33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

SALMA KIKWETE AFUNGUKA UBUNGE WAKE

Na ALLY BADI

-LINDI

MKE wa Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Salma Kikwete,  amemshukuru  Rais  Dk. John  Magufuli  kwa kumwona na kumteua kuwa  mbunge  wa Bunge  la Jamhuri ya  Muungano wa Tanzania.

Salma ambaye pia ni Mjumbe  wa Halmashauri Kuu ya CCM akitokea Wilaya ya Lindi Mjini, alitoa shukrani  hizo wakati alipopewa nafasi ya kutoa  salamu kwa wakazi wa Kata ya Ngapa  waliohudhuria  ziara ya Rais Magufuli ya  kukagua mradi wa maji wa eneo hilo.

Salma ambaye yupo mkoani Lindi, alijitokeza jana katika ziara ya Rais Dk. Magufuli mkoani humo ambapo mbali na kutoa shukrani hizo alisema tatizo la  maji katika Manispaa ya Lindi limekuwa  kero ambayo inanyima utulivu  kwa  watendaji  na viongozi wa wilaya na mkoa huo kwa ujumla.

Katika hilo alisema kwa nafasi aliyopewa atahakikisha anawawakilisha vyema wananchi wa Lindi na atashirikiana na wabunge wa mkoa huo kutatua kero ya maji.

Uteuzi huo wa Salma umekuja ukiwa umepita zaidi ya mwaka mmoja tangu jina lake litajwe na kuhusishwa katika kinyang’anyiro cha ubunge wa Jimbo la Lindi Mjini.

Tetesi za Salma kuhusishwa na kinyang’anyiro hicho zilififia baada ya yeye mwenyewe kushindwa kujitokeza katika kinyang’anyiro hicho wakati wa Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwaka 2015.

Kwa upande wake Rais Magufuli katika ziara hiyo ambayo alikuwa ameambatana na Mama Salma lakini pia viongozi kadhaa wa kiserikali, kisiasa na mkoa akihutubia baadaye katika Uwanja wa Ilulu alimsifia akisema:

“Nimewaongezea Salma ni mchapakazi, anakipenda chama naamini kupitia yeye nitajua changamoto, hata mzuri ni mzuri jamani au naongopa? Naongea hayo Kikwete hayupo angerusha ngumi lakini naamini hatasikia,” alitania Rais Magufuli huku akiangua kicheko na kupokewa na shangilio kutoka kwa watu waliokusanyika kumsikiliza na wengine walisikika wakipiga vigelegele.

Kwa upande  wake Mbunge  wa Viti  Maalumu Mkoa  wa Lindi,  Hamida Abdalah, alimpongeza Rais Magufuli  kwa kumteua  Salma  kuwa  mbunge  na  kuongeza  kuwa  kitendo  hicho  cha kuwaongezea wawakilishi wananchi kitaleta ufanisi  na maendeleo  kwa  mkoa huo.

Amina Chapunga mkazi  wa Ngapa, alisema kuteuliwa  kwa  Mama Kikwete  kuwa  mbunge   kumeonyesha jinsi alivyokuwa  karibu na jamii na  kuwatumikia  wananchi wakati alipokuwa mke wa rais.

Fatuma Khatibu alisema kitendo hicho kimeleta gumzo na mshangao  mkubwa kwa wakazi wa Lindi.

“Unajua tunachoshangaa mke wa rais tena kuwa mbunge kwani ubunge na mke wa rais mkubwa nani? Hivi  tumeshindwa kufaidika akiwa mke wa  rais tutafaidika akiwa mbunge?” Alishangaa Fatuma Khatibu.

Kumekuwa na mitazamo mbalimbali baada ya Jumatano wiki hii Rais Magufuli kumteua Salma kuwa mbunge.

Wakati wengine wakisifia na kutaka watu wasiunganishe uteuzi huo na Rais Mstaafu Kikwete, wapo ambao wamekuwa na mtazamo tofauti wakihusisha na uamuzi huo na mfumo wa utawala wa kulindana na kuendelezana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles