27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 8, 2023

Contact us: [email protected]

POLISI WAPEKUA TENA NYUMBANI KWA GWAJIMA

Na AZIZA MASOUD, DAR ES SALAAM

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limekanusha taarifa zilizozagaa katika mitandao ya kijamii kwamba wamemkamata Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima, kuwa si za kweli, bali walichokifanya ni kwenda nyumbani kwake Salasala kufanya upekuzi mwingine.

Jana Gwajima alifika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam kwa ajili ya kutekeleza taratibu za kawaida za kuripoti tangu atajwe hivi karibuni na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, katika orodha ya watu wanaodaiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya, lakini baada ya muda taarifa zilisambaa katika mitandao ya kijamii zikionyesha kuwa kiongozi huyo anashikiliwa na polisi.

Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro, alisema Gwajima hajakamatwa, isipokuwa polisi walikwenda kufanya upekuzi nyumbani kwake.

“Mnasema kakamatwa kwani tatizo nini hadi akamatwe, mtu akija kuripoti polisi ndiyo anakuwa amekamatwa,” alisema Sirro.

Alipoulizwa taarifa za kiongozi huyo kupekuliwa nyumbani kwake, alisema: “Hata kupekuliwa kwa mtu anayeripoti polisi si tatizo kwa sababu tunakuwa tumekwenda kumpeleleza, ni kweli tumempekua nyumbani kwake lakini hajakamatwa na tayari ameshaondoka,” alisema Sirro.

Awali, akizungumza na gazeti hili, Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa Kanisa hilo, Mchungaji David Mgongolwa, alisema hana taarifa za kukamatwa kwa kiongozi huyo, isipokuwa anachojua alifika polisi kwa ajili ya kuripoti.

“Huwa anakwenda kuripoti polisi mara kwa mara na mara ya mwisho alikwenda Jumatatu akaambiwa arudi tena Ijumaa (jana), taarifa za kukamatwa mimi sina,” alisema Mgongolwa.

Alipoulizwa kama amerudi au hajarudi, alisema bado hajatoka polisi, lakini hiyo ni hali ya kawaida kwa sababu zipo siku ambazo anakwenda kuripoti na kurudi usiku.

Taarifa zilizopatikana ndani ya polisi zinadai kuwa, upekuzi huo umetokana na sauti ya mahubiri ya Gwajima yanayomtaja kijana aliyetambulika kwa jina la Daudi Bashite.

Kwa mujibu wa sauti hiyo, kijana huyo anayedaiwa kusoma Shule ya Msingi Kolomije na kufeli mtihani, pia alisoma Shule ya Sekondari Pamba, jijini Mwanza na kupata daraja la sifuri katika mtihani wake wa kumaliza elimu ya kidato cha nne.

Pia Gwajima alisema vyeti vya matokeo ya kijana huyo anatajwa kuwa ndiye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na alinunua cheti cha kidato cha nne ambacho kina jina analotumia sasa, huku lengo likitajwa kuwa ni kuendelea na masomo ya elimu ya juu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,871FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles