31.8 C
Dar es Salaam
Thursday, December 12, 2024

Contact us: [email protected]

Safari ya mwisho ya Komba *Vilio vyatawala, Rais Muluzi amlilia

Francis Godwin na Amon Mtega, Nyasa

RAIS Jakaya Kikwete ameongoza Watanzania katika mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Mbinga Magharibi, Kapteni John Komba yaliyofanyika jana kijijini kwao Lituhi, Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma.

Wakati vilio na simanzi vikitawala muda wote msibani hapo, Rais mstaafu wa Malawi, Dk. Bakili Muluzi, ametuma salamu za rambirambi kwa wanafamilia na wananchi wa Mbinga Magharibi kutokana na msiba wa mbunge huyo.

Akitoa mahubiri katika ibada ya mazishi, Askofu wa Jimbo la Mbinga, John Ndimbo, aliwataka Watanzania kuacha matendo ya kumpuuza Mwenyezi Mungu, badala yake watende yaliyo mema katika maisha yao kwani hakuna binadamu aliyefunga mkataba na Mungu juu ya kuishi hapa duniani.

“Miili yetu ni hekalu la Bwana na maskani ya mpito hapa duniani, inatupasa kufanya kila jitihada kwa mambo ambayo yanampendeza Mungu, hakuna binadamu asiyekuwa na utashi juu ya kifo,” alisema Askofu Ndimbo.
Alisema kutokana na utukufu wa Mungu, ana uwezo wa kumchukua mtu ambaye binadamu walimtegemea kwa namna moja au nyingine hapa duniani, huku akisisitiza Watanzania kutenda mema.
Askofu Ndimbo, alisema Kapteni Komba alikuwa tegemeo kubwa kwa wananchi wa Wilaya ya Nyasa kupitia huduma zake alizokuwa akizitoa kwa jamii.

JK ABUBUJIKWA MACHOZI
Wakati ibada ya mazishi ikiendelea, Rais Kikwete alishindwa tena kujizuia na kujikuta akibubujikwa machozi.
Pamoja na watu wengi kuzungumza, lakini Rais Kikwete hakusema jambo lolote katika msiba huo.

RAIS MULUZI AMLILIA
Rais mstaafu wa Malawi, Dk. Muluzi, ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya Kapteni Komba.
Dk. Muluzi alituma salamu hizo jana kupitia kwa Mbunge wa Songea Mjini, Dk. Emmanuel Nchimbi.
Katika salamu hizo alizotuma kwa barua pepe na kusomwa makaburini hapo mbele ya Rais Kikwete na Ofisa wa Bunge, Saidi Yakubu, Dk. Muluzi alisema anatambua mchango mkubwa wa marehemu Komba enzi za uhai wake.
“Nimepokea taarifa ya kifo cha mbunge Komba kwa masikitiko makubwa, nipo pamoja na familia na wananchi wote wa Jimbo la Mbinga Magharibi katika maombolezo haya,” alisema Dk. Muluzi.
Komba ni mmoja kati ya watu waliomuunga mkono Dk. Muluzi na kumfanyia kampeni za urais nchini Malawi ambapo aliibuka na ushindi.
“Ninatuma salamu zangu za rambirambi kutokana na kifo cha Kapteni John Komba, nimepata habari za kifo chake ambazo zimenishtua.
“Ninamfahamu Kapteni Komba ni rafiki yangu na ninakuomba unifikishie salamu zangu za rambirambi kwa familia yake na Komba alikuwa kipenzi kwa wananchi wa Malawi,” alisema Dk. Muluzi katika ujumbe wake kwenda kwa Dk. Nchimbi.

SPIKA MAKINDA
Akitoa salamu za Bunge, Spika wa Bunge, Anne Makinda, alisema anasikitishwa na kitendo cha kuibuka kwa manabii wa uongo, ambao wameendelea kueneza uongo katika Taifa hili kwa lengo la kupandikiza chuki ili kuvuruga amani na utulivu.
Alisema manabii hao wa uongo wamekuwa wakizunguka kwa wananchi kupandikiza chuki kuhusu Katiba Inayopendekezwa kwa kudanganya umma.
“Jambo kubwa linalosumbua kwa sasa ni juu ya manabii wa uongo, ni wengi, mtu anavumisha tu jambo ambalo si la kweli.
“Nasema kwa mfano na naomba kusema kwa sababu nafsi yangu inanituma niseme suala kubwa hivi sasa linalosumbua ambalo litakuja katika Bunge na muswada tayari ninao, na lengo la muswada huo ni kufanya mabadiliko ya sheria ya Kiislamu iliyopo katika vitabu vya Kiislamu ya mwaka 1964,” alisema.
Alisema sheria hiyo ipo ila tofauti yake ni kwamba wakati wa mkoloni wao waliitambua kwa kutenga viongozi wa kushughulikia suala hilo na baada ya uhuru suala hilo lilitazamwa upya.
“Ila wataalamu na manabii wa uongo wanaeneza kuwa mambo haya yapo katika Katiba Inayopendekezwa, nawaomba sana msiwasikilize, na suala hili lilifanyiwa kazi karibu wiki tatu usiku na mchana kuona suala hilo halipo, lakini wapo watu wanaotangaza kuwa lipo, huo ni uongo na CCM ilijadiliana na makundi yote na halipo katika Katiba Inayopendekezwa,” alisema.

LOWASSA ASHIRIKI
Mbali na viongozi wa juu wa Serikali kushiriki msiba huo, wengine walioshiriki ni pamoja na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ambaye alikuwa ameongozana na Mbunge wa Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani (CCM) maarufu kwa jina la Profesa Maji Marefu.
Akiwa katika msiba huo, Ngonyani alijipambanua zaidi kuhusu urafiki wake na Lowassa na kusema kuwa kamwe hataacha kumuunga mkono popote atakapokwenda.
“Mimi na Lowassa ni marafiki wa siku nyingi, hatujaanza leo, urafiki wetu wa damu. Ni mengi amenisaidia, hivyo nipo pamoja na Lowassa kama mnavyoniona, tupo hapa kumzika rafiki yetu Komba,” alisema.

KINANA NA SALAMU
Akitoa salama za chama katika msiba huo, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, alisema amepotea kiongozi ambaye ana upendo, mchapakazi ambaue alikuwa mstari wa mbele kusaidia watu wake.

“Alhamisi iliyopita alikuja ofisini kwangu tukazungumza, akaniambia anataka kupeleka bati jimboni kwake, bahati mbaya kafariki. Tumepata pigo kubwa ndani ya chama, daima tutamkumbuka kwa upendo, uvumilivu na mchango wake mkubwa katika chama,” alisema Kinana.
Naye Mbunge wa Mbinga Mashariki, Gaudence Kayombo, akitoa salamu kwa niaba ya wabunge wa Mkoa wa Ruvuma, alisema walishtushwa na msiba huo mzito, kamwe hawatamsahau Kapteni Komba kwani alikuwa kiongozi jasiri, mkweli na mpenda wapigakura wake.

MBUNGE BARWANY
Akitoa salamu kwa niaba ya wabunge wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Mbunge wa Lindi Mjini, Salum Barwany (CUF), alisema wamepokea kifo hicho kwa masikitiko makubwa kwani marehemu alikuwa akimfariji na kuwa mstari wa mbele kupinga mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) nchini.
“Kila wakati Kapteni Komba, alikuwa akitufariji yalipokuwa yakitokea mauaji dhidi ya watu wenye albino na hata kusema ipo siku yatakwisha, huku akinitania kila mara, hasa tulipokuwa Dar es Salaam kuwa nitalindwa na nitakuwa salama wakati wote.
“Ndugu zangu wananchi, marehemu alikuwa kipenzi cha watu na hakika ni kiongozi mpenda watu, kambi ya upinzani inasikitika sana kumpoteza kiongozi huyu mahiri na shupavu,” alisema Barwany.
Wabunge wengine walioshiriki maziko hayo ni pamoja na Deo Filikunjombe wa Ludewa, ambaye alisema kifo cha Komba si pigo tu kwa wananchi wa Mbinga Magharibi, bali hata kwa Wilaya ya Ludewa.
Alisema mara kadhaa waliungana katika kuwatoa hofu wananchi wa mwambao wa Ziwa Nyasa, ambao walikuwa na hofu ya vita kutokana na chokochoko za mpaka kati ya Tanzania na Malawi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles