Na ALLY BADI
-LINDI
MKE wa Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Salma Kikwete, amemshukuru Rais Dk. John Magufuli kwa kumwona na kumteua kuwa mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Salma ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM akitokea Wilaya ya Lindi Mjini, alitoa shukrani hizo wakati alipopewa nafasi ya kutoa salamu kwa wakazi wa Kata ya Ngapa waliohudhuria ziara ya Rais Magufuli ya kukagua mradi wa maji wa eneo hilo.
Salma ambaye yupo mkoani Lindi, alijitokeza jana katika ziara ya Rais Dk. Magufuli mkoani humo ambapo mbali na kutoa shukrani hizo alisema tatizo la maji katika Manispaa ya Lindi limekuwa kero ambayo inanyima utulivu kwa watendaji na viongozi wa wilaya na mkoa huo kwa ujumla.
Katika hilo alisema kwa nafasi aliyopewa atahakikisha anawawakilisha vyema wananchi wa Lindi na atashirikiana na wabunge wa mkoa huo kutatua kero ya maji.
Uteuzi huo wa Salma umekuja ukiwa umepita zaidi ya mwaka mmoja tangu jina lake litajwe na kuhusishwa katika kinyang’anyiro cha ubunge wa Jimbo la Lindi Mjini.
Tetesi za Salma kuhusishwa na kinyang’anyiro hicho zilififia baada ya yeye mwenyewe kushindwa kujitokeza katika kinyang’anyiro hicho wakati wa Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwaka 2015.
Kwa upande wake Rais Magufuli katika ziara hiyo ambayo alikuwa ameambatana na Mama Salma lakini pia viongozi kadhaa wa kiserikali, kisiasa na mkoa akihutubia baadaye katika Uwanja wa Ilulu alimsifia akisema:
“Nimewaongezea Salma ni mchapakazi, anakipenda chama naamini kupitia yeye nitajua changamoto, hata mzuri ni mzuri jamani au naongopa? Naongea hayo Kikwete hayupo angerusha ngumi lakini naamini hatasikia,” alitania Rais Magufuli huku akiangua kicheko na kupokewa na shangilio kutoka kwa watu waliokusanyika kumsikiliza na wengine walisikika wakipiga vigelegele.
Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Lindi, Hamida Abdalah, alimpongeza Rais Magufuli kwa kumteua Salma kuwa mbunge na kuongeza kuwa kitendo hicho cha kuwaongezea wawakilishi wananchi kitaleta ufanisi na maendeleo kwa mkoa huo.
Amina Chapunga mkazi wa Ngapa, alisema kuteuliwa kwa Mama Kikwete kuwa mbunge kumeonyesha jinsi alivyokuwa karibu na jamii na kuwatumikia wananchi wakati alipokuwa mke wa rais.
Fatuma Khatibu alisema kitendo hicho kimeleta gumzo na mshangao mkubwa kwa wakazi wa Lindi.
“Unajua tunachoshangaa mke wa rais tena kuwa mbunge kwani ubunge na mke wa rais mkubwa nani? Hivi tumeshindwa kufaidika akiwa mke wa rais tutafaidika akiwa mbunge?” Alishangaa Fatuma Khatibu.
Kumekuwa na mitazamo mbalimbali baada ya Jumatano wiki hii Rais Magufuli kumteua Salma kuwa mbunge.
Wakati wengine wakisifia na kutaka watu wasiunganishe uteuzi huo na Rais Mstaafu Kikwete, wapo ambao wamekuwa na mtazamo tofauti wakihusisha na uamuzi huo na mfumo wa utawala wa kulindana na kuendelezana.