LONDON, ENGLAND
MSHAMBULIAJI wa Liverpool, Mohamed Salah, amesema licha ya Manchester City kushikilia hatima ya mbio za Ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu, wanaweza kuipiku ikiwa watashinda michezo minne ya mwisho.
Salah alitoa kauli hiyo juzi baada ya Liverpool kuifunga Chelsea mabao 2-0 katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Anfield, England.
Manchester City ambayo inatetea taji hilo msimu huu, juzi iliibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Crystal Palace lakini Sadio Mane na Salah walifanikiwa kuisaidia Liverpool kupata pointi tatu dhidi ya Chelsea.
Liverpool kwa sasa wanaongoza msimamo wa ligi hiyo kwa tofauti ya pointi mbili dhidi ya Manchester City ambayo ina mchezo mmoja mkononi dhidi ya Machester United utakaochezwa Aprili 24, mwaka huu.
Vijana wa Jurgen Klopp wanapewa nafasi ya kunyakua taji hilo msimu huu kama itafanikiwa kuifunga Cardiff City na Newcastle United ugenini na michezo miwili ya Huddersfield Town na Wolves itakayochezwa Uwanja wa Anfield.
Salah anahisi wanatakiwa kupata ushindi katika michezo hiyo ili kutwaa taji hilo kwa mara ya kwanza akiwa katika timu hiyo.
“Maoni yangu ni hayo kwamba tukipata ushindi katika michezo minne iliyobakia, tunatwaa ubingwa msimu huu,” alisema Salah wakati akihojiwa na runinga ya Sky Sports.
“Tunatakiwa kujikita katika michezo yetu. Tuna matumaini Manchester City itapoteza pointi.
“Nitakuwa nikiifuatilia Manchester City katika michezo yao. Hii inaweza kutusaidia kufanya vizuri kwenye michezo yetu, alisema.
Mshambuliaji huyo kwa sasa yupo kwenye mbio za kugombea tuzo ya mfungaji bora wa Ligi Kuu England, baada ya kufikisha mabao 19 sawa na mshambuliaji wa Manchester City, Sergio Aguero.