25.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, January 19, 2022

VITABU FEKI VYAWAPONZA VIGOGO ELIMU

MAREGESI PAUL Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA


WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, amewasimamisha kazi Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu Tanzania, Dk. Paul Mushi  na Kaimu Kamishna wa Elimu, Nicolaus Buretta ili kupisha  uchunguzi wa uwepo wa vitabu vyenye makosa katika shule za msingi na sekondari nchini.

Pamoja na hayo, amesema waliohusika kuhariri na kuandika maudhui ya vitabu hivyo, nao watachukuliwa hatua baada ya uchunguzi kufanyika.

Profesa Ndalichako alichukua hatua hiyo bungeni jana usiku  wakati wabunge walipokuwa wakijadili hoja ya uwepo wa vitabu hivyo mashuleni wakati wa kuhitimisha hotuba ya bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka wa fedha 2017/18.

Pamoja na mambo mengine, hoja hiyo ilijadiliwa baada ya Mbunge wa Viti Maalum, Esther Mmasi (CCM), kutoa shilingi katika bajeti hiyo na kuwaomba wabunge wamuunge mkono katika hoja yake hiyo kabla Bunge halijapitisha bajeti hiyo.

Katika maelezo yake, Mmasi alisema kitendo cha kiongozi kupitisha vitabu vibovu mashuleni ni sawa na uhaini kwa kuwa vitabu hivyo vinaharibu mfumo wa elimu nchini.

“Shilingi bilioni 108 zilizotumika kutunga vitabu hivyo ni nyingi na matumizi mabaya ya fedha hizo ni sawa na uhaini.

“Pia, kwa mujibu wa sheria zetu, ufisadi unaozidi shilingi bilioni 100, mhusika anapelekwa katika mahakama ya ufisadi. Sasa kwanini wahusika katika suala hili hawajapelekwa katika mahakama ya mafisadi?

“Kwa hiyo, naomba waheshimiwa wabunge, mniunge mkono katika hoja yangu hii tujadili jambo hili,”alisema Mmasi.

Baada ya kauli hiyo, Profesa Ndalichako alisimama na kulieleza Bunge, hatua alizochukua katika kushughulikia suala hilo ikiwa ni pamoja na kuunda timu ya wataalam kuchunguza jambo hilo.

Pamoja na hayo, alisema hataweza kuwavumilia wahusika na kwamba kila mmoja atabeba msalaba wake kwa kuwa waliopitisha vitabu hivyo ni wasomi walioajiriwa na kulipwa mshahara na Serikali.

Hata hivyo, kauli hiyo haikumfanya Mmasi abadili msimamo wake na hivyo kuwataka wabunge waendelee kumwunga mkono ili wajadili jambo hilo kwa kuwa waziri alikuwa hajatoa maelezo ya kutosha.

“Mwaka jana tulikuomba uchukue hatua juu ya jambo hili lakini hukuchukua hatua na sasa unataka tukuunge mkono.

“Hilo haliwezekani, nawaomba wameshimiwa wabunge mniunge mkono tujadili jambo hili,”alisisitiza Mmasi.

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wabunge waliosimama na kujadili hoja hiyo ni Mbunge wa Songwe, Philipo Mulugo (CCM), ambaye alisema alikopa Sh milioni 22  katika Benki ya CRDB kununulia vitabu hivyo ambavyo sasa vimekataliwa.

Naye Mbunge wa Bukombe, Dotto Biteko (CCM), alisema lazima waziri alieleze Bunge hatua thabiti atakazochukua katika suala hilo ili kuinusuru sekta ya elimu nchini.

Naye Susan Lyimo (Chadema), alisema lazima Waziri awajibike katika suala hilo kwa kuwa vitabu hivyo vimeingia sokoni tangu mwaka jana.

Kwa upande wake, Mbunge wa Vunjo, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), alisema kuna haja suala hilo kupelekwa katika Kamati ya Bunge ya Maendeleo na Huduma za Jamii ili ikalifanyie kazi.

Wengine waliochangia hoja hiyo baada ya kutoridhishwa na kauli ya Profesa Ndalichako ni Mbunge wa Mbozi, Paschal Haonga (Chadema), Mbunge wa Mchinga, Hamidu Bobali (CUF), Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba (CCM), Mbunge wa Busega, Dk. Raphael Chegeni (CCM), Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema) na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko (Chadema).

Wengine ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, Naibu Waziri wa Tamisemi, Seleman Jafo na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage.

Akichangia bajeti hiyo jana, Mbunge wa Bukombe, Dotto Biteko (CCM), aliishangaa Serikali kuruhusu vitabu vilivyojaa makosa vipelekwe shuleni wakati wakijua vinaharibu elimu nchini.

“Kwanza kabisa, naomba idara ya ukaguzi wa shule, itolewe katika Wizara ya Elimu na badala yake iundwe wakala maalum itakayokuwa na wajibu wa kukagua shule.

“Kuhusu vitabu vibovu, nashangaa sana kwa Serikali kuruhusu vitabu hivyo vilivyojaa makosa viingizwe sokoni wakati wakijua vinaharibu watoto wetu.

“Yaani vitabu vina makosa mengi na havifai kabisa kwenda sokoni. Kwa mfano kuna kitabu hapa cha Form Four kina makosa 34 ya kimaudhui na

kimantiki na kingine ni cha Form Three kina makosa 12 ya kimaudhui na kimantiki pia.

“Haiwezekani Rais atenge fedha kwa ajili ya kununulia vitabu, halafu mnatulisha matango pori. Hamchukui hatua kwa sababu huenda inawezekana aliyevichapsha ni mtu wa Serikali ndiyo maana mnashikwa kigugumizi kumchukulia hatua.

“Vitabu hivyo tumeambiwa vimetumia Sh bilioni 108, ambazo tumezipiga kiberiti bila sababu za msingi. Yaani walimu wetu walipoona vitabu mlivyowapelekea vina makosa, waliviacha na kuanza kufundisha kwa uzoefu wao,” alisema Biteko.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
175,234FollowersFollow
531,000SubscribersSubscribe

Latest Articles