27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Samatta amtetea Messi

samatta4NA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM
MCHEZAJI wa Kimataifa anayechezea klabu ya TP Mazembe ya nchini Congo, Mbwana Samatta, amemkingia kifua mchezaji mwenzake wa klabu ya Simba, Ramadhani Singano ‘Messi’ kuwa hana ujanja wa kughushi mkataba.
Mkataba wa miaka miwili wa mchezaji huyo unadaiwa umechezewa kwa kuongezewa mwaka mmoja zaidi unaoisha Julai, mwakani, tofauti na ule alionao yeye unaomalizika mwezi ujao.
Akizungumza na MTANZANIA jana akiwa kwenye kambi ya timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, Samatta alisema haamini katika hilo na hafikirii kama Messi anaweza kuwa na ujanja wa kufanya hivyo, hilo jambo litakuwa limefanyika ndani ya klabu hiyo.
“Messi hawezi kuwa na ujanja wa kubadilisha mkataba na siamini katika hilo, siku zote nikiwa kama mchezaji nitasimamia upande wa wachezaji wenzangu na kwa hilo sikubaliani nalo,” alisema.
Alisema klabu nyingi zimekuwa na ujanja wa kuwabadilishia wachezaji mikataba, hivyo kuwadhulumu haki yao na hasa mchezaji anapokuwa anajiandaa kwa makubaliano mapya.
Kwa upande wa Messi, alisema hakuna sehemu yoyote aliyowahi kutamka suala la mkataba wake kughushiwa.
“Mimi nashindwa kuelewa haya mambo, mimi sijawahi kutamka kama mkataba wangu kughushiwa, mimi nilitaka maelezo kutoka kwa Simba mkataba huu wa miaka mitatu ni upi,” alisema Messi.
Kauli hiyo ya Messi iliungwa mkono na Mwenyekiti wa Chama cha Wachezaji Tanzania (Sputanza), Mussa Kisoky, aliyesema Messi hajawahi kutamka kughushiwa mkataba wake na Simba, bali anachohitaji ni maelezo ya kina yenye kueleweka.
Kisoky alisema Messi alijaribu kuomba ufafanuzi kutoka kwa viongozi wa Simba, suala ambalo walishindwa kulifanyia kazi, ndipo alipochukua maamuzi ya kufika Sputanza.
“Hakuna mahali ambako Messi ametamka kugushiwa mkataba wake, bali tunachokihitaji ni maelezo ya kina ya kueleweka,” alisema Kisoky.
Mwenyekiti huyo alieleza wamesikia tetesi za Simba kutaka kulifikisha suala hilo polisi, ila upande wao wanawaonya wekundu hao wa Msimbazi kutojaribu kuupotosha umma.
“Tumesikia hizo tetesi, lakini kitu cha kujiuliza wanakwenda polisi kufanya nini, wasipende kudanganya, watambue wanachotakiwa kukifanya ni kueleza ukweli.
“Suala hili tumeshalifikisha Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Simba kutaka kwenda polisi ni maamuzi yao ila watambue tunataka ukweli,” alisema.
Kisoky alisema wanachotambua tayari TFF wamepokea barua yao ya kuomba kupatiwa ufafanuzi juu ya mvutano huo.
MTANZANIA lilifanya jitihada za kumpata msemaji wa klabu ya Simba, Haji Manara, ili kutolea ufafanuzi maamuzi ya klabu kulifikisha suala hilo polisi, hata hivyo simu yake ya mkononi haikuwa hewani.
Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa TFF, Celestine Mwesigwa, alisema tayari barua hiyo imewafikia na wameanza kuifanyia kazi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles