Na Mwandishi Wetu-MWANZA
MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, ameunga mkono jitihada za kupambana na dawa za kulevya, kama hatua ya kuliokoa taifa na janga hilo ambalo limesababisha madhara makubwa katika jamii.
Kauli hiyo aliitoa jana wakati akizungumza na watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, ambako alisisitiza kuwa mapambano dhidi ya dawa za kulevya yatakuwa ni endelevu lengo likiwa kukomesha uuzaji, usambazaji na utumiaji wa dawa hizo kama hatua ya kuokoa kizazi cha sasa na kijacho.
“Kamwe Serikali ya Awamu ya Tano haitarudi nyuma katika vita dhidi ya dawa za kulenya,” alisema na kuwataka wananchi waendelee kutoa taarifa za siri kwa vyombo vya dola zitakazosaidia kuwabaini watu wanaojihusisha na biashara hiyo ili waweze kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.