wanaoishi katika mataifa 40 masikini zaidi duniani, ambayo mengi yalikuwa na mzigo mkubwa wa madeni yasiyolipika, huishi chini ya dola moja kwa siku.

Wengi hufa mapema, wana uchache wa shule na walimu na huishi kwa njaa na maradhi kuliko wenzao katika mataifa mengine yanayoendelea.

Kwa sababu hiyo, Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF) na Benki ya Dunia (WB) walikuja na mpango wa msamaha wa madeni katika mataifa masikini yenye madeni makubwa yasiyolipika (HIPC).

Katika mpango huo yalipatikana mataifa 38 yenye kiwango kikubwa cha madeni, ambacho kiliangukia katika eneo linalostahili msaada maalumu kutoka vyombo hivyo iwapo yatafuzu masharti.

Mpango huo wa nchi za HIPC ulianzishwa na IMF na WB mwaka 1996, kufuatia harakati kali za ushawishi zilizofanywa na asasi zisizo za kiserikali na vyombo vinginevyo.

Ulilenga kutoa nafuu ya deni na mikopo ya masharti nafuu ili kufuta au kupunguza madeni ya nje kwa viwango himilivu, ikimaanisha nchi zinaweza kukopa kwa namna zinazokubalika siku za usoni.

Hilo lingesaidia pia mataifa hayo kuwa na uhuru wa kuzitumia fedha ambazo zilipaswa kurejeshea madeni kwa masuala mengine ya kimaendeleo na kijamii.

Msaada huo una masharti kwa kuzitaka nchi zifikie viwango vya usimamizi wa uchumi na ufanisi pamoja na mageuzi ya kiuchumi na kijamii.

Kufikia Januari 2012, mpango wa HIPC ulitambua mataifa 39, ambayo 33 kati yao yanatoka Kusini mwa Jangwa la Sahara Afrika kuwa stahili kupokea msamaha huo wa madeni.

Mataifa hayo Tanzania ikiwamo zilipokea msamaha wa deni lote au sehemu ya deni.

Hata hivyo, kinachotia wasiwasi kwa sasa baadhi ya mataifa hayo baada ya kufuzu na kusamehewa yanaonekana sasa kurejea kule yalikotoka, yakionekana kutojifunza kutokana na makosa.

Tanzania pamoja na kuonekana kutojifunza kutokana na mwelekeo wa deni lake kukua mwaka hadi mwaka kufikia Sh trioni 29 kutoka Sh trilioni 10 mwaka 2005, haimo miongoni mwa mataifa yaliyotajwa kuwa katika tishio kubwa la kuangukia tena katika zigo kubwa la madeni yasiyolipika.

Miongoni mwa mataifa yanayokumbwa na tishio zaidi la kuongezeka kwa viwango vyao vya ukopaji kimataifa ni pamoja na Burundi, Cameroon, Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), Chad, Ghana na Mauritania, Sao Tome na Principe ambayo yalikuwa sehemu ya mataifa yale 38 ya HIPC.

 

Baadhi ya mataifa ya Afrika yanakabiliwa tena na jinamizi la malimbikizo ya madeni kwa mujibu wa wachambuzi wa masuala ya uchumi duniani.

Mataifa katika eneo la kusini mwa jangwa la Sahara yaliyokopa nje sasa yanakabiliwa na hali ngumu kiuchumi huku thamani ya bidhaa ikiporomoka.

Wasiwasi huo unakuja miaka 20 tangu kufanyika kwa kampeni ya ushawishi duniani kote ya kuyafutilia mbali madeni hayo sugu.

Julien Marcilly, mchumi mkuu wa mashirika ya Coface nchini Ufaransa yanayotoa bima kwa mataifa yanayokabiliwa na madeni makuu kote duniani kuyaepusha dhidi ya kushindwa kulipa, anasema hali hii inayozua wasiwasi mkubwa haikutarajiwa.

Kupitia HIPC, IMF tangu ianzishe mpango huo mwaka 1996 kufikia sasa iliidhinisha dola bilioni 68 kusaidia mataifa 36 yasiyojiweza kulipa madeni yao ya nje ambapo 30 kati ya mataifa hayo yanatoka Afrika.

Kinachotia hofu ni kuwa mataifa hayo yanaendelea kukopa madeni kiholela kwa viwango vya juu mno.

Baada ya kupata ahueni ya kulipiwa madeni yao na mpango wa shirika hilo, baadhi ya mataifa yalifurahia uhuru wa bajeti zao kunawirisha chumi zao ambazo tayari zilikuwa zimekumbwa na mfumuko mkubwa wa bei.

Kwa mujibu wa wachambuzi wa uchumi, hali hii imechangiwa na Afrika kuagiza bidhaa nyingi zaidi kuliko inazouza katika masoko ya dunia.

Katika miaka michache iliyopita, mataifa katika eneo la kusini mwa jangwa la Sahara yameshiriki uuzaji wa hati fungani kama njia ya kujipatia fedha kuendeleza bajeti zao, mengine yakishiriki katika utaratibu huo kwa mara ya kwanza.

Hata hivyo, ripoti ya hivi karibuni kutoka Shirika la Viwango la Standard and Poors inasema hiyo si njia nzuri ikizingatia baadhi ya nchi ziliuza hati fungani zake wakati viwango vya thamani ya hati hizo zikiwa chini bado.

Ripoti hiyo imeonya kuwa hali imebadilika na mataifa husika yatahitajika kutumia fedha zaidi katika miaka mitatu ijayo kulipa madeni yao, na kwamba mataifa mengi katika eneo la kusini mwa jangwa la Sahara yatakumbwa na uamuzi mgumu kati ya kupunguza matumizi yao na kulazimika kulipa madeni kwa riba za juu siku za usoni.

Mbaya zaidi kipindi hiki mengi ya madeni hayo yametokana na mashirika ya binafsi, yenye riba kubwa badala ya IMF au WB katika kile kinachoonekana baada ya kushindwa kufuzu masharti ya kukopeshwa.

Hadithi hii kwa kiasi fulani inaoana na kashfa iliyoikumba Tanzania wakati wa utawala uliopita baada ya kushindwa kupata mkopo kwa njia ya kawaida kutokana na hati zake fungani kukosa sifa.

Hivyo basi, Benki ya Stanbic, tawi la Tanzania ikiliona hilo kuwa dili, ikajitosa kutoa ofa ya kuisaidia serikali kupata mkopo huo kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambayo haijafahamika bado.

Katika hilo Benki ya Standard ilikubali kuipokesha Serikali ya Tanzania Dola milioni 600 sawa na Sh trilioni 1.3 mwaka 2012 kwa masharti ya kulipwa riba ya asilimia 1.4.

Lakini Stanbic, iliongeza asilimia moja na hivyo kufanya serikali kutakiwa kulipa riba ya asilimia 2.4, ambayo ni Sh bilioni 12.

Matokeo ya hali hiyo ni mzigo kwa taifa, ambao unatakiwa kulipwa na walipakodi masikini, ilihali fedha hizo zilizoongezwa hazikuwanufaisha bali ziliingia katika mifuko ya watu binafsi.

Aidha Shirika la Standard and Poors linasema kudorora kwa thamani ya sarafu za mataifa katika eneo la kusini mwa jangwa la Sahara, kunakohusishwa na kupungua kwa bei za bidhaa, kumechangia kuongezeka kwa viwango vya madeni katika sarafu za kimataifa.

Lingine ni nidhamu mbovu ya udhibiti wa bajeti.

Utafiti uliofanywa na Wizara ya Fedha nchini Ufaransa umeonyesha mpango wa IFM kwa ushirikiano na WB ulipunguza madeni ya mataifa 30 ya Afrika kutoka asilimia 119 hadi 33 kila mwaka.

Miongoni mwa mataifa 30 yaliyopata msaada kuwawezesha kulipa madeni ya nje, 13 kati yao yameongeza viwango vyao vya mikopo kwa asilimia 10 kila mwaka katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) iliongoza orodha hiyo kwa asilimia 25, ikifuatwa na Niger asilimia 23 na Malawi kwa asilimia 19.

Huku ikionya mataifa mengine huenda yakarejea hali ya awali ya miaka 20 kabla ulimwengu kufutilia madeni ya mataifa masikini na yatakwamisha mipango ya kustawisha nchi hizo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles