30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

ATHUMANI CHIUNDU; NIDHAMU INAUBEBA MCHEZO WA GOFU

Na SHARIFA MMASI-DAR ES SALAAM

UNAUKUMBUKA ule msemo wa Kiswahili usemao ukitaka kazi ya jeshi lazima ugangamale? Kumbe msemo huo sio jeshini tu, hata kwenye mchezo wa gofu kwasababu bila nidhamu na kujituma mambo yanakuwa magumu.

Kwa siku za hivi karibuni, gofu imekua miongoni mwa michezo inayoendelea kujizolea mashabiki wa kila rika.

Ukiacha watu wazima ambao wamekuwa wakiutumia mchezo huo kama sehemu ya kulinda afya za miili yao, lakini pia kumekuwa na ongezeko la chipukizi wanaojitokeza kutaka kujifunza mchezo huo.

Ongezeko la wachezaji hao wachanga wanaojifunza mchezo huo limekuwa likiwapa kazi kubwa makocha katika kufikia malengo kutokana na changamoto mbalimbali wanazopitia.

MTANZANIA lilifanya mahojiano na kocha wa watoto chini ya umri wa miaka 18 katika klabu ya Gofu ya Lugalo iliyopo jijini Dar es Salaam, Athuman Chiundu, aliyezungumzia mambo mbalimbali yanayohusiana na mchezo huo.

Chiundu anasema alianza rasmi kufundisha watoto kucheza gofu katika klabu ya Lugalo mwaka 2015 huku akiwa na jumla ya wachezaji tisa; wavulana watano na wasichana wanne.

“Mwaka 2015 ndio nilianza rasmi kufundisha watoto mchezo wa gofu katika klabu ya Lugalo, kipindi naanza nilikuwa na watoto tisa tu, wanawake walikuwa wapo wanne na waliobaki ni wanaume.

Chiundu anasema klabu hiyo kwa sasa ina jumla ya wachezaji 36 anaoendelea kuwapa mafunzo hadi watakapofikia hatua ya kupanda daraja na kupewa kibali cha kuwa wachezaji wa kulipwa (professionals).

“Kwa sasa nina jumla ya wachezaji 36 ninaowanoa ambapo mipango yangu mikubwa ni kuhakikisha wote kwa pamoja wanafikia hatua ya kuwa wachezaji wa kulipwa kama nilivyo mimi mwalimu wao.

Anasema changamoto kubwa anayokumbana nayo kwa watoto anaowafundisha ni uhaba wa vifaa na hiyo ni kutokana na kuwategemea wadhamini mbalimbali.

“Vifaa ni moja ya changamoto kubwa inayoendelea kuniumiza kichwa mimi kama mwalimu wao, kama mnavyojua tabia za watoto kuna wakati wanafurahi wakijiona wamependeza na jezi zao za kufanana kipindi cha mazoezi lakini kwa sasa hilo ni tatizo kwetu.

“Mipira ya kuchezea pamoja na fimbo zake ni janga kwa baadhi ya wachezaji, gharama zake ndiyo zinapelekea wazazi kushindwa kuwanunulia watoto wao na hii husababisha kugeuka ‘ombaomba’ kwa wenzao ambapo wakati mwingine husababisha kero.

Akizungumzia suala la nidhamu kwa wachezaji anaowafundisha, anasema ni kitu kikubwa kinachotiliwa mkazo kuanzia uongozi wa juu wa klabu hiyo hadi yeye kocha mwenyewe.

“Nidhamu ni kitu pekee kinachopewa mkazo ndani ya klabu ya Lugalo bila ya kujali rika ya mchezaji.”

Chiundu anasema upande wake mchezaji yeyote mwenye utovu wa nidhamu, anampa adhabu ya kucheza kwenye viwanja vitatu ambapo atahitajika kupata alama nne katika kila kiwanja kimoja bila kukosea.

“Moja ya adhabu ninayowapa wachezaji wangu pindi wanapokosea ni kuhakikisha wanacheza viwanja vitatu na kila kimoja atalazimika kupata alama nne na kama hatafanikisha zoezi hilo, atalazimika kupiga mipira 100 kutoka mita moja hadi 100 za kiwanja.

“Ninapoona mchezaji kafanikisha hilo na bado nidhamu yake mbovu, sina budi kumfuta kabisa katika klabu yangu ili kuwa mfano wa wengine wenye tabia kama hiyo,” anasema Chiundu.

Akizungumzia suala la maendeleo ya watoto hao, anasema yanaridhisha kwani hadi sasa wachezaji wawili wamefuzu vema kuchezea viwanja 18, huku akidai wakiendelea na mbio hizo, watapata kibali cha kuwa wachezaji wa kulipwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles