27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Sakata la Mo: Polisi wamuhoji Makamba kwa dakiaka 30 

*Lema naye ahojiwa Arusha, Msumbiji wazungumzia gari lililohusika kwenye utekaji

Na ANDREW MSECHU



SIKU mbili baada ya mfanyabiashara maarufu nchini, Mohamed Dewji (Mo) kuachiwa huru na watekaji nyara waliomshikilia kwa siku tisa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Muungano na Mazingira, January Makamba, amehojiwa na polisi kuhusu tukio hilo.

Mbali na Makamba, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema naye jana alihojiwa na polisi jijini Arusha.

Mo alitekwa nyara na watu wasiojulikana alfajiri ya Alhamisi, Oktoba 11 alipowasili katika kituo cha mazoezi cha Hoteli ya Colosseum iliyoko Oysterbay, Dar es Salaam na alirejeshwa na kutelekezwa katika eneo la viwanja vya Gymkhana, alfajiri   Oktoba 22.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, aliliambia gazeti hili jana kuwa walimuhoji Makamba kwa takriban dakika 30 kuhusiana na suala la Mo.

“Tulimwita Makamba atupe ufafanuzi wa mambo kwenye kesi ya Mo, yeye siyo mshtakiwa wala mshukiwa na hakukamatwa kama ambavyo baadhi ya watu wanadai, tulihitaji habari kwake akaja, akatupa tukamalizana naye,” alisema Mambosasa.

Alieleza huenda taarifa zinazozagaa ni kwa sababu Makamba ni mtu maarufu na ni waziri.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Makamba alisema alipigiwa simu na polisi ambao walitaka kujua kama kuna kitu cha ziada ambacho Mo alizungumza naye tofauti na kile alichoeleza polisi.

“Mimi sikukamatwa, polisi walinipigia simu tu na tukaongea kirafiki kabisa, tulikaa nao maeneo ya Mtukazungumza na baadaye wakaniambia kuna vitu inatakiwa niende kusaini kwenye Kituo cha Polisi Mburahati.

“Kwanza walinisindikiza kabisa na eskoti, kwahiyo nashangaa sasa hao wanaosema nilikamatwa,” alisema Makamba.

Pia kupitia ukurasa wake wa Twitter, Makamba alikiri kuhojiwa na polisi baada ya taarifa kusambaa kwenye mitandao ya jamii zikieleza kuwa alikamatwa na kuhojiwa na polisi.

Majira ya saa 3.07 asubuhi ya jana aliandika; “Sijakamatwa na polisi. Niko salama.”

Ilipofika saa 4.48 asubuhi, Makamba aliandika tena; “Ufafanuzi: Polisi walinipigia simu kuniomba kama rafiki wa @moodewji, niwasaidie kama kuna chochote cha ziada ambacho Mo aliniambia kinachoweza kusaidia uchunguzi. Niliwaeleza. Wakasema kinafanana na alichowaeleza. Wakanishukuru. Wamefanya hivi pia kwa wanafamilia. Sikukamatwa.”

Tangu kutekwa kwa Mo, Makamba amekuwa akitoa taarifa mbalimbali kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Oktoba 11 saa 2:36 asubuhi, Makamba aliandika katika ukurasa wake wa Twitter; “Nimezungumza na baba yake @moodewji. Habari za kutekwa kwa rafiki yetu Mo ni za kweli. Nimetikiswa sana. Naamini polisi watatoa taarifa kamili. Mohammed ana familia na watoto wadogo. Tumuombee yeye na familia yake. Tusaidie kutoa taarifa zitakazosaidia kupatikana kwake.”

Oktoba 16  saa 3:12 asubuhi, Makamba aliandika; “I hope they are at least allowing you to pray. See you soon.” Tafsiri nyepesi ya Kiswahili: “Natumaini wanakupa hata nafasi ya kusali. Natarajia kukuona punde.”

Oktoba 18 saa 6:06 mchana, aliandika; “When the person who you say is your friend is still missing, there should be some moderation in your display of celebration of your life.” Tafsiri nyepesi ya Kiswahili inaweza kuwa; “Iwapo mtu unayemjali kuwa rafiki yako hajulikani alipo, furaha yako katika maisha inaweza kuwa na walakini kidogo.”

Baada ya Mo kupatikana, Makamba pia alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kutoa taarifa za kupatikana kwake.

Wakati ikidaiwa Mo alitelekezwa na watekaji wake saa 8.00 usiku, ilipofika saa 9.50 alfajiri Makamba aliandika; “Mohammed Dewji amerudi nyumbani salama. Nimezungumza naye kwa simu dakika 20 zilizopita. Sauti yake inaonyesha yu mzima bukheri wa afya. Shukrani kwa wote kwa dua na sala. Naenda nyumbani kwake kumuona muda huu.”

Hakuishia hapo, saa 10:51 alfajiri Makamba aliendelea; “Nimemuona na kuongea kwa kirefu na Mohammed Dewji. Ni mzima wa afya isipokuwa ana alama za kufungwa kamba mikononi na miguuni. Mnamo saa nane usiku, watekaji waliamua kumtupa kwenye maeneo ya viwanja vya Gymkana. Naamini polisi watatoa taarifa za ziada kuhusu kilichojiri.”

 

MO ASHUKURU MUNGU KUOKOA MAISHA YAKE

Jana saa 12:23 jioni, kupitia ukurasa wake wa Twitter, Mo aliandika; “Nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kuokoa maisha yangu. Pamoja na kupitia kipindi kigumu lakini daima amesimama upande wangu. Marafiki zangu napenda kuwashukuru wote kwa maombi yenu na kunitakia kheri. Mungu awazidishie kwa wema wenu. Baraka za Mungu ziwe nanyi leo na daima.”

Mara ya mwisho kwa mfanyabiashara huyo kuandika kwenye twitter ilikuwa ni Oktoba 10 ambako aliandika masuala ya wanafunzi kufundishwa masuala ya kubajeti.

 

LEMA KITANZINI

Naye Lema jana aliripoti Kituo Kikuu cha Polisi mkoani Arusha kufuatia wito wa polisi uliomtaka kufika bila kukosa.

Lema aliripoti polisi saa 4:55 asubuhi akiwa katika gari ya Mercedes Benz ya zamani na kuliegesha ndani ya eneo la polisi, lakini akatakiwa kuliondoa na kuliegesha nje.

Baada ya kushuka aliingia polisi akiongozana na Katibu wa Chadema Mkoa wa Arusha, Elisa Mungure, mkewe Neema na Ofisa Habari wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Muzeki Joseph.

Mbunge huyo alihojiwa kwa saa kadhaa kabla ya kutoka na kupitia ukurasa wake wa Twitter aliandika; “Polisi wameniuliza maswali juu ya utekwaji wa Mo. Nimesema kutekwa kwa Mo na kupatikana kwake kumeacha wasiwasi mwingi. Naamini kama Biblia ingekuwa bado inaandikwa pengine suala hili lingeandikwa kama muujiza.”

Taarifa ya kuitwa polisi pia aliitoa kupitia Twitter juzi saa 11: 45 jioni ambapo aliandika; “Nimepigiwa simu na polisi kwamba natakiwa kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi Arusha kesho bila kukosa, sijaelezwa sababu lakini wito unaonekana kuwa wa lazima sana, lakini nafikiri kupigania haki ndiyo linaweza kuwa kosa langu kubwa. MSIOGOPE.”

Akizungumza na MTANZANIA kuhusu wito huo, Lema alisema aliupata juzi akiwa njiani kuelekea Arusha, wakimtaka aripoti Kituo Kikuu Arusha haraka vinginevyo wangetumia nguvu kumkamata.

“Nimepata taarifa za wito na wanasisitiza nifike leo (juzi) na mimi muda huu ndio ninaingia Arusha, kwa hiyo lazima nionane kwanza na wakili wangu ili kujua namna nitakavyokwenda kwao (polisi). Sababu za kuitwa polisi ninaona ni vita baina ya nuru na giza,” alisema.

Lema alikuwa mstari wa mbele katika kampeni ya mtandaoni ya kutaka kurejeshwa kwa Mo, ambako katika baadhi ya maandiko yake kwenye Twitter, muda mfupi baada ya kupatikana kwa Mo, Oktoba 20 aliandika; “Imani kwa vyombo vya usalama inajengwa na haki.

“Ushujaa siyo kutoa amri bali ni uwezo wa kubeba kweli, haki na uadilifu katika wajibu. Suala la Mo kutekwa mpaka kupatikana limejaa wasiwasi. Kama MB (Mbunge) nitaongea na niko tayari kulipa gharama kwani mambo haya yakiendelea ni hatari kwa nchi.”

Muda mfupi baada ya mazungumzo ya Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Simon Sirro na wanahabari Ijumaa Oktoba 19, Lema aliandika; “Nilimsikiliza Mambosasa. Leo nimemsikiliza IGP Sirro katika mkutano wake na waandishi, IGP ameacha maswali mengi yanayoumiza na kuleta hofu kubwa katika jamii. Kama Waziri Kivuli nitachambua hotuba yake na kuongea na waandishi wa habari katika muda sahihi. Poleni sana familia ya Mo Dewji.”

Hata hivyo, Lema aliahirisha mkutano wake Jumamosi Oktoba 20 baada ya taarifa za kupatikana kwa Mo akieleza kuwa ataufanya siku zijazo baada ya kupata picha kamili kuhusu namna alivyotekwa na namna alivyorejeshwa.

 

UBALOZI WA MSUMBIJI WATOA NENO

Baada ya namba za gari lililodaiwa kumteka Mo kufanana na zile za magari ya Msumbiji, jana Ubalozi wa Msumbiji nchini ulisema hauwezi kuzungumzia tukio hilo kwa kuwa haujapata taarifa rasmi tofauti na kuzisikia tu kwenye vyombo vya habari.

Gari inayodaiwa kuhusika kwenye tukio la utekeji ni Toyota Surf ambayo IGP Sirro alisema ilivuka mpaka wa nchi moja jirani (ambayo hakutaka kuitaja) Septemba mosi ikiwa na namba AGX 404 MC ambazo uchunguzi wa MTANZNAIA ulibaini kuwa mfumo huo wa namba hutumika Msumbiji.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Ofisa wa Ubalozi wa Msumbiji nchini, Maria Miceli alisema kwa sasa hawezi kuzungumza lolote kuhusu suala hilo kwa kuwa hata wao wamesikia tu na kuona kupitia vyombo vya habari.

“Kuhusu kama tumeombwa kutoa ushirikiano kuhusiana na suala hilo, kwa sasa hatuwezi kuzungumza lolote kwa kuwa hata sisi tumesikia tu na kuona kupitia vyombo vya habari,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles