Na WAANDISHI WETU, DAR NA MIKOANI
BEI ya simenti imeanza kupanda katika baadhi ya maeneo nchini, imefahamika.
Uchunguzi uliofanywa na MTANZANIA unaonyesha kuwa bei hiyo imepanda zikiwa ni siku chache baada ya kiwanda cha simenti cha Dangote kilichoko mkoani Mtwara, kusimamisha uzalishaji kutokana na gharama kubwa ya uzalishaji.
Taarifa zilizopatikana mkoani Mtwara zinasema mfuko wa simenti umepanda kutoka Sh 11,500 hadi Sh 17,000.
Mmoja wa wafanyabiashara wa simenti mjini Mtwara, Abdallah Said, aliiambia MTANZANIA, kwamba kupanda kwa bidhaa hiyo kumesababishwa na Kiwanda cha Dangote kusimamisha uzalishaji.
Said alisema kuna haja Serikali kuangalia namna ya kutatua mgogoro uliopo kati yake na mmiliki wa kiwanda hicho.
DODOMA
Mjini Dodoma, bei ya jumla ya mfuko mmoja wa simenti hadi jana ni Sh 12,500 na rejareja ni kati ya Sh 13,500 na 14,000.
Akizungumza na MTANZANIA katika eneo la Uwanja wa Jamhuri, mfanyabiashara wa jumla ambaye ni wakala mkuu wa kusambaza simenti mkoani Dodoma, Fred Mushi wa Kampuni ya Priscus Alexander Company Limited (PACL), alisema bei ya jumla ya mfuko mmoja wa saruji ni Sh 13,500 hadi Sh 14,000.
Katika maelezo yake, Mushi alisema bei hiyo imepanda kutoka Sh 12,500 iliyokuwa ikiuzwa hivi karibuni.
Kauli hiyo ya Mushi iliungwa mkono na mfanyabiashara, Muhommed Fahkim wa Kampuni ya Fasam General Supply.
MOROGORO
Mjini Morogoro, bei ya mfuko mmoja wa simenti nayo imepanda kutoka Sh 12,000 na Sh 12,500 hadi Sh 13,000 na Sh 13,500 kufikia jana.
Mmoja wa wafanyabiashara wa bidhaa hiyo wilayani Gairo, mkoani Morogoro, Samuel Kivanda, alisema bei hiyo ni katika wilaya za Kilombero, Ulanga na Kilosa.
TANGA
Mkoani Tanga, bei ya mfuko mmoja wa simenti uliokuwa ukiuzwa kwa Sh 13, 000 hadi Sh 14,000, imeshuka hadi Sh 11500.
Baadhi ya wafanyabiashara mjini hapa waliozungumza na MTANZANIA jana, walisema bei hiyo imeshuka kutokana na viwanda viwili vya simenti mjini hapa kuzalisha bila kusimama.
Mmoja wa wafanyabiashara hao, Shaban Ally kutoka Barabara ya 20 Tanga, alisema mjini hapa saruji iliyokuwa ikiuzwa kwa Sh 14, 000 na Sh 15,000 sasa inauzwa kwa Sh 13, 000 hadi Sh 12,500.
MBEYA
Jijini Mbeya nako bei ya bidhaa hiyo kwa mfuko mmoja imeshuka kutoka Sh 18,000 hadi Sh 14,500.
Kwa mujibu wa baadhi ya wakazi wa jijini hapa waliozungumza na MTANZANIA, mfuko mmoja wa simenti ya Tembo inayozalishwa mjini hapa iliyokuwa ikiuzwa kwa Sh 15,000, kwa sasa inauzwa Sh 14,500 kwa mfuko mmoja.
Mmoja wa wafanyabiashara hao, mkazi wa Soweto mjini hapa, Nsaji Mwakilili, aliiambia MTANZANIA, kwamba mfuko wa simenti aina ya Nyati uliokuwa ukiuzwa Sh 18,000, umeshuka na kuuzwa kati ya Sh 16,000 na Sh 17,000.
ARUSHA
Jijini Arusha, bei ya mfuko mmoja wa saruji imeendelea kuuzwa kwa Sh 13,500 na bei hiyo imeelezwa kuwa imeendelea muda mrefu bila kubadilika.
Akizungumza na MTANZANIA mjini hapa jana, mmoja wa wauzaji wa simenti eneo la Mji mpya la Burka City, Abdallah Rashid, anashangaa bei hiyo kutobadilika kwa muda mrefu sasa.
KILIMANJARO
BEI ya bidhaa hiyo katika maduka ya rejareja mkoani hapa, imeshuka kutoka Sh 12,500 hadi Sh 11,900 kwa mfuko mmoja wa kilo 50.
Baadhi ya wafanyabiashara waliozungumza na MTANZANIA kwa nyakati tofauti, walisema simenti iliyoshuka bei ni ya kampuni zinazozalisha bidhaa hiyo katika mikoa ya kaskazini.
TIC NA DANGOTE
Wakati hayo yakiendelea, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kimevunja ukimya na kuzungumzia hatua ya Dangote kusimamisha uzalishaji wa simenti kwa kinachoelezwa kuwa ni kupanda kwa gharama za uzalishaji.
Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, Meneja Uhusiano kwa Umma wa Kituo hicho, Pendo Gondwe, alisema wamekwisha kukutana na uongozi wa Kiwanda cha Dangote na kuzungumzia madai yao.
Kwa mujibu wa Gondwe, uwekezaji uliofanywa na Dangote ni mkubwa hivyo Serikali siyo rahisi kukubali asimamishe uzalishaji kwa sababu zozote zile zikiwamo gharama kubwa za uzalishaji.
“Kampuni ya Dangote ilipokewa na kituo hiki na ikapewa huduma zote za kuiwezesha kufanikisha uzalishaji.
“Hiyo ni kampuni kubwa ambayo ina uwezo wa kuzalisha ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja zinazofikia 6,000 kama itafanya uzalishaji kwa kiwango kilichokusudiwa.
“Kwa hiyo, tayari tumezungumza nao, tumejiridhisha na tumefikia hatua ya kuamua kwenda kutembelea kiwanda chake baada ya siku 10 kuanzia sasa kwa kuwa uzalishaji utakuwa umerejea.
“Lengo letu la kwenda huko ni kuangalia changamoto zilizopo zinazoweza kuathiri uzalishaji wake,” alisema Gondwe.
Akizungumzia taarifa zilizosema mwekezaji huyo alipewa baadhi ya vivutio na Serikali ya awamu ya nne ambavyo vimeondolewa na Serikali iliyoko madarakani, Gondwe alisema kwa mwekezaji wa aina ya Dangote, lazima apewe vivutio.
“Wako wawekezaji na wawekezaji mahiri ambao kwa utaalamu hufahamika kama ‘strategic investors’. Kampuni ya Dangote ni moja ya wawekezaji mahiri na ambao kwa kawaida hupewa vivutio maalumu.
“Kwa taarifa yako ni kwamba wanaopewa vivutio hivyo ni wawekwzaji wenye mtaji unaofikia Dola za Marekani milioni 50 na Dangote uwekezaji wake unafikia Dola za Marekani milioni 500.
“Katika kutoa vivutio hivyo, pia huwa tunaangalia ajira zinazoweza kuwapo kutokana na uwekezaji huo na pia uwekezaji ambao hufanyika maeneo ya vijijini na umbali kutoka eneo yanapopatikana masoko makubwa, nao hupewa vivutio.
“Kwa kuwa tumekuwa na nia njema kwa wawekezaji, tumekuwa tukishirikiana na sekta binafsi kuondoa changamoto zinazowakwamisha uwekezeji katika sekta mbalimbali nchini,” alisema.
Dangote ambaye ni kati ya matajiri wakubwa duniani, amesimamisha uzalishaji wa simenti katika kiwanda chake cha Mtwara akidai kutoridhishwa na mazingira ya uwekezaji wake.
Serikali kwa upande wake imekuwa ikisema kuwa madai ya mwekezaji huyo hayana msingi wowote.
Hata hivyo, uongozi wa kiwanda hicho nao umejitahidi kueleza upande wake jambo ambalo limesababisha mvutano kati ya pande hizo mbili.