24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Safari ya Simba SC hadi robo fainali Afrika ilianzia hapa

BADI MCHOMOLO-DAR ES SALAAM

SIMBA SC imeandika historia mpya nchini kwenye michuano ya Klabu Bingwa Barani Afrika baada ya kuingia hatua ya robo fainali baada ya ushindi wa juzi wa mabao 2-1 dhidi ya AS Vita Club ya nchini Congo.

Simba SC imeshiriki michuano hiyo msimu huu baada ya kufanya vizuri kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita na kutwaa ubingwa.

Hivyo safari ilianzia hapo kwa timu mbili za Tanzania kushiriki michuano ya Caf, huku Mtibwa Sugar kutoka Tanzania Bara ikishiriki michuano ya Kombe la Shirikisho pamoja na Zimamoto kutoka Zanzibar.

Hata hivyo timu hizo mbili kwenye michuano hiyo ya Kombe la Shirikisho hazikuweza kufika mbali zikajikuta zikitolewa na kubakia Simba SC kwenye michuano hiyo mikubwa ya Klabu Bingwa.

Haikuwa kazi rahisi kwa Simba SC klabu kuweza kufika hapo, lakini kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na mfanya biashara Mohammed Dewji, umesaidia kw akiasi kikubwa timu hiyo kufika hapo.

SPOTIKIKI leo imekuanikia safari hiyo yote kwa timu walizokutana na Simba SC na matokeo yake ambayo yamewavusha kwa kuwaondoa vigogo Afrika.

Simba SC vs Mbabane Swallows

Huu ulikuwa mchezo wa kwanza kwenye michuano hiyo ambapo Simba SC walikuwa kwenye uwanja wa nyumbani jijini Dar es salaam na kuwakaribisha wapinzani wao kutoka Eswatini.

Kutokana na kuonesha kwamba wamejiandaa vizuri, waliweza kushinda mabao 4-1, yaliyowekwa wavuni na John Bocco akifunga mabao mawili, huku mabao mengine yakifungwa na Meddie Kagere na Clatous Chama, wakati huo bao la Mbabane likifungwa na Stevy Nzambe. Mchezo huo ulipigwa Novemba 28 mwaka jana.

Marudiano ilikuwa Desemba 4, 2018, ambapo Simba walikuwa wageni, lakini kutokana na ubora wao waliweza kutamba na ugenini kwa ushindi wa mabao 4-0.

Chama alifunga mabao mawili, huku mabao mengine yakiwekwa wavuni na Kagere pamoja na Emmanuel Okwi na kuwafanya Swallows washindwe kusonga mbele kutokana na jumla ya kichapo cha mabao 8-1.

Nkana vs Simba

Hii ilikuwa Desemba 15, Simba walikuwa ugenini na wakakubali kichapo cha mabao 2-1, mabao ya Nkana yalifungwa na Ronald Kampamba na Kelvin Kampamba, wakati bao la pekee la Simba likifungwa na Bocco.

Desemba 23, Simba walikuwa kwenye uwanja wao wa kujidai wakati wakirudiana na Nkana, hivyo kwenye uwanja huo jijini Dar es salaam mgeni anakuwa hayupo salama, hivyo Nkana alikubali kichapo cha mabao 3-1, mabao yaliyofungwa na Jonas Mkude, Kagere na Chama katika dakika za lala salama huku bao la Nkana likifungwa na Walter Bwalya.

Hivyo Nkana ikayaaga mashindano kutokana na kichapo hicho cha jumla ya mabao 4-3.

Simba wakaingia hatua ya makundi, ambapo kundi lao lilikuwa D, ambapo timu zake ni Al Ahly, JS Saoura na AS Vita Club.

Simba walitabiriwa kuwa vibonde kwenye kundi hilo kutokana na uzoefu wa timu zingine, lakini wakaweza kuziba midomo ya watu hao kwa kufanya vizuri na kuingia hatua ya robo fainali, huku kila kundi likiingiza timu mbili, hivyo Simba na Al Ahly wamefuzu. Safari ya hatua ya makundi ilikuwa kama ifuatavyo.

Simba vs JS Saoura

Huu ulikuwa mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi, Simba walianzia nyumbani dhidi ya JS Saoura kutoka nchini Algeria na Simba iliweza kuibuka na ushindi wa mabao 3-0, yakifungwa na Kagere mabao mawili na bao lingine likifungwa na Okwi. Huku mchezo wa marudiano Machi 9, Simba ilikuwa ugenini na kukubali kichapo cha mabao 2-0, yakifungwa na Sid Cherif na Mohamed Hammia.

Al Ahly vs Simba

Hapa walikutana na joto lingine la jiwe baada ya kuchezea kichapo cha mabao mengine 5-0, yakifungwa na Amr Elsolia, Ali Maaloul, Junior Ajayi na Karim Walid, mchezo huo ulipigwa Februari 2, lakini mchezo wa marudiano ulipigwa Februari 12 na Simba kufanikiwa kushinda bao 1-0, likifungwa na Kagere kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

AS Vita vs Simba

Simba walikuwa ugenini na kukubali kichapo cha mabao 5-0 huko nchini Congo, mabao yakifungwa na Jean-Marc Makusu akifunga mawili na mengine yakifungwa na Botuli Bompunga, Fabrice Ngoma na Makwekwe Kupa, hiyo ilikuwa Januari 19.

Marudiano ilikuwa juzi kwenye uwanja wa taifa Dar es salaam na Simba kushinda mabao 2-1 ambayo yamewapeleka moja kwa moja kutokana na idadi kubwa ya pointi.

Huu ulikuwa ni mchezo ambao ulikuwa unaamua timu ya kwenda kuungana na Al Ahly na kufuzu robo fainali kwa kuwa kila timu ilikuwa na nafasi hiyo endapo ingepata ushindi.

Simba imefanikiwa kuingia hatua hiyo baada ya kujizolea jumla ya pointi 9, kutokana na kushinda michezo yote mitatu ya nyumbani, huku ikipoteza michezo ya ugenini.

Al Ahly wamemaliza nafasi ya kwanza kwenye kundi hilo wakiwa na jumla ya pointi 10, wakati huo JS Saoura ikishika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 8 na AS Vita ikiwa na pointi 7.

Kutokana na matokeo hayo, Simba SC inaungana na timu mbili kutoka kundi A, WAC Casablanca na Mamelodi Sundowns, huku kundi B, ES Tunis na Horoya na kundi C ni TP Mazembe na CS Constantine, wakati huo kundi D ni Al Ahly na Simba SC.

Katika timu hizo zote zilizofuzu, Simba ni timu pekee yenye pointi chacha, lakini wapinzani wengine wamefuzu kwa pointi kuanzia 10 hadi 14, wakati huo Simba wakifuzu kwa pointi 9. Droo ya robo fainali inatarajiwa kuchezeshwa kesho kutwa.

Simba ni timu pekee Afrika Mashariki kuendelea kuwepo hadi hatua hiyo ya robo fainali, timu zingine zilitolewa tangu hatua ya mtoano.

Kwa hali hiyo, Simba SC ni moja kati ya timu za kuogopwa kati ya nane ambazo zimefuzu kwenye hatua hiyo.

Kila la heri Simba SC kwa hatua hiyo, safari ni ndefu lakini hakuna kinachoshindikana katika soka, kutokana na ubora walionao wanaweza kufika mbali zaidi ya hapo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles