26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 17, 2024

Contact us: [email protected]

Kibarua cha Nooij shakani

ABDUCADO EMMANUEL NA MWALI IBRAHIM, DAR

KOCHA Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania, ‘Taifa Stars’, Mart Nooij raia wa Uholanzi, yupo shakani kuendelea kukinoa kikosi hicho kutokana na matokeo mabaya aliyopata kwenye michuano ya Kombe la Cosafa.

Stars imeambulia vipigo kwenye mechi mbili za awali za Kundi B la michuano hiyo na timu ndogo Swaziland (1-0) na Madagascar (2-0), leo itamalizia ratiba kwa kuchuana na Lesotho iliyoko juu yake.

Habari za ndani zilizoifikia MTANZANIA jana zimeeleza kuwa, baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), hawaridhishwi na mwenendo wa kikosi hicho tokea Mholanzi huyo alipokabidhiwa mikoba hiyo Aprili mwaka jana akimrithi Mdenish, Kim Poulsen.

“Kila siku timu ya Taifa imekuwa ikipanda na kushuka na tumeshindwa kukaa kwenye mwelekeo mmoja, matokeo tuliyopata Cosafa ndiyo yameharibu kila kitu na kibarua chake kitajadiliwa mara baada ya timu kurejea Dar es Salaam mwishoni mwa wiki hii,” alisema.

Habari hizo zilizidi kueleza kuwa suala la upangaji kikosi na uhitaji wa kikosi hicho, nalo limewachukiza baadhi ya wajumbe na wengi wanajiuliza ataweza mtihani wa kuiongoza Stars kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika (Afcon) 2017 na ile ya Wachezaji wa Ndani (CHAN) mwakani.

Nooij amelalamikiwa na wadau wengi wa soka nchini kwa uamuzi wake wa mara kwa mara wa kuteua kikosi kinachojirudia, wakiwemo wachezaji wanaokaa benchi huku akiwafungia vioo baadhi waliong’ara kwenye klabu zao.

Hata hivyo, taarifa iliyotumwa jana na TFF imeeleza kuwa, Kamati hiyo itakutana Jumapili hii kwenye kikao cha kawaida, huku moja ya ajenda ikiwa ni kupokea na kujadili mwenendo, maandalizi na maendeleo ya timu za Taifa za Tanzania ikiwemo Stars.

Mara baada ya kipigo dhidi ya Madagascar, Nooij alinukuliwa na kituo cha televisheni cha Supersports 9 akieleza kuwa: “Tumefungwa kama tulivyofungwa na Swaziland, kwangu mimi sio jambo kubwa, nimekuja kwenye michuano hii kwa ajili ya maandalizi ya CHAN na Afcon, nimekuja huku bila baadhi ya wachezaji wangu muhimu ambao wamepata majeruhi.”

Makocha wafunguka

Kocha Msaidizi wa Yanga, Charles Mkwasa, amesema tatizo linaloiangusha timu hiyo linaanzia kwenye uteuzi wa kikosi, baadhi ya wachezaji walioitwa ni majeruhi hivyo kocha alipaswa kuwasiliana kwanza na makocha wa timu walizotoka ili kuweza kupata taarifa zao kabla ya kuwaita.

“Wachezaji wamechezeshwa nafasi si zao hivyo kushindwa kuzimudu, wengine wamekuwa wakicheza kipindi cha pili kwenye klabu zao, lakini kwenye timu hiyo ya Taifa ndio wamechaguliwa kikosi cha kwanza na kucheza muda mrefu, hivyo lazima watafanya vibaya,” alisema.

Aliongeza hata wachezaji nao hawakuwa makini uwanjani, kwani walikuwa wakicheza utadhani hawataki ushindi licha ya kupangwa na timu dhaifu, jambo ambalo liliifanya Stars kuonekana dhaifu zaidi ya vibonde hao.

Naye Kocha Mkuu wa Mbeya City, Juma Mwambusi, amesema ufike wakati wa TFF kuthamini na kuheshimu mchango wa makocha wazawa na kuondoa fikra mgando kuwa wazawa hawawezi na kuthamini wageni pekee, huku akihoji mbona kwenye ligi wamekuwa wakizifunga timu zenye makocha wa kigeni.

“Pia ni vigezo gani alivyotumia kuita timu kama mchezaji kwenye timu yake anakaa benchi, anawezaje kuitwa timu ya Taifa hujiulizi kwanini amekuwa hatumiki kwenye kikosi chake, ipo haja ya kufanya mabadiliko kwani hali hii ni aibu kwa nchi, huku akiwataka wadau wa soka kuweza kumpa mawazo Rais wa TFF (Jamal Malinzi) kama alivyoomba,” alisema.

Kocha wa JKT Ruvu, Fred Minziro, alisema kocha huyo anapaswa kubadilisha timu hiyo aliyoikariri kila mara anapoiita, amedai bila kufanya hivyo itaendelea kupata matokeo mabaya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles