24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, October 31, 2024

Contact us: [email protected]

SALMA KIKWETE AZUA JAMBO BUNGENI

Na MAREGESI PAUL-DODOMA


SUALA la wanafunzi kuendelea na masomo baada ya kupata mimba wakiwa shuleni, limewagawa wabunge.

Tukio hilo lilitokea jana wakati wabunge hao walipokuwa wakichangia hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka wa fedha 2017/18 iliyowasilishwa mwishoni mwa wiki na Waziri wake Profesa Joyce Ndalichako.

Wakati wa mjadala huo, wabunge walikuwa wakiomba miongozo mara kwa mara na kumfanya Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu kuwa katika wakati mgumu kutokana na wingi wa miongozo.

Aliyekuwa wa kwanza kuchangia bajeti hiyo ni Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, Mama Salma Kikwete, ambaye alisema haungi mkono wanafunzi kuendelea na masomo baada ya kujifungua.

Katika maelezo yake, Mama Salma alisema kama wanafunzi wataruhusiwa kuendelea na masomo baada ya kujifungua, kitakuwa ni kichocheo kwao kuendelea kufanya mapenzi katika umri mdogo.

“Kwanza kabisa, naomba walimu wanaojiendeleza, wasiombe kazi tena pindi wanapotaka kuhamia sehemu zingine bali wabakizwe katika vituo vyao vya kazi na kuboreshewe masilahi yao.

“Kuhusu suala la watoto kuendelea na masomo baada ya kujifungua, sikubaliani na hoja hiyo kwa sababu mila, desturi na dini zetu, zinazuia watoto kufanya mapenzi.

“Badala yake, itafutwe njia mbadala ya kukabiliana na tatizo hilo kama hapa bungeni tulivyo na taratibu na kanuni zinazotuongoza.

“Kwa hiyo, nawaomba wabunge wenzangu, tuungane katika hili na kama hoja ni kuwatetea watoto wetu, utafutwe utaratibu mwingine wa kuwasaidia,”alisema Mama Salma.

Mama Salma ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA), kwa muda mrefu amekuwa akipigia debe haki za mtoto wake na kuongozwa na kauli mbiu ya ‘Mtoto wa mwenzio ni wako’.

Hata hivyo, Mbunge wa Viti Maalumu, Susan Lyimo (Chadema), alipokuwa akichangia bajeti hiyo, alisema anamshangaa mama Salma kwa mtazamo wake huo ingawa naye ni mwanamke.

“Nimesikitishwa sana na mheshimiwa Salma Kikwete ambaye ni mwanamke mwezetu. Lakini simshangai kwa sababu hata mumewe alipokuwa rais, aliwahi kusema watoto wanaopata mimba ni kutokana na viherehere vyao,” alisema Lyimo.

Kwa upande wake, Mbunge wa Makete, Profesa Norman Sigalla (CCM), alisema haungi mkono wanafunzi kuendelea na masomo kwa sababu kuna njia nyingine za kuwasaidia baada ya kuachishwa masomo.

“Mtoto wangu akipata mimba siyo kwamba haruhusiwi kuendelea na masomo bali ninachotakiwa kufanya ni kumpeleka katika shule nyingine baada ya kujifungua.

“Yaani, ukimwambia mtoto, kwamba mwanangu ukipata mimba utaendelea na shule, basi tujue mimba zitakuwa nyingi sana mashuleni,” alionya Profesa Sigalla.

Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalum, Tauhida Gallos Nyimbo (CCM), alianza kwa kuwashangaa wabunge wanaopinga wanafunzi wasiendelee na masomo baada ya kujifungua.

Kwa mujibu wa mbunge huyo, watoto wanaofanikiwa kuendelea na masomo baada ya kujifungua ni walioko katika familia zenye uwezo kifedha na wanaotoka katika familia masikini, watalazimika kubaki nyumbani kwa kuwa wazazi wao hawana fedha.

“Atakayempa mimba mwanafunzi awekwe ndani na mwanafunzi wa kike apewe elimu ya kuepuka mimba na pia ziwepo taratibu kali za kuwalinda watoto  wa kike.

“Hiyo hoja ya kwamba watoto wanaweza kuendelea na masomo baada ya kujifungua, hilo linawezekana kwa watoto wanaotoka katika familia zenye uwezo kifedha na wasiokuwa na uwezo, watoto wao watabaki nyumbani.

“Yaani mtoto wa mwenye fedha akipata mimba, mimba itatolewa na anaendelea na masomo, kwa hiyo watoto waruhusiwe kusoma baada ya kujifungua,”alisema Gallos.

Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalum , Lucia Mlowe (Chadema), alisema kutowaruhusu watoto wa kike wasiendele na masomo kwa sababu ya mimba ni kutowatendea haki kwa sababu baadhi yao hubeba mimba baada ya kudanganywa.

Naye Mbunge wa Mbinga Mjini, Sixtus Mapunda (CCM), alisema ili watoto waruhusiwe kuendelea na masomo baada ya kujifungua, kuna haja ya kubadili Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 kwa sababu inazuia watoto kufanya mapenzi wakiwa na umri mdogo.

Pamoja na hayo, alitaka hadhari zaidi ichukuliwe kabla ya kufikia uamuzi wowote huku mila, desturi na imani za kidini zikizingatiwa kwa kuwa baadhi ya dini zinazuia mapenzi katika umri mdogo.

Kwa upande wake, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Kessy (CCM), aliwataka wabunge wanawake wanaotaka watoto waruhusiwe kusoma baada ya kujifungua, watoe ushuhuda wao kama walianza mapenzi wakiwa watoto.

Kwa mujibu wa mbunge huyo, dini ya kiislam inapinga mimba katika umri mdogo, hivyo akataka Serikali isikubaliane na wazo hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles