BIRMINGHAM, ENGLAND
MSHAMBULIAJI wa timu ya Aston Villa, Mbwana Samatta, amedai furaha yake ni kukamilisha ndoto ya kufanya kazi na nyota walioitikisa dunia.
Nahodha huyo wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ ambaye alijiunga na klabu hiyo ya Ligi Kuu England akitokea Genk wakati wa uhamisho wa Februari mwaka huu, amekuwa Mtanzania wa kwanza kucheza ligi hiyo.
Tangu amejiunga na Aston Villa hadi sasa amecheza jumla ya michezo 14 na kufanikiwa kupachika bao moja kwenye Ligi Kuu.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, mchezaji huyo aliposti picha akiwa na aliyekuwa mkongwe wa klabu ya Chelsea, John Terry ambaye kwenye kikosi cha Aston Villa ni kocha msaidizi, hivyo Samatta alisema, awali alikuwa anamuangalia nyota huyo akicheza mpira bila ya kujua kama ipo siku angeweza kufanya naye kazi.
“Mwanzo ilikuwa kama ndoto, kwenda mara kwa mara kwa mzee Achi (Kibanda Umiza), maarufu Mbagala Rangi 3 kuangalia wakicheza. Leo niseme ni bahati au juhudi kuweza kuwa nao karibu, inaweza kuwa kimoja wapo au vyote, ila nina furaha na nilipotoka hadi nilipo sasa. Aina maana kuwa nimemaliza, ila nichukue nafasi hii kuwaambia vijana wanaochipukia kuwa wanaweza kuyakamilisha yale yote ambayo wanayaoya, haina kufeli,” aliandika mchezaji huyo.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27, hadi sasa amecheza jumla ya michezo 56 akiwa na Taifa Stars, huku akifunga mabao 20.
Katika mahojiano yeka ya kwanza mara baada ya kujiunga na klabu ya Aston Villa, mchezaji huyo aliweka wazi kwamba, alikuwa anavutiwa sana na nyota wa zamani wa Chelsea, Didier Drogba pamoja na mshambuliaji wa Juventus, Cristiano Ronaldo.
“Nimekuwa nikiwaangalia wachezaji wengi na kuna wakati nimekuwa nikitaka kuwa kama wao, lakini ukweli ni kwamba Didier Drogba amekuwa kivutio kwangu hasa baada ya kuisaidia Chelsea kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya,” alisema mchezaji huyo.