ADAM MKWEPU NA MITANDAO
KILA mtu ana ndoto zake anazotamani zikamilike, miongoni mwa ndoto kubwa anazoziota mshambuliaji wa kimataifa Mtanzania, Mbwana Samatta, ni kukanyaga Uwanja wa Old Trafford pale nchini England.
Njia pekee ambayo Samatta anaona itamfanya kukanyaga uwanja huo kwa sasa ni kupitia michuano ya Europa League ambayo timu yake inashiriki sambamba na Manchester United inayonolewa na kocha Jose Mourinho.
Samatta anafahamu wazi fursa atakayopata wakati akicheza dhidi ya Manchester United kwa kuwa wasaka vipaji wa klabu kubwa watakuwa wakitolea macho mchezo huo ili kusaka vipaji vya wachezaji wachanga.
Kiu ya mafanikio na uthubutu vinamweka mbali Samatta na wachezaji wengine ambao waliwahi kucheza Ulaya bila ya mafanikio.
Hatua aliyofikia nyota huyo inawafanya wengine kujiuliza mara mbili walipokosea hasa wakimwona mchezaji huyo akiyoyoma anga za kimataifa katika michuano ya Ulaya akicheza dhidi ya timu kubwa.
Ubora wake umeonekana tangu awe mchezaji bora wa Afrika mwaka 2015 kwa wachezaji wa ndani akicheza timu ya TP Mazembe ya Kidemokrasia ya Kongo na sasa Genk ya Ubelgiji ambako tayari yupo nafasi ya nane akiwa na mabao 10 katika orodha ya wachezaji waliotupia nyavuni msimu huu nchini humo.
Samatta ndiye aliyesababisha Watanzania wengi wafuatilie Ligi Kuu ya Ubelgiji ili kufahamu maendeleo yake ikiwa ni pamoja na kupata nafasi ya kumtofautisha na wengine katika kupambana kuliwakilisha taifa vema.
Wapo waliompa uraia wa Kenya wakidhani Samatta si Mtanzania sababu kubwa ni utofauti wa nyota huyo na wengine walioenda Ulaya na kuishia kupiga ‘selfie’ huku wakituaminisha kwamba hali ya hewa pamoja na mazingira ndiyo sababu ya wao kushindwa kuonesha ubora wao.
Ukimwona Samatta utagundua kwamba si mchezaji wa aina yao kwa kuwa amegubikwa na tamaa ya kuyafikia mafanikio ya nyota wakubwa duniani katika soka.
“Ukiachana na mambo ya fursa na kwamba labda ndiyo itakuwa njia, kabla hata hatujacheza na Gent, nilikuwa naomba ratiba itokee tukutane na Manchester United kwa sababu ndoto yangu ya kukanyaga Old Trafford itakuwa imekamilika.
“Nina ndoto ya kukanyaga Old Trafford ukiachana na mambo mengine yote kwamba huenda ikawa ndiyo fursa au njia kwangu, hayo mambo yatakuja baadaye kwenye game lakini nitakuwa najua naenda kuikanyaga Old Trafford kitu ambacho nimekuwa nakiota,” anasema Samatta.
Genk iliingia hatua ya robo fainali baada ya kupata sare ya bao 1-1 na KAA Gent katika mchezo uliochezwa Alhamisi ya wiki iliyopita katika Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk.
Matokeo hayo yaliipeleka Genk hatua hiyo kwa ushindi wa jumla ya mabao 6-3 baada ya awali kushinda mabao 5-2 ugenini wiki iliyopita kwenye mchezo wa kwanza wa hatua ya 16 bora wakiungana na United ya England inayonolewa na kocha Mreno, Jose Mourinho.
Hata hivyo, Samatta atalazimika kusubiri hadi hatua inayofuata ili kukanyaga ardhi ya Uwanja wa Old Trafford baada ya Ijumaa iliyopita timu yake kupangwa na Celta Vigo ya Hispania katika ya hatua ya robo fainali ya Europa League.
United wao wamepangwa kucheza na Anderlecht ya Ubelgiji, wakati Lyon ya Ufaransa itamenyana na Besiktas ya Uturuki na Ajax ya Uholanzi itavaana na Schalke ya Ujerumani.
Wakati huo huo mabingwa watetezi wa England, Leicester City wamepangwa kucheza dhidi ya Atletico Madrid ya Hispania katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Leicester City watasafiri kwenda Hispania kucheza na kikosi cha Diego Simeone kwenye mchezo wa kwanza Aprili 11 au 12, kabla ya kurudiana wiki moja baadaye England.
Wakati huo mabingwa watetezi, Real Madrid ya Hispania watamenyana na Bayern Munich ya Ujerumani katika mchezo unaotarajiwa kuwa mkali zaidi kwenye hatua hiyo, kikosi cha Zinedine Zidane kikiwania kuwa timu ya kwanza kutetea taji hilo kwa mafanikio.
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Hispania (La Liga), Barcelona wao watacheza na Juventus ya Italia baada ya kufuzu kimiujiza katika mchezo wa robo fainali wakiwatoa Paris Saint-Germain (PSG) wakati Borussia Dortmund ya Ujerumani pia itamenyana na Monaco ya Ufaransa.