THERESIA GASPER, DAR ES SALAAM
MSHAMBULIAJI wa timu ya Taifa anayekipiga katika Klabu ya TP Mazembe nchini Kongo, Mbwana Samatta, amewataka Watanzania wajitokeze kwa wingi Jumamosi katika mchezo kati ya Stars na Algeria, akieleza hawatawaangusha katika mchezo huo.
Mchezaji huyo ambaye majuzi aliitoa kimasomaso klabu yake ya TP Mazembe kwa kuisaidia kuchukua ubingwa wa Afrika baada ya kuitoa timu ya USM Algier ya Algeria kwa jumla ya mabao 4-1 huku akiwa amefunga mabao saba, ameeleza Watanzania wategemee matokeo mazuri katika mchezo huo na kuibuka na ushindi.
“Tunawashukuru Watanzania wote kwani tumekuwa tukiona sapoti yenu katika vyombo vya habari, tunawaahidi hatutawaangusha bali mtarajie mambo mazuri, mambo ya TP Mazembe yabaki huko huko kwa sasa ni zamu ya Taifa Stars,” alisema.
Naye Thomas Ulimwengu alisema wapo tayari kupambana na wana imani watafanya vizuri katika mchezo huo na hawatakuwa tayari kuona wanapoteza ushindi.
“Tunashukuru kwa sapoti ambayo mmekuwa mkitupa, hivyo ushindi wa TP Mazembe ubaki historia kilichobaki ni kuangalia timu yetu ya Taifa,” alisema.
Hata hivyo, Samatta ameeleza bado anayo ndoto ya kuzidi kuitangaza vema Tanzania hasa pale atakapocheza ligi kubwa barani Ulaya.
Alisema bado wanazingatia ushauri wa Rais mstaafu Dk. Jakaya Kikwete, hawafikirii kwamba TP Mazembe ndiyo mwisho wao bali wanafikiria kwenda mbali zaidi na kucheza soka Ulaya.
“Bado ndoto yetu ipo pale pale, hatutaweza kuishia Mazembe na kujiona tumemaliza lazima tufanye kitu ambacho vizazi vijavyo waje waone kweli tulipata watu ambao wamesogea, hivyo wakati utakapofika tutalifanyia kazi,” alisema.