26.1 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

SAFARI YA YANGA LIGI YA MABINGWA AFRIKA 2017

YANGA ambao ni wawakilishi wa Tanzania Bara katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, mwishoni mwa wiki hii watashuka dimbani kutupa karata yao ya kwanza ugenini dhidi ya Ngaye De Mbe ya visiwa vya Comoro.

Yanga mwaka huu watashiriki michuano hiyo wakiongozwa na kocha mpya, George Lwandamina, aliyetokea Zesco United ya Zambia, huku ikikumbukwa mwaka jana wakiwa chini ya Hans van der Pluijm, waliishia hatua ya robo fainali na kupewa nafasi ya kucheza Kombe la Shirikisho.

Hata hivyo, Pluijm hakuweza kufanikisha ndoto za timu hiyo kung’ara kimataifa, kwani haikuweza kuvuna chochote katika Kombe la Shirikisho na kujikuta wakitolewa katika hatua za awali.

Rekodi ya Lwandamina kuwabeba

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, watatumia uzoezi wa Lwandamina katika michuano ya kimataifa, ambapo rekodi yake ni kuifikisha Zesco hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka jana.

Lwandamina amekuwa na sifa nzuri ya kutoa vipigo, hasa kwa timu za Waarabu, ambapo katika michuano iliyopita akiwa na Zesco, aliiwezesha kuvuka kundi A lililokuwa na timu ngumu kama Al Ahly ya Misri, Wydad Casablanca ya Morocco na Asec Mimosas ya Ivory Coast.

Licha ya maandalizi ya mechi za kimataifa kutoridhisha, Yanga inapewa nafasi ya kufika fainali kwenye mashindano ya kimataifa msimu huu kupitia mgongo wa kocha huyo raia wa Zambia.

Ugeni wa Ngaye De Mbe

Kwenye mchezo wa kwanza Yanga inatabiriwa kusonga mbele kutokana na wapinzani wao kutokuwa na rekodi ya kufanya vizuri katika michuano mbalimbali ya kimataifa.

Uzoefu wa Yanga unatarajiwa kuwa ni kipimo kwa Ngaye De Mbe, ambayo inashiriki michuano hii kwa mara ya kwanza, baada ya kunyakua taji la Ligi Kuu nchini Comoro.

Ngaye De Mbe ambayo kwa sasa ni bingwa mtetezi wa Ligi ya Comoro, kwenye historia yake imeweza kutwaa mataji mara nne, ambapo msimu uliopita iliweza kuivua ubingwa wa ligi hiyo timu ya Volcan Club de Moroni.

Timu hiyo inayonolewa na Lucien Sylla Mchangama, imeweza kujizolea mataji ya ligi za ndani mara nne, ambapo baadhi yake ni Kombe la Ligi Ngazija, Ligi Kuu ya Ngazija na Ligi Kuu ya Comoro.

Kikosi bora Yanga

Mbali na rekodi safi ya Lwandamina, Yanga inapewa nafasi ya kushinda mchezo huo wa awali kutokana na ubora wa kikosi ambacho kinaundwa na nyota kutoka mataifa saba tofauti, Togo, Rwanda, Zimbabwe, Burundi, Tanzania na Zambia huku wapinzani wao wakiwa ni timu yenye asilimia kubwa ya wachezaji wazawa.

Mbali ya kuwa na nyota kutoka mataifa saba, gharama za usajili zilizotumiwa na Yanga zina utofauti mkubwa na klabu ya Ngaye De Mbe.

Mara nyingi Yanga imekuwa ikijizolea sifa kubwa kwa kila mwaka kushiriki michuano ya kimataifa, kutokana na juhudi ambazo zimekuwa zikionyeshwa na wachezaji wake wa ndani na nje ya nchi.

Wachezaji wenye majina na uzoefu wa mashindano ya kimataifa katika klabu hiyo, wamekuwa wakitumiwa kama njia mojawapo ya kufanikisha mafaniko ya timu hiyo.

Mwaka huu Yanga inapewa nafasi ya kusonga mbele, baada ya kuwa na kikosi bora kile kile kilichoiwezesha kutinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho, huku kikiongezewa nguvu na Lwandamina.

Historia yao kimataifa

Hii ni mara ya tatu kwa Yanga kupangiwa timu ya Comoro, kwani mwaka 2009 ilicheza na Etoile d’or de Mirontsy na kuifunga jumla ya mabao 14-1, mwaka 2010 ikaitoa Komorozine kwa mabao 12-2.

 

Licha ya kufanikiwa kupata nafasi ya kushiriki michuano hiyo na ile ya Kombe la Shirikisho, mara nyingi Yanga imekuwa ikishindwa kupiga hatua za mbali na kujikuta ikitolewa.

Yanga wanashiriki michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara 25, huku wakiwa wamefanikiwa kutinga hatua ya makundi mara moja na raundi nyinginezo wakiishia kwenye hatua za awali na ikizidi sana raundi ya pili na hasa inapokutana na timu kutoka Kaskazini na Magharibi mwa Afrika.

Mabingwa hao mara 26 wa Ligi Kuu Tanzania Bara, wamekuwa wakizinyanyasa timu ndogo wanazopangiwa nazo hatua ya awali kutoka Comoro, Botswana au Zimbabwe, lakini safari yao hufikia ukingoni pale wanapokutana na miamba ya soka la Afrika.

Mwaka 2012, Yanga iliaga mapema ligi ya mabingwa, ambapo mchezo wa raundi ya kwanza walipangiwa na klabu ya Zamalek ya Misri na kujikuta wakiambulia kipigo cha jumla ya mabao 2-1 katika mechi zote mbili.

Kabla ya fainali za mwaka jana, mara ya mwisho timu hiyo kushiriki ligi ya mabingwa ilikuwa ni 2014 ilipotolewa na National Al Ahly kwa changamoto ya mikwaju ya penalti, baada ya kutoka sare ya mabao 1-1, Yanga wakishinda bao 1-0 nyumbani na katika mchezo wa marudiano Al Ahly nao wakashinda 1-0 na kuamuriwa zipigwe penalti.

Awali Yanga iliitoa Komorizone ya Comoro, kwa idadi kubwa ya mabao, mchezo huo ulimpa tuzo ya ufungaji bora aliyekuwa winga wa kikosi cha Wanajangwani hao, Mrisho Ngasa ambaye alifunga ‘hart trick’ mbili kwenye mechi zote mbili.

Baada ya hapo msimu uliofuata Yanga ilikosa ubingwa ikamaliza msimu nafasi ya pili, ambapo ilishiriki Kombe la Shirikisho na kujikuta ikiondolewa na Etoile du Sahel kwa mabao 2-1.

Katika michuano ya Kombe la Shirikisho, Yanga ilianza vizuri kwa kuwatoa BDF XI ya Botswana, baada ya hapo ikapangiwa FC Platinum ya Zimbabwe lakini ilipokutana na Etoile du Sahel ikasukumwa nje ya michuano kwa mara nyingine.

Mwaka jana Yanga ilishiriki tena ligi ya mabingwa na kuondolewa mashindanoni, baada ya kukubali kichapo cha jumla ya mabao 3-2 dhidi ya Al Ahly.

Mchezo wa kwanza uliopigwa kwenye dimba la Taifa, Dar es Salaam timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 kabla ya Yanga kukubali kichapo cha mabao 2-1 ugenini.

Kutolewa katika michuano ya klabu bingwa, kuliipa nafasi Yanga ya kuungana na Azam katika Kombe la Shirikisho.

Hata hivyo, bahati haikuwa yao kwani licha ya kupambana vilivyo, ilitolewa katika hatua ya robo fainali baada ya kuburuza mkia kwenye kundi A.

Kutolewa kwao huko kuliwanyima nafasi ya kusonga mbele ili kwenda kuivunja rekodi ya Simba, ambayo ilifika fainali ya CAF mwaka 1993 na kufungwa mabao 2-0 Uwanja wa Taifa, ikiwa ni baada ya kutoka sare ya bila kufungana Abidjan, Ivory Coast na Stella Artois.

Makala hii imeandaliwa na ZAINAB IDD, JENNIFER ULLEMBO -DAR ES SALAAM

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles