Na VERONICA ROMWALD-DAR ES SALAAM
TAKWIMU za Shirika la Kimataifa la Atomiki la Utafiti wa Saratani (IARC) na Shirika la Afya Duniani (WHO), zinaonyesha kuwa kila mwaka kuna wagonjwa wapya wa saratani wanaokadiriwa kufikia milioni 14.1 duniani kote.
IARC linaeleza kwamba kati ya hao zaidi ya wagonjwa milioni 8.2 hufariki dunia kwani huchelewa kufika au kufikishwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.
Kwa mujibu wa WHO ugonjwa wa saratani huathiri watu wa rika na jinsia zote na huchangia asilimia 13 ya vifo vyote vinavyotokea duniani.
Shirika hilo linaonya idadi ya wagonjwa itaongezeka hadi milioni 24 ifikapo mwaka 2035 hasa katika nchi zinazoendelea Tanzania ikiwamo, iwapo hatua madhubuti za kinga, uchunguzi wa mapema na tiba stahiki hazitachukuliwa haraka.
Saratani ya shingo ya kizazi
Ni saratani ambayo hutokana na mabadiliko ya ukuaji wa chembechembe au seli za mlango wa uzazi.
Mabadiliko hayo husababisha chembechembe hizo kushamiri na kukua kwa kasi kinyume na mpangilio wa maumbile.
Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa saratani hiyo huweza kusambaa na kushambulia kibovu cha mkojo, uke na sehemu ya chini ya utumbo mkubwa na baadaye figo, ini na sehemu zingine za mwili.
WHO inaeleza kwamba saratani ya shingo ya kizazi inazidi kuwa tishio duniani kwa kusababisha vifo vya wanawake wengi.
Chanzo chake
Waziri Ummy anasema saratani ya shingo ya kizazi husababishwa na kirusi cha HPV (Human Pappiloma Virus).
“Wataalamu wanasema wanaume ndiyo ambao hubeba kirusi hicho na huingia katika mwili wa mwanamke pale wanapojamiana,” anasema.
Anasema wanawake wanaoshiriki ngono mapema huwa katika hatari zaidi ya kupata saratani hiyo kuliko wale wanaoanza umri ukiwa umeenda.
“Wasichana wanaoanza ngono chini ya miaka 18 na wale wanaoshiriki na wenzi tofauti tofauti wapo hatarini zaidi kupata saratani hii. Ingawa zipo sababu nyinginezo kama vile uvutaji wa sigara,” anasema.
Kwa mujibu wa wataalamu wanawake wanaoishi na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) wapo katika hatari zaidi ya kupata saratani ya shingo ya kizazi kuliko wale wasiougua ugonjwa huo.
Wasichana wapo hatarini
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani wa Hospitali ya Agakhan, Harrison Chuwa, anasema hiyo ni kwa sababu kirusi hicho huchukua muda wa miaka 20 kuanza kuonesha athari zake.
“Kirusi cha HPV hukaa hadi miaka 20 kuanza kuonesha athari zake tangu kinapoingia katika mwili wa mwanamke, ndiyo maana tunasema wasichana wanaoanza ngono katika umri mdogo wapo katika hatari kubwa ya kupata saratani hii kuliko wale wenye umri mkubwa.
Anasema ukweli juu ya tafiti hizo unabainika wazi kwani idadi kubwa ya wanawake wanaosumbuliwa na tatizo hilo ni wale wenye umri wa miaka 45 na kuendelea.
“Tumebaini kuwa wanawake wanaougua saratani hii wanaofika kwetu wengi ni wale walioko kwenye umri wa miaka 45. Kwa kuzingatia tafiti
zilizowahi kufanyika tunakadiria kwamba huenda walianza kujamiiana wakiwa na umri wa miaka 25 kushuka chini,” anasema.
Anasema wasichana wanaoshiriki uhusiano huo na wanaume wengi huwa katika hatari zaidi kuliko wale wanaoshiriki na mmoja.
Kuna aina 70 za virusi
Daktari huyo anasema zipo aina 70 za virusi vya HPV ambavyo vinaweza kusababisha maambukizi kwenye njia za uzazi za wanaume na wanawake. Husababisha pia maambukizi katika sehemu za mdomoni pamoja na kwenye koo.
“Ingawa kuna aina 70 za virusi vya HPV hata hivyo aina ya 16 na 18 ndivyo ambavyo husababisha saratani zote za mlango wa kizazi kwa asilimia 70,” anasema.
Hali ilivyo nchini
Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), kila mwaka hupokea wagonjwa 22,000 kutoka sehemu mbalimbali nchini.
Kati ya wagonjwa hao idadi ya wagonjwa wa saratani ya shingo ya
kizazi inatajwa kuongoza idadi ya wagonjwa wanaopokelewa.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, anasema nusu ya wagonjwa hao wanaugua saratani ya shingo ya kizazi na saratani ya matiti.
“Wagonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi na matiti wanachukua asilimia 45.6 ya wagonjwa wote. Kati ya wagonjwa 100 wagonjwa 33 hukutwa na saratani ya shingo ya kizazi ambao ni sawa na asilimia 33,” anasema.
Anasema asilimia 13 ya wagonjwa hukutwa wakiwa tayari wanaugua saratani ya matiti.
Umaskini unatajwa kuchangia
Dk. Chuwa anasema mojawapo ya chanzo kinachotajwa kusababisha kuongezeka kwa tatizo la saratani ya shingo ya kizazi ni umaskini.
“Umaskini unachangia kwa kiasi fulani kwa sababu tunaona katika baadhi ya maeneo wasichana wamekuwa wakijiuza ili waweze kujikimu kimaisha ingawa si wote.
“Wengi wao wanafanya hivyo kwa sababu walikosa elimu, serikali imeliona suala hilo na kuja na sera ya elimu bure, itasaidia kwani watapata fursa ya kwenda shule na tunatarajia elimu watakayoipata itawakomboa kifkra na kiuchumi katika maisha yao ya baadae hivyo watafanya maamuzi sahihi kwa wakati sahihi,” anasema.
Dk. Chuwa anaongeza “Hata hivyo ni vema wasichana wakajitunza na kuacha kufanya matendo hayo wakiwa katika umri mdogo kujiepusha na uwezekano wa kupata saratani hii siku za usoni.”
Anasema matatizo ya saratani katika miaka ya hivi karibuni yamezidi kuongezeka huku idadi ya watu wanaosumbuliwa na maradhi hayo wanaokwenda hospitalini hapo nayo ikiongezeka.
Dalili
Daktari huyo anasema dalili za saratani ya mlango wa kizazi mara nyingi hujitokeza wakati ikiwa imeshasambaa.
“Dalili hizo ni pamoja na kutokwa damu sehemu za siri bila mpangilio au kutokwa damu baada ya kujamiana, maumivu ya mgongo, miguu na au
kiuno, kuchoka, kupungua uzito, kupungikiwa hamu ya kula, kutokwa uchafu kwenye uke wa majimaji, rangi kahawia au wenye damu,” anasema
Anasema iwapo mwanamke hatafika hospitalini kupata matibabu ya haraka, saratani hiyo huweza kusababisha madhara katika viungo vingine vya mwili.
“Huweza kusababisha pia kuishiwa damu, figo kushindwa kufanya kazi na hatimaye kufariki dunia,” anasema Dk. Chuwa.
Matibabu
Mkurugenzi wa ORCI, Dk. Julius Mwaiselage, anasema saratani ya mlango wa kizazi si rahisi kuitambua hadi pale wataalamu wa afya wanapofanya uchunguzi.
“Saratani hii ikigundulika mapema inatibika, huwa tunaondoa seli zote ambazo zitakuwa zimeathirika kwa kutumia kifaa maalumu, lakini ikiwa imesambaa huwa tunaondoa mfuko wote wa uzazi ili kuokoa maisha ya mama,” anasema Dk. Mwaiselage
Mkurugenzi huyo anasema mwanamke anayefanyiwa kipimo hicho anapaswa kukaa miezi sita pasipo kukutana na mwezi wake ili virusi vya ugonjwa huo vife.
Mikakati ya serikali
Waziri Ummy anasema serikali tayari imepokea mashine 15 za kutibu dalili za awali za saratani ya shingo ya kizazi toka kwa Shirika la IARC.
“Tunakusudia kuzisambaza mashine hizi katika hospitali za rufaa na mikoa, lengo letu ni kupunguza idadi ya vifo vitokanavyo na saratani hii, tunakusudia kufikia wanawake milioni mbili baada ya miaka miwili.
“Hivyo mashine hizi tutazipeleka katika mikoa 10 ambayo haina kabisa huduma ya matibabu ya saratani na naamini tutafikia lengo letu,” anasema.
Wasichana kuchanjwa
Waziri Ummy anasema ili kuwakinga wasichana dhidi ya ugonjwa huo serikali inakusudia kuanza kutoa chanjo kwa wale walio na umri wa kuanzia miaka tisa hadi 17 ifikapo mwakani.
“Hawa tunaamini bado hawajaanza kujihusisha na mahusiano ya kingono, hivyo tutawapa chanjo ili kuwakinga, tayari tumewapatia wasichana walioko katika Mkoa wa Kilimanjaro.
“Wapo ambao hudhani kwamba tunafanya hivyo kwa majaribio au kuna mbinu za kuua watoto wa kitanzania, naomba wazazi waachane na dhana hiyo kwani ni potofu, chanjo hii si kwa nia mbaya na kwa kuonesha mfano hata mwanangu nitamchanja,” anasema.
Waziri Ummy anawahimiza wanawake wajitokeze na kuwahi hospitalini kufanyiwa vipimo kwani saratani hiyo inatibika.
“Nawahimiza wawahi hospitalini, wapate matibabu mapema, huduma ni bure kabisa na taasisi yetu (ORCI) tumeiongezea bajeti ya dawa kutoka bilioni moja hadi saba, na tumeiagiza ijenge duka lake la dawa ili zipatikane kwa bei nafuu pale inapotokea zimeisha,” anasema.