28.4 C
Dar es Salaam
Thursday, February 22, 2024

Contact us: [email protected]

Sakata la wanawake Rombo laibukia bungeni

selasiniNa Debora Sanja, Dodoma
SIKU chache baada ya kuripotiwa kwa taarifa za wanawake wa Wilaya ya Rombo kulazimika kukodi wanaume kutoka nchini Kenya baada ya waume wao kuzidiwa kwa ulevi, hatimaye sakata hilo limechukua sura mpya kwa kuibukia bungeni.
Akihoji hatua hiyo jana, Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema), alimtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, awaombe radhi wananchi wa Wilaya ya Rombo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Lembles Kipuyo.
Selasini alidai Kipuyo ndiye aliyesema kwamba baadhi ya wanawake wa Rombo na maeneo ya mipakani wamekuwa wakikodi wanaume kutoka nchi ya Kenya ili kufanya nao mapenzi baada ya wanaume wao kutowatendea haki kutokana na kuzidiwa na ulevi.
Selasini alisema taarifa hiyo imezua tafrani wilayani humo na kwamba, huo ni udhalilishaji na ni kinyume cha haki za binadamu.
“Waziri Mkuu unaweza kusema chochote juu ya udhalilishaji huu ikiwemo kuwaomba radhi wananchi wa Rombo ambao wameathirika kutokana na tafrani hii?” alihoji.
Waziri Mkuu alisema halifahamu jambo hilo na kutaka kupewa muda ili alifanyie uchunguzi.
“Lakini kama ni kuomba radhi anatakiwa kuomba mhusika aliyesema jambo hilo katika eneo husika na mimi nitawaamimbia Tamisemi walifanyie kazi kuona jinsi ya kuchukua hatua kwa mtendaji wetu,” alisema.
Katika swali lake la msingi, Selasini aliitaka Serikali kuweka viwango vya utengenezaji wa pombe ya gongo kwa kuwa wananchi wa Rombo wamekuwa wakipika kwa ajili ya kujipatia kipato.
Alisema kwa sasa wananchi wanaotengeneza gongo hiyo wanapigwa na askari na kunyang’anywa vyombo vyao.
Pinda, alisema Serikali haiko tayari kuruhusu pombe aina ya gongo kuwa halali kutengenezwa, kuuzwa au kunywewa na watu wake.
Pia alisema viwango vya pombe hiyo havipimiki na kwamba hata kama watauziwa wasinywe.
Alisema kuna pombe aina ya konyagi ambayo ni kama mbadala wa gongo.
“Mimi si mtaalamu wa masuala hayo labda nitawauliza wahusika ili tuwape nafasi wenzetu wa viwanda na biashara waziangalie pombe hizo, au kama zinaweza kutumika kama bidhaa za konyagi,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles